John Elisha “Boneka” ashinda tuzo ya muigizaji bora wa kiume Afrika Mashariki

Na Mwandishi wetu

Msanii na muigizaji wa filamu nchini John Elisha, anayefahamika zaidi kwa jina la Boneka, (officialboneka) amepokea pongezi lukuki baada ya kuibuka kinara wa kuigiza Afrika Mashariki kwa mwaka 2025.

Boneka alishinda Tuzo ya Muigizaji Bora wa Kiume kupitia tamthilia ya Kombolela, inayorushwa na chaneli ya Sinema Zetu ya Azam TV

Tuzo hiyo imetolewa na East African Youth Panel, ikimtambua kama mmoja wa wasanii wanaoendelea kung’ara katika tasnia ya filamu ukanda wa Afrika Mashariki.

Mbali na tuzo hiyo, Boneka pia alishinda Tuzo ya Muigizaji Bora wa Kiume 2024 katika Zanzibar International Film Festival (ZIFF) kupitia filamu ya Sozi iliyoandaliwa na Juma Sada (@iamjumasada).

Pongezi nyingi zimemiminika kutoka kwa wadau wa sanaa, akiwemo Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Nchini, Dkt. Gervas Kasiga (PhD), ambaye alimpongeza rasmi alipomtembelea ofisini kwake jijini Dar es Salaam.

Dkt. Kasiga alisisitiza kuwa ushindi wa Boneka ni ishara ya maendeleo chanya katika sekta ya filamu na mfano mzuri kwa wasanii wengine nchini.

Kwa sasa, Boneka anaendelea kushiriki katika tamthilia mpya ya “Upepo”, inayotarajiwa kuanza kurushwa hivi karibuni kupitia chaneli ya Maisha Magic ya DStv.

Akizungumza na vyombo vya habari, Boneka alieleza furaha na shukrani zake kwa mashabiki na wadau wote wanaomuunga mkono:

“Kwangu sanaa ni vazi la heshima, haliwezi kumpendeza kila mtu. Tuzo ni tunu, na kwa miaka hii miwili mfululizo imekuwa ya baraka sana kwangu,” alisema Boneka.

Ushindi huu unaendelea kumuweka Boneka katika ramani ya kimataifa kama mmoja wa waigizaji bora wa kiume wa kizazi kipya kutoka nchini Tanzania.

Chapisha Maoni

Please Select Embedded Mode To Show The Comment System.*

Mpya zaidi Nzee zaidi