Guardians of the Peak wapokelewa kwa kishindo kwenye banda la HeyU Sabasaba

Na Charles Mkoka

Dar es Salaam. Timu ya Guardians of the Peak imeendelea kuvutia wadau mbalimbali baada ya kupokelewa rasmi katika banda la HeyU kwenye Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), katika tukio lililoonyesha mshikamano kati ya ubunifu, teknolojia na utalii.

Kupitia ujumbe uliotolewa na HeyU, kampuni hiyo ilieleza kufurahishwa na kuipokea timu hiyo, ikisifu uthabiti, ushirikiano na ari yao ya kuendelea kuvuka mipaka katika safari yao ya kuhamasisha uhifadhi wa mazingira na kuitangaza Tanzania kupitia simulizi za filamu.

"Baadhi ya timu hazifuatilii tu kilele, bali ndizo zinazokiweka. Tunajivunia kuwakaribisha Guardians of the Peak katika banda la HeyU Sabasaba. Asanteni kwa kutuhamasisha kupitia uthabiti, mshikamano na roho yenu isiyokata tamaa," ulieleza sehemu ya ujumbe wa HeyU.

Ziara hiyo ni sehemu ya mwendelezo wa shughuli za Guardians of the Peak katika Sabasaba 2026, ambapo timu hiyo imekuwa ikikutana na wadau, wanafunzi na wananchi kwa lengo la kuhamasisha utunzaji wa mazingira, matumizi ya nishati safi na kuitangaza Tanzania kama kitovu cha utalii na utengenezaji wa filamu.

Mradi wa Guardians of the Peak umejijengea nafasi kama mpango unaounganisha filamu za kumbukumbu (documentary), uhifadhi wa mazingira na utalii kupitia safari ya Mlima Kilimanjaro, huku ukiwakutanisha vijana, watetezi wa mazingira na taasisi mbalimbali ndani na nje ya Tanzania.

Ushirikiano kama huu unaendelea kuonyesha namna sekta ya filamu inavyoweza kushirikiana na kampuni za teknolojia na wadau wengine kuifikisha hadithi ya Tanzania kwa hadhira pana zaidi.

 Kadiri Guardians of the Peak inavyoendelea na kampeni zake za msimu wa pili, ushirikiano na wadhamini pamoja na washirika kama HeyU unazidi kuipa nguvu safari ya kutumia simulizi za filamu kama chombo cha kuhamasisha maendeleo endelevu.

Chapisha Maoni

Please Select Embedded Mode To Show The Comment System.*

Mpya zaidi Nzee zaidi