Na Mwandishi Wetu
Maandalizi ya Tamasha la Tuzo za Filamu mkoani Iringa yanaendelea kwa kasi, huku wasanii wakongwe wa filamu wakijitokeza kwa nguvu kuhamasisha na kunadi tukio hilo kubwa la kisanaa.
Katika kampeni za kuhamasisha wadau kupitia video maalum, msanii mkongwe Single Mtambalike, anayefahamika zaidi kama 'The Gentleman' Richie Rich, amewataka wafadhili, wadau wa filamu na wananchi kwa ujumla kujitokeza kusapoti tuzo hizo, akisisitiza umuhimu wake katika kukuza tasnia ya filamu nchini.
Tuzo hizo zinatarajiwa kufanyika mwezi Desemba mwaka huu, ambapo hadi sasa wasanii na vikundi mbalimbali vya sanaa wanaendelea kuwasilisha kazi zao kwa ajili ya kushindanishwa.
Naye nguli wa filamu Jacob Steven ‘JB’, alisema tuzo hizo si tu zinatambua vipaji, bali pia zinatoa fursa ya ajira kwa vijana.
“Nipo Iringa kusapoti tuzo hizi, na nawaomba mashirika, makampuni na wafanyabiashara wazisapoti tuzo zetu hizi. Msimu huu wa tatu unapaswa kuwa na nguvu zaidi,” alisema JB.
Tukio hilo limeendelea kuvutia hamasa kubwa kutoka kwa wadau, huku magwiji mbalimbali wa filamu wakiahidi kuziunga mkono ili kuongeza chachu ya ushindani na kuibua vipaji vipya.
Hivi karibuni, tamasha hilo limepokelewa kwa mikono miwili na kupewa baraka zote na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Komredi Kheri James, hatua iliyoongeza uthibitisho wa heshima na ukubwa wa tukio hilo

