Na Charles Mkoka
Najua umeshawahi kuwaona Art Gallery TZ, kikundi cha ubunifu ambacho kimekuwa kikitrend mdogomdogo kwa kutengeneza vipande vya filamu/Tamthilia za Hollywood ndani ya locations za kibongo.
Kinachowafanya waonekane na utofauti sio tu ubunifu wao, bali uwezo wao wa kuoainisha mazingira ya hapa nyumbani kwneye hadithi za kimataifa kwa uhalisia wa kuvutia.
Kama unacheki skits au reels, ukikutana na kipande cha scene ya filamu ya Peaky Blinders, au Den of Thieves, alafu wameigiza watu weusi, ujue hao sio wanaijeria wala wasauzi, ni watoto flani hivii wa kinondoni washafanya yao.
Clips zao zinaendelea kusambaa, na kuwapa hamasa ya kufanya zaidi na zaidi, hadi sasa wameshafanya kazi zilizotafsiri upya filamu maarufu kama Friday, Den of Thieves, Zatima, Peaky Blinders, Fast & Furious, John Wick na nyingine nyingi.
Kivutio kikubwa cha clips hizo ni uwezo wao wa kuendana na uhalisia wa juu ndani ya dakika chache tu, pamoja na matumizi makini ya sauti na mazingira, jambo linalowafanya watazamaji wahisi kama wanaangalia sehemu halisi ya filamu kubwa, katika mazingira yetu halisi. nakuambia, hata uwe nani, laizma wakuchukue.
Anaanza kwa kucheka kidogo, “Mwanzo, wazo lilikuwa ni kutengeneza covers za nyimbo za muziki, lakini niliona kuna namna ya kufanya vitu huku unafurahi, na pia kuonesha uwezo mkubwa zaidi tulionao, zaidi tu ya muziki,” anasema Bruno Ceasar.
Msanii huyo alianza partnership na mwenzake, wakiwa wawili tu, lakini hadi sasa crew nzima imekua na kufikia zaidi ya watu 15, na idadi inaendelea kuongezeka kadri mahitaji na ubunifu vinavyopanuka.
“Ni vizuri kufanya kitu unachokipenda, na sisi tunapenda sana filamu. Tunajua ugumu wake, ila inasaidia pia kurejesha zile moments kwa njia ya kipekee,” anaongeza.
Kwa kawaida, uandaaji wa skits na reels kwa watu wengi huchukua muda mfupi, lakini kwa upande wa Art Gallery TZ, kazi zao huwa na upekee unaohitaji maandalizi makubwa zaidi.
“Tunakutana na changamoto nyingi kwenye kushuti, kwa sababu props na locations vina gharama. Kwa sasa bado hatujapata mfadhili au udhamini,” anafafanua.
Swali: Na kama akitokea mtu wa kuja kutia hela?
Jibu: Tunakaribisha. Menejimenti ipo, nia na madhumuni ni kukaa mezani, kuzungumza, na kukubaliana ili kufanya vitu vya faida zaidi, na kila upande unufaike.
Swali: So, kwanini mmeamua kufanya hivi zaidi?
Jibu: Tunataka kufanya hasa filamu, na kuwekeza huko. Tunatumia nafasi hii kujipika zaidi. Zipo kazi zinazokuja ambazo ni originals, na hopefully tunatarajia zikiingia sokoni ziwe na mchango chanya zaidi na kupokelewa vyema.
Swali: Kazi halisi (original), ni filamu fupi au ndefu?
Jibu: Hii inaitwa Streets of Dar es Salaam, na itatoka mwaka huu huu. Mpaka sasa imeshavuka hatua zote za awali za maandalizi, hivyo fans wetu wakae mkao wa kula.
Swali: Unadhani soko zima liko tayari kupokea kazi za filamu za Kiingereza?
Jibu: Tunaona, kwa sasa filamu zote zinaangaliwa. Watu wanaangalia za Kiswahili, na wapo wengine wanaangalia Netflix, Amazon na platforms zingine. So, yah, nahisi fursa bado zipo.
Swali: Vipi kuhusu crew yenu?
Jibu: Tulianza wachache, now tunamshukuru Mungu watu wanajitokeza kukubali tunachokifanya na wanatamani kuwa onboard. So, yah, na tunapokea kila mtu, ilimradi uwe na nia na unaweza kufanya kazi.
"Lugha yetu ya kwanza ya taifa ni Kiswahili, na Kiingereza ni lugha ya pili. Kutumia Kiingereza kwenye sanaa pia sio mbaya, maana sanaa haibagui lugha; sanasana inatengeneza uhalisia wa kueleweka zaidi au kubeba utamaduni wetu."
“Tanzania bado ipo nyuma sana kwenye utengenezaji wa filamu nzuri ukilinganisha na Korea, China, nchi za Ulaya, hata South Africa. Nadhani tukitumia lugha ya Kiingereza inatusaidia kusogea, ingawa sio lazima, kwani kufanya vizuri kisekta kunategemea zaidi mifumo,” anaongeza.
Swali: Je, kwenye kazi zenu mna matumizi ya akili unde na akili mnemba?
Jibu: Hapana. Kazi zote ni halisia. Zina waigizaji halisi, na nyingi zina sauti halisi pia, kwani tunafanya dubbing sisi wenyewe.
Swali: Tunaona mkipongezwa na watu mbalimbali, wengine ni mastaa na wengine ni mashabiki wenu wa kimataifa. Hii mnaichukuliaje?
Jibu: Inatupa faraja, na inatupa hamasa ya kukaza zaidi. Sisi bado tunatamani kukua zaidi na zaidi, na kuchangia maendeleo ya sanaa kwa kitu kipya kizuri na chenye manufaa. wengine wanaweza wasituelewe ila kuna mahali tunaelekea.
"Mwanzoni tulikuwa tunafanya tu for fun (kwa kujifurahisha), lakini hatukujua kuwa tunachokifanya ni kitu kikubwa sana. Pia imetufanya kuona kuwa kumbe tunaweza kufanya zaidi na zaidi. Kuna pongezi tunapokea kutoka serikalini, wadau mbalimbali; na sasa tunajua kuwa tunapaswa kuwa serious (makini) zaidi na zaidi.
Swali: Ukiiangalia tena Mobland, ambayo so far inafanya vizuri kwa kubeba views za kutosha, anengagement, wewe binafsi unaionaje?
Jibu: (anacheka), mimi naona tumeweka nguvu ya kutosha, na tukiangalia tena kwa jicho la mtazamaji, tunaishia kuwaza kuboresha zaidi na zaidi na zaidi.
Swali: Serikali yetu unaionaje kwenye filamu?
Jibu: Sisi bado hatujaamua kuwa serious sana, lakini naiomba sana serikali yetu kuwekeza kwenye filamu, maana ni sekta inayoonesha wazi kuwa na manufaa makubwa kwa taifa letu. Kuna utalii; Kwa mfano tuna wazo zuri sana la kutengeneza filamu ya kutangaza utalii wetu kimataifa, mbuga za wanyama na uasili wetu tulionao. Ipo kimaandishi (muswada); tutafanya tutakapoweza, lakini tukipata support huenda ikawa kubwa zaidi kimataifa.
Swali: Unataka kusema neno gani kuhusiana na mashabiki wenu wa mitandaoni?
Jibu: Tunaweza kuwaambia mashabiki wetu wazidi kutuamini. Tunawapenda sana, tupo karibu nao, hatuwezi kuwaangusha. Tunawasapoti na tunaitegemea sana support yao. Tutaendelea kuwa nao, na labda kwa kuongezea tu, wasituchonganishe sana (kisha anacheka).
Swali: Kuhusu tuzo za filamu na zingine zinazokuja?
Jibu: Tupo kwenye moja ya kinyang’anyiro cha Tanzania Creators Awards kwenye nafasi ya utengenezaji bora wa Filamu fupi (Best Short Film Making). Tunashukuru kuchaguliwa, na wadau wote nchini tunaomba watupigie kura.
Akimalizia, amesema kuwa kwa wanaotaka kujiunga kwenye crew wanakaribishwa ofisini kwao Kinondoni, na wanapenda watu wanaojijua kuwa wako vizuri kwenye maeneo mbalimbali, waje, na sio kuigiza pekee.
“Kila kazi yetu tunafanya casting, maandalizi mengine, rehearsal, n.k., na bado tunahitaji wataalamu pia kwa ajili ya kuongeza uhalisia. Tunatarajia kufanya usaili hivi karibuni, hivyo wadau wetu wooote wawe tayari. Tunawakaribisha wote.”
Kuhusu kufanya kazi nje ya nchi, wamepokea mialiko kutoka nchi mbalimbali barani Afrika, wengi wakidhani wanatoka Nigeria. Mialiko hiyo ilisimama kutokana na vurugu za Oktoba 29 zilizotokea mwaka jana katika kipindi cha uchaguzi.
“At first watu wengi walidhani sisi tunatoka Nigeria, na wengine walidhani ni Wasauzi. Kwa sasa, nadhani tunaweza kuendelea na projects zilizosimama kipindi cha uchaguzi,” anaongeza.
Swali: So, tutarajie kazi mbalimbali kuruka Netflix?
Jibu: Tunatarajia kuanzisha streaming service yetu hapa nchini, na haizuii kazi zetu zingine kuonekana Showmax au Netflix. So, yes, tunaendelea kumuomba Mungu