Nduttu a.k.a Bishoo la Sinza: elimu, Maisha na Sanaa ya Kuigiza.


Na Charles Mkoka

Ukimuona kwa mara ya kwanza, unaweza kudhani ni mwalimu wa hesabu anayesubiri wanafunzi waje kuchelewa ili awaandikie adhabu. Mtulivu, mpole, mwenye macho ya “nimepanga maisha yangu vizuri.” 

Lakini mara tu anapofungua mdomo na kuanza kuigiza, unajikuta unacheka bila ridhaa yako mwenyewe. Huyu si mwingine bali ni Emmanuel Nduttu, maarufu kama Bishoo la Sinza, au kama Instagram inavyomjua, @Nduttum1

Kama hujamwona bado, basi kuna sehemu ya mtandao ambayo hujafungua vizuri. 

Huyu jamaa ndiye yule anayerejesha ladha ya zile demo za filamu za kibongo za miaka ya 2010, zile sauti zilizokuwa zinaonekana zinashindiliwa na kugandamiziwa kama mtu anaesoma script kwa kutumia kipaza sauti cha shilingi elfu tano, lakini bado zilikuwa zinafika rohoni. 

Nduttu amezichukua, amezipiga pasi, amezivalisha suti mpya ya kisasa, kisha akazitupa mitandaoni zikiwa zimekolea ucheshi wa hali ya juu.

Kinachovutia zaidi ni kwamba, huyu si mtu wa mzaha mzaha tu. Ni msomi. Nduttu ana Shahada ya Filamu na Michezo ya Kuigiza kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Yaani si tu anakufanya ucheke, bali anakufanya ucheke kitaalamu.

“Nilianza kuigiza tangu shule ya msingi, darasa la sita, hadi namaliza darasa la saba nilikuwa tayari najulikana kwa vichekesho na michezo ya jukwaani,” anasema Nduttu kwa sauti ya mtu ambaye ana uhakika na historia yake.


Akiwa St. James Secondary Kigoma, kwenye talent show, ndipo moto ulipoanza kuwaka na kuamua kukazana. Akaendelea mpaka kidato cha sita, na kuchagua kusomea sanaa, pale  UDSM, taaluma ya Filamu na Runinga, na hapo kipaji chake kikaanza kupata misuli halisi.

Lakini swali moja muhimu linabaki: Kwanini Bishoo la Sinza?

“Kwa sababu nataka kuwa tofauti,” anasema bila kusita. Na ukiangalia, jina lenyewe linafanana kabisa na kazi zake, halieleweki mara moja, lakini ukilielewa tuu, unacheka.

Akiwa chuo, tayari alianza kufanya filamu kama Dilemma na kazi nyingine, ambazo anaziona kama maabara ya maisha. “Zilikuwa kama vipimo vya kuelewa tasnia vizuri zaidi,” anasema. 

Leo hii, ameamua zaidi kufanya skits na reels mitandaoni. Sababu? Rahisi, lakini ya busara. “Ni njia nzuri ya kufanya mazoezi, kuwa active, na inaongeza sana engagement,” anasema. Kwa lugha nyingine: ni sawa na kusema, ni gym ya uigizaji, na Instagram/Tiktok ndiyo treadmill.

Na mwamko wa watu je? “Mpaka sasa watu wanapokea vizuri sana, na sijaanza kupata comments mbaya,” anasema kama mtu anayejua anaendelea kushinda, lakini hataki kuharibu bahati kwa kujisifia sana. “So, yah, mambo yanaenda.”

Kwa kasi ya maudhui ya mitandaoni nchini, Nduttu anaamini kabisa kwamba tasnia inaweza kukua hadi kwenye hadhi ya kimataifa. 

“Inawezekana sana,” anasema. “Kama mtu unaendelea kufanya, hata kidogokidogo, ukuaji unakuwepo. Angalia ubunifu wa akina King Pusi, unagusa moja kwa moja soko la kimataifa. Kama wachekeshaji tutaongeza bidii, na staili zetu zitazidi kuwa bora, naamini tutafika mbali.”


Lakini pia anaelewa mipaka ya mitandao. Haamini kwamba video ya dakika mbili inaweza kushindana moja kwa moja na kipindi cha televisheni cha dakika 30 au filamu nzima.

 “Huwezi kufananisha kazi ya dakika moja na kazi ya dakika hamsini,” anasema. “Ni vitu viwili tofauti, kila kimoja kina nafasi yake.”

Kwa upande wa wasanii anaowakubali, Nduttu anamkubali sana Joti, akiamini anafanya sanaa ya uchekeshaji iheshimike zaidi, na bidii yake inaendelea kukuza genre hiyo. 

Kuhusu urasimishaji, Nduttu tayari amejisajili kwenye mamlaka husika, na anawaasa wengine wafanye hivyo. 

“Hakuna kitu kizuri kama kutambulika rasmi,” anasema. “Kuna fursa, kuna changamoto za kazi, na mambo ya kibinadamu. Kujisajili kunakuweka salama na kusaidika kwa urahisi.”

Na mashabiki? Hao wanaongezeka kila siku. Wengi wakifurahia jinsi anavyotania mastaa kwa ucheshi, bila matusi, bila dharau, bila kuumiza. 

“Mpaka sasa sijapata lalamiko lolote wala kukosolewa vibaya na wahusika,” anasema. “Naamini ni kwa sababu ninachotengeneza ni cha kufurahisha kwa nia njema. Namshukuru Mungu kwa kunipa kipaji na kukubalika na jamii.”

Nduttu tayari ameshapata nominations kwenye tuzo za watengeneza Maudhui nchini, za  Tanzania Creators Awards katika vipengele vya ucheshi na miswada (script)

Lakini hata kabla ya hapo, alikuwa tayari anakusanya tuzo akiwa bado masomoni. “Nilipata tuzo mwaka 2021, 2022, 2023 na 2024 nikiwa chuo, na zingine Dodoma — zote zikiwa kwenye ucheshi,” anasema. 

Kwa kifupi, Bishoo la Sinza siyo tu mchekeshaji wa mitandao. Ni msanii mwenye misingi, elimu, maono, na kipaji kinachojua kuchekesha bila kelele, kuelimisha bila kuchosha, na kufundisha bila kuhubiri. 



Chapisha Maoni

Please Select Embedded Mode To Show The Comment System.*

Mpya zaidi Nzee zaidi