Na Mwandishi wetu
Tamthilia maarufu ya Jumba la Dhahabu inatarajiwa kurejea kwa msimu mwingine, baada ya uthibitisho kutoka kwa muandaaji na mwongozaji wake, Tuesday Kihangala.
Akizungumza kuhusu maandalizi hayo, Kihangala amesema msimu huu mpya unakuja kwa ubora wa kimataifa, huku ukihusisha mchanganyiko wa wasanii wakongwe na kizazi kipya cha filamu.
Mr. Chuz ambaye pia aliigiza katika tamthilia hio pendwa amesema kuwa amewapa nafasi mastaa wapya ambao hawakupata fursa katika msimu uliopita.
“Wasanii tunaowatumia ni wa kiwango cha hali ya juu. Tunahusisha wakongwe, vijana, na sura mpya kabisa. Ni msimu mkubwa na wa aina yake,” alisema Kihangala.
Hata hivyo, hakufichua ni kituo gani kitakachorusha tamthilia hiyo, akibainisha kuwa nguvu nyingi kwa sasa zinaelekezwa kwenye utengenezaji na maboresho ya msimu huo mpya.
Tamthilia hiyo inashutiwa katika maeneo mbalimbali nchini kwa kutumia kamera za kisasa za kimataifa kama RED na Black Magic, ili kuhakikisha inabeba hadhi ya kimataifa.
“Lengo letu ni kutokumuangusha mtazamaji. Msimu wa kwanza ulioneshwa ndani na nje ya nchi, ikiwemo Kenya, Uganda na kisha kupelekwa DSTV. Safari hii ubora ndio nguzo kuu zaidi,” aliongeza Kihangala.
Kwa mujibu wake, msimu huu mpya umejikita pia katika kuhamasisha utalii wa ndani kwa kushuti katika mikoa tofauti ikiwemo Tanga, Arusha, Tabora na Dodoma.
Wadau wa filamu wameipokea habari hiyo kwa furaha wakisema ni hatua kubwa katika kukuza sekta ya filamu nchini, hasa kutokana na mchango wa Jumba la Dhahabu katika kuinua vipaji na kutoa burudani kwa vizazi vyote.
“Hii siyo kuhusu mimi, bali ni kiu ya mashabiki. Maoni yao yamekuwa yakiongezeka kila siku, ndiyo maana niliunda timu ya wataalamu kuhakikisha tunakonga nyoyo za wengi,” alisisitiza Kihangala.
Tamthilia hiyo inatarajiwa pia kusambazwa kwenye majukwaa ya kimataifa ya streaming, ambayo yatatajwa rasmi mara tu maandalizi yatakapokamilika.
.jpg)