Na Mwandishi wetu
Rais wa Shirikisho la Filamu nchini (TAFF), Rajabu Amiri, amewaasa vijana kote nchini kutumia mitandao ya kijamii kwa manufaa ya kimaendeleo badala ya kuigeuza kuwa chanzo cha matatizo.
Akizungumza na Sauti za Filamu, Rajabu alisema mitandao ya kijamii inabeba taswira, hulka na tabia za mtu kwa urahisi zaidi kuliko inavyodhaniwa, jambo linaloweza kuathiri hata nafasi za ajira, biashara au mahusiano.
"Msingi wa mtandao umekuja kama fursa ili wa mbali na wa karibu wawasiliane kwa urahisi, ila ukitumika vibaya unaweza kuwa laana inayotuwinda vijana kila kukicha,” alisema kwa ufafanuzi.
Amiri aliongeza kuwa ongezeko la matumizi ya mitandao ya kijamii kwa vijana nchini limekuwa kubwa, hali ambayo inahitaji elimu ya matumizi sahihi ili iwe chachu ya maendeleo.
“Kwa kijana anayeomba kazi, unaweza ukakosa nafasi kizembe kwani waajiri siku hizi wanakuchungulia hadi mitandaoni kwa urahisi ili kujua kuwa unaposti nini,” alisisitiza.
Aidha, alisema kuwa mitandao inaweza kuwa njia bora ya kujiajiri kupitia sanaa na ubunifu, endapo vijana wataitumia kama fursa, na kwa busara.
“Siku hizi CV sio maneno tu, bali muonekano wako na uhalisia wako kwenye mitandao ya kijamii unaweza kukuelezea wewe ni mtu wa aina gani,” alisema.
Akizungumza kwa mifano halisi, Rajabu alieleza jinsi matumizi mabaya ya mitandao yalivyowahi kugharimu wenzake katika safari za kimataifa.
“Miaka minane iliyopita tulienda Hong Kong, tukiwa vijana tisa, lakini wawili tu ndio tulioruhusiwa kuingia nchini Hong Kong. Wengine walinyimwa kuingia palepale Airport na baada ya kukaguliwa mitandaoni, walirudishwa hapohapo. Hii yote ni baada ya kuonekana na tabia zisizofaa,” alieleza.
Alimalizia kwa kuwataka vijana kutumia mitandao kama daraja la mafanikio, si chombo cha matusi au picha zisizofaa.
“Vijana wenzangu, hakikisheni mnatoboa kupitia mitandao, msiiache iwe laana. Tuwe mabalozi wa heshima na mabadiliko chanya,” alihitimisha.
