Mfahamu Ziggy Wakimataifa, muigizaji maarufu wa Tanzania ambaye jina lake limejijenga kupitia filamu, tamthilia na matangazo ya kibiashara yaliyowahi kutamba kwenye tasnia ya burudani nchini.
Safari yake ya kuigiza ilianza tangu akiwa shule ya msingi enzi hizo wanaomfahamu ni kwa jina la Sogurd Gurdson na baadae kuja kuwa mmoja wa waigizaji wenye ushawishi mkubwa zaidi Afrika Mashariki. Ziggy ni mfano hai wa safari ya uvumilivu, nidhamu na kujitunza.
“Nilianzia kuigiza tangu shule ya msingi,” anasema Ziggy. “Baada ya kumaliza sekondari, nikiwa Shinyanga, nikaanza mazoezi kwenye kikundi cha kuigiza mkoani humo.”
Mwaka 2012, ndipo alipoanza rasmi kujiunga na filamu kupitia kampuni ya Tip Top Connection, akishiriki filamu ya Ndoa pamoja na watu maarufu akiwemo Tundamani na Husna Sajenti.
Safari yake iliendelea katika maeneo mengine, hadi kufikia kupata cast kwenye tamthilia ya Siri za Familia.
“Niliwahi kufanya kazi na Chrisant Mhenga kwenye tamthilia ya Dhamira iliyokuwa ikirushwa ITV, na baadaye kidogo nikafanya Siri za Familia. Lakini dili kubwa la kwanza la matangazo lilikuwa la Airtel, na hapo ndipo kila kitu kilipoanza kupendeza,” anasisitiza.
Kwa kujiamini, Ziggy anajihesabia kuwa mmoja wa waigizaji wenye mvuto mkubwa Afrika Mashariki.
“Nakumbuka, Audition ya Siri ya Familia, tulikuwa tumepangwa audition (mchujo) zaidi ya watu 600, lakini jina langu ndilo lilikuwa la kwanza kutangazwa. Huwezi amini,” anasema kwa tabasamu.
Mvuto alionao, umempa nafasi ya kuonekana kwenye filamu na tamthilia mbalimbali, ikiwemo Shilingi iliyokuwa ikirushwa Azam TV.
Wengine wanaweza kubeza uwepo wake kwenye tasnia, lakini kwa upande wake, Ziggy ana mtazamo tofauti kabisa.
“Nahisi TV inanipenda,” anasema. “Nilishiriki kwenye TV Show ya Bingwa ya Startimes na TV3, ipo kama Big Brother hivi..”
Ingawa alitolewa ndani ya mwezi mmoja tu, mashabiki wengi na watazamaji wa kipindi hiko, walishinikiza sana waandaaji hadi akarejeshwa.
“Siez sema sipendwi. Nachojua ni kwamba nilirejeshwa, na nikaendelea kushindana mpaka mwisho, na kuwa finalist wa TV Show hiyo,” anaongezea kwa ufahari.
Licha ya mafanikio hayo, safari yake haijakosa changamoto kwani haonekani msanii wa kupata casts mara kwa mara. Lakini kazi anazozipata, anazitendea haki kwa kiwango cha hali ya juu.
“Nadhani baadhi ya waandaaji filamu/tamthilia wanaangalia waigizaji kwa jinsi wanavyoona wao. Hauwezi kumlazimisha mtu akupe nafasi ya kuigiza kama anahisi haufai. Ila ukipata kazi, lazima uifanye vizuri, na kwa ubora wa hali ya juu” anasisitiza.
Swali: Na unawezaje sasa kufanya vizuri?
Jibu: Naheshimu sana kazi. Napenda kufanya mazoezi na kujiandaa. Nachukulia kazi veery seriously. Siwezi kujiita msanii, hapana, bali ninapenda kuitwa muigizaji, hasa ninapoigiza.
Swali: Na unazungumziaje kuhusu wanaotamba mitandaoni?
Jibu: Kuwa na followers wengi sio kwamba unajua. Siku hizi kila mtu anaweza kupambana na kuwa na followers wa kutosha, sio issue sana. Ila kuigiza ni kazi, kushuti ni kazi, na fani zingine pia ni kazi. Hili ni tatizo kwa generation ya sasa tunayoishi. linaweza lisionekane mapema ila lipo.
Swali: Unahisi kisanaa tunaelekea tunapopataka?
Jibu: Sina uhakika.
Ziggy anaunga mkono juhudi za mastaa wengine katika kukuza sanaa, akiwataja Hemedi Suleimani, Yusuph Mlela na Adam Kuambiana kama mifano ya kuigwa kwenye Tasnia.
“Upendo ndio kila kitu, asikuambie mtu,” anasema. “Wakati mwingine unaweza kukubaliana na mtu kufanya kazi kwa gharama zako (standards), ila baadhi ya producers wakaona kama unaringa, hii pia haijakaa sawa.”
Anafafanua kuwa hali hiyo hupelekea waigizaji kuonekana kama wanapandisha bei, jambo linalosababisha wazalishaji kutafuta mbadala wa bei nafuu, kusambaza majungu, kuharibiana kazi, na hatimaye kudumaza sanaa.
“Waigizaji wanapewa pesa ndogo, hawana maisha. Na sidhani ni sahihi kusema sanaa inapanda. Hatuna hata wasanii wanaopata nafasi kwenda kuitwa kuigiza kwenye kazi za Nigeria au South Africa. Tumeona wachache wakienda Kenya, nk. Msanii hatakiwi kuwaza pesa ya kujikimu, wakati kiuhalisia, tunaonana kila siku mitaani tukililiana njaa. Matokeo yake umaarufu unazidi kipato, hii nayo sio sawa” anasisitiza kwa uzito.
Akifafanua safari yake ya kimataifa, Ziggy anasema aliwahi kufanya kazi na Wamarekani wa Hollywood kama muigizaji wa ziada (extras) kwenye filamu iliyoshutiwa Uwanja wa Taifa wa Mwl. Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.
“Sikumbuki jina la filamu, ila nakumbuka ilikuwa miaka michache iliyopita. Sijui kama ilishatoka au la, nadhani nitaulizia,” anasema huku akicheka.
Kwa lugha nyingine, Ziggy anaonekana kama mtu mwenye kuijali jamii kuliko kuwa kioo tu cha umaarufu.
“Mimi ni mtu ninayetoa ideas nyingi kwa watu mbalimbali. Nipo vizuri sana. Ninasadia wengi, na kuzungumza na wengi. Hata ukiwa na jambo lako au unahitaji rafiki wa kuzungumza naye, nipo, we nicheki tu anytime.”
Swali: Ni msanii gani unadhani anastahili kuwa role model wako?
Jibu: Swali zuri mno, na jibu lake ni rahisi sana, namkubali mno Ziggy Wakimataifa. Huyu ndio role model wangu. Nampenda sana. Ndio namba moja wangu. Wengine ni Single Mtambalike kwenye Lerato alinikosha sana kwa uhalisia wake, yupo so natural; na pia Yusuph Mlela.
Ingawa hakupata nafasi nyingi kimataifa, Ziggy Wakimataifa aliwahi kuteuliwa mara moja kwenye 360 Awards, tuzo zinazoshirikisha zaidi ya nchi sita za Afrika Mashariki na Kati.
“Nilishinda mwaka 2025 nafasi ya Muigizaji wa kiume anayehamasisha zaidi (The Most Influential Actor) wa Afrika Mashariki. Yep, nimeiwakilisha nchi yangu vizuri sana,” anasema kwa kujiamini.
Swali: So, tutarajie kubeba Oscar? Au tuzo yoyote ya kimataifa?
Jibu: (anacheka kwa nguvu) Soko la Oscar? Kwa sasa bado bado. Mimi nataka kwenda slow, steady but sure. Kibongobongo, Soko la kimataifa linawezekana, ila kwa sasa hakuna wa kufikia level za Oscar, wala tusidanganyane.
“Kwa mfano, Kenya inaweza kutusaidia kufika mbali zaidi. Ukiwa bora East Africa (Afrika Mashariki), ni rahisi kufanya vizuri kimataifa.”
Swali: Unaamini katika umaarufu wa kuandaa kiki?
Ziggy: Nadhani muhimu kwa mwigizaji ni kujitunza. Skendo hazifanyi sanaa, sanasana ni ujinga tu. Mimi nilishafundishwa nidhamu kazini, hivyo sifikirii kufanya mambo hayo hata kidogo, wala kufuata huo upepo.
Swali: Unazungumziaje wimbi la uwepo wa tuzo nyingi nchini, zinanyanyua ubora wa fani na sanaa?
Ziggy: Tuzo ni motisha kwa wanaofanya sanaa, ni jambo zuri. Lakini ili ziwe bora zaidi, zinapaswa kuwa na pesa. Mfano, waandishi au waigizaji unapowapa fedha kama support, zinanyanyua hadhi na heshima."
"Kuwa na washindi kabla ya kutangaza tuzo sio sawa. Lile bati au kioo halina thamani kama litakuwa tupu. Waandaaji waache kupendelea."
Swali: Kwa hiyo ni sahihi kusema kuwa tuzo zinanyanyua wasanii wachanga?
Ziggy: Naona hii hali kwa madogo (wasanii chipukizi) wanahisi ukishinda tuzo unakuwa bora kuliko wengine. Hii inajenga chuki na uhasama usio na maana, kwani tuzo ni tuzo tu, isiharibu utu uliopo ndani yetu.
Swali: Unaamini digital content creators wa TikTok na Instagram wanasaidia kuunda mwelekeo wa tasnia ya uigizaji nchini?
Ziggy: Man, kutoa viconent (maudhui) vifupi vifupi haviwezi kukuza tasnia, hata kidogo. Huko TikTok, Insta, nk., kuna series ya unprofessionalism (muelekeo usio na Maadili) kwa sababu watu wanatafuta sana views, posts na likes.
“Mimi nimeanza Insta kabla ya 2013, enzi hizo unapandisha video za sekunde 15. Leo mtu alikuwa fan (shabiki) wako, kesho anakuwa content creator (mtengeneza maudhui), na wakati mwingine hana hata maudhui ya maana katika anachotengeneza. Hii ni hatari, kwani inaweza kuangusha tena tasnia kama ilivyotokea zamani baada ya enzi za Kanumba.”
Ziggy anaendelea kusema kuwa sanaa ni zaidi ya kuigiza, kuna ufundi, maadili na maandalizi.
“Ukiwachunguza madogo, wana muonekano unaofanana, mavazi yanakaribiana. Kila mtu hawezi kuwa muigizaji, tusidanganyane.”
Akizungumza kuhusu mchango wa serikali na taasisi za umma, Ziggy Wakimataifa anaamini Bodi ya Filamu ina nafasi kubwa katika kukuza sanaa, na anaiomba iendelee kuleta fursa na kuzisambaza kwa wasanii wote, kitaifa na kimataifa.
“Kwa vyama, vinapaswa kuamka pia. TDFAA ipo miaka yote. Vyama vya waongozaji, wahariri na wengine vinapaswa kuelewana, kusomana na kushirikiana. Taasisi za umma na viongozi wataweza kwa urahisi kutusikiliza na kutusaidia tukionesha bidii.”
Ziggy pia amewaomba radhi mashabiki wake kwa kutokuonekana sana kwenye filamu tangu mwaka 2022.
“Naomba waendelee kunifuatilia kwenye mitandao ya kijamii. Mwaka huu 2026 ninakuja na series yangu mpya inaitwa Kimoja cha Afya. Mkae mkao wa kula!”
Ziggy Wakimataifa pia alipokea na kuheshimishwa kuwa kwenye DUCE GOT TALENT 2019, na kupewa Tuzo ya Heshima; na pia aliwahi kuwa mgeni rasmi wa MUHASO 2022.
Swali: Je, unaamini katika biashara ya kupandisha kazi zako YouTube au Netflix?
Ziggy: Broo, YouTube inalipa. Mimi napenda kuwekeza pesa ilipo. Nimewaelekeza hadi mastaa kutumia mitandao vizuri. Hata kazi zangu zinazokuja, mashabiki wangu wataziona YouTube, na Mungu akijaalia, hadi Netflix zitafika