"Tuwe mabalozi wa amani” – rais wa TAFF awaambia wasanii

 

Na Mwandishi wetu

Rais wa Shirikisho la Filamu Tanzania (TAFF), Ndg. Rajabu Amiry, amewataka wasanii wa filamu nchini kushiriki kwenye masuala ya kisiasa kwa njia ya kistaarabu na yenye kulinda amani ya taifa.

Akizungumza katika mahojiano maalum na Global TV, Ndg. Rajabu Amiry alisema ni muhimu kwa wasanii kuwa mfano wa kuigwa katika kulinda utulivu, hasa kuelekea kipindi cha uchaguzi.

“Nchi hii inatutegemea sisi. Amani na utulivu unatutegemea sisi. Tuwe mabalozi wazuri na kuhakikisha kuwa usalama wa nchi hii upo mikononi mwetu,” alisema.

Amiry aliongeza kuwa wasanii pamoja na wananchi kwa ujumla wanapaswa kuendelea kufanya kazi kwa bidii kwa ajili ya maendeleo binafsi, ya sekta na ya taifa kwa ujumla.

“Kila mmoja ana wajibu wa kufanya kazi, tena kwa haki, huku akilinda na kutunza amani yetu sote,” alisisitiza.

Aidha, aliwahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi katika mikutano ya hadhara na kushiriki kikamilifu katika zoezi la upigaji kura tarehe 29, ili kuchagua viongozi wanaowataka.

“Nawaomba Watanzania wote tupige kura kwa amani na kumchagua kiongozi wa kweli, bila lawama, ili tuone matokeo ya maendeleo kupitia viongozi tunaowachagua,” alisema Amiry.

Chapisha Maoni

Please Select Embedded Mode To Show The Comment System.*

Mpya zaidi Nzee zaidi