Filamu kuwa nyenzo muhimu kuelekea siku ya Kiswahili Duniani


 Na Charles Mkoka

Wakati maandalizi ya Kongamano la Pili la Kiswahili la Kimataifa yakipamba moto kuelekea kufanyika jijini Paris, Ufaransa kuanzia Julai 4 hadi 7 mwaka huu, sekta ya filamu imetajwa kuwa miongoni mwa nyenzo muhimu zinazochangia kuikuza na kuisambaza lugha ya Kiswahili duniani.

Katibu Mtendaji wa Bodi ya filamu nchini, Dkt. Gervas Kasiga, amesema filamu za Kitanzania zimekuwa daraja muhimu la kuifikisha lugha hiyo kwa mamilioni ya watazamaji katika nchi mbalimbali za Afrika na kwingineko duniani.

Kwa mujibu wa Dkt. Kasiga, umaarufu wa filamu za Kiswahili pamoja na ukuaji wa majukwaa ya kidigitali umeongeza kasi ya usambazaji wa lugha hiyo nje ya mipaka ya Tanzania.

Kongamano hilo litafanyika katika makao makuu ya UNESCO jijini Paris na linatarajiwa kukutanisha wataalamu wa lugha, wasomi, viongozi wa serikali, wabunifu wa maudhui na wadau wa utamaduni kutoka mataifa mbalimbali.

Kiswahili kinaendelea kupata hadhi kubwa kimataifa tangu UNESCO ilipotangaza Julai 7 kuwa Siku ya Kiswahili Duniani mwaka 2021, hatua iliyokifanya kuwa lugha ya kwanza ya Kiafrika kutambuliwa kwa siku maalumu ndani ya mfumo wa Umoja wa Mataifa.

Kwa mujibu wa UNESCO, Kiswahili kinazungumzwa na zaidi ya watu milioni 200 duniani na kinaendelea kuwa moja ya lugha zinazokua kwa kasi zaidi barani Afrika, kikitumika kama daraja la mawasiliano katika Afrika Mashariki, Kati na Kusini.

Wadau wa filamu wanaamini kuwa pamoja na fasihi, muziki na elimu, filamu imeendelea kuwa moja ya nguzo muhimu zinazochangia kuifanya lugha ya Kiswahili kuwa sehemu ya mazungumzo ya kimataifa, huku Tanzania ikiendelea kujitangaza kama kitovu cha uzalishaji wa maudhui ya Kiswahili duniani.

Chapisha Maoni

Please Select Embedded Mode To Show The Comment System.*

Mpya zaidi Nzee zaidi