Na Mwandishi wetu
Tamasha la Regal Film Festival and Awards (REFFA) limefungua rasmi wito kwa watengenezaji wa filamu kutoka barani Afrika kuwasilisha kazi zao kwa ajili ya kushiriki katika tamasha hilo la kimataifa.
Tamasha hilo hufanyika jijini Accra, Ghana, likiwa na lengo la kusherehekea ubunifu, utofauti na ubora wa filamu za Afrika, huku likitoa jukwaa muhimu la kuonesha kazi za watayarishaji wa filamu pamoja na kuwaunganisha na wadau mbalimbali wa tasnia kupitia maonesho ya filamu na mijadala ya kitaaluma.
Waandaaji wa REFFA wameeleza kuwa aina mbalimbali za filamu zinakaribishwa kushiriki katika tamasha hilo, zikiwemo filamu ndefu (feature films), filamu fupi (short films), makala (documentaries), filamu za uhuishaji (animation) pamoja na filamu za majaribio (experimental films).
Mbali na maonesho ya filamu, watayarishaji pia watapata nafasi ya kushindania tuzo mbalimbali zinazotambua ubora katika vipengele tofauti vya utengenezaji wa filamu kama uongozaji, uigizaji, uandishi wa hadithi pamoja na ubunifu wa kiufundi.
Kwa watayarishaji wa filamu kutoka Tanzania, hii ni fursa muhimu ya kupeleka hadithi za Kitanzania kwenye jukwaa la kimataifa na kuionesha dunia kiwango tulichonacho cha ubunifu na upekee wa tasnia ya filamu nchini.
Mwisho wa kuwasilisha filamu kwa ajili ya REFFA Film Awards ni Agosti 3, 2026.
Kwa maelezo zaidi kuhusu ushiriki na namna ya kuwasilisha filamu, tembelea tovuti ya tamasha hilo kupitia www.reffaawards.com