TAVIC yapata leseni ya kwanza ya kukusanya mirabaha ya kazi za filamu Tanzania

 Na Mwandishi wetu

Tasnia ya filamu nchini Tanzania imeingia katika hatua mpya baada ya Kampuni ya Tanzania Audiovisual Collection Ltd (TAVIC) kukabidhiwa rasmi leseni ya kuwa Collective Management Organisation (CMO) ya kwanza kwa sekta ya kazi za sauti na picha (audiovisual). Leseni hiyo inairuhusu TAVIC kukusanya na kusambaza mirabaha kwa wenye haki za kazi za filamu na maudhui mengine ya audiovisual. 

Kupatikana kwa leseni hiyo kunafuatia mchakato wa takribani miezi minne uliokuwa ukisimamiwa na Ofisi ya Hakimiliki Tanzania (COSOTA). Katika kipindi hicho, TAVIC ilitakiwa kutimiza masharti mbalimbali yaliyowekwa na mamlaka hiyo, ikiwemo kuweka dhamana ya Tsh 250 milioni, kabla ya kuidhinishwa kuanza shughuli zake rasmi. 

Hatua hiyo inaifanya TAVIC kuwa taasisi ya kwanza nchini yenye jukumu maalumu la kusimamia ukusanyaji na ugawaji wa mirabaha kwa watayarishaji wa filamu, waongozaji, waigizaji na wadau wengine wa kazi za audiovisual. 

Mfumo huo unatarajiwa kuongeza uwazi katika ukusanyaji wa mapato yanayotokana na matumizi ya kazi za filamu kupitia televisheni, majukwaa ya kidijitali, sehemu za burudani na watumiaji wengine wa maudhui hayo. 

Kwa miaka mingi, jukumu la ukusanyaji na ugawaji wa mirabaha lilikuwa likifanywa na COSOTA. Hata hivyo, marekebisho ya mfumo wa usimamizi wa hakimiliki nchini yamefungua nafasi kwa kampuni binafsi zilizopewa leseni kufanya kazi hiyo kama Collective Management Organisations, huku COSOTA ikibaki kuwa msimamizi wa utoaji wa leseni na ufuatiliaji wa shughuli zao. 

Wadau wa tasnia ya filamu wanaamini kuanza kwa shughuli za TAVIC kutasaidia wabunifu kupata stahiki zao kwa ufanisi zaidi na kuongeza thamani ya kazi za ubunifu nchini. Pia, hatua hiyo inatarajiwa kuimarisha ulinzi wa hakimiliki na kutoa motisha kwa watayarishaji kuendelea kuwekeza katika utengenezaji wa filamu zenye ubora.

Kukabidhiwa kwa leseni hiyo ni sehemu ya mageuzi makubwa yanayoendelea katika sekta ya hakimiliki Tanzania, yakilenga kuhakikisha wasanii na wabunifu wananufaika zaidi na matumizi ya kazi zao kupitia mfumo wa kisasa wa ukusanyaji na ugawaji wa mirabaha.