Serikali Yatenga Bilioni 2 kwa Watengeneza Maudhui: “Hii Sasa Ni Kazi, Sio Hobi”


Na Charles Mkoka

Kuna siku simu ilikuwa tu chombo cha kupiga picha za misosi, selfies na locations za mchongo. 

Leo hii, simu ni ofisi, studio, benki, na wakati mwingine hata chanzo cha madili. Na sasa, serikali imethibitisha rasmi: vile unavyotengeneza mtandaoni vinaweza kuwa ajira halali.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Paul Makonda, ametangaza kuwa Wizara imepatiwa Tshs. Bilioni 2 kwa ajili ya kuwawezesha watengeneza maudhui ya kidijitali kuimarisha kazi zao na kuongeza kipato kupitia majukwaa mbalimbali ya mtandao.

Ametoa kauli hiyo Januari 29, 2026 jijini Dodoma, akibainisha kuwa fedha hizo zimetolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa lengo la kuyawezesha makundi yote ya watengeneza maudhui kwenye sekta mbalimbali kuanzia Utalii, Michezo, Habari, Jamii, Muziki, Filamu hadi sanaa nyinginezo. 

Yaani kama unarekodi, unaandika, unaigiza, unahamasisha, au unaelimisha kupitia mtandao jua kuwa huu ni mchongo wako.

Makonda amesema zoezi la uandikishaji wa walengwa linaanza rasmi Januari 30 hadi Februari 15, 2026. 

Watengeneza maudhui wanatakiwa kufika katika ofisi za Halmashauri za Wilaya, Manispaa za Miji na Majiji kupitia vitengo vya habari, kuchukua na kujaza fomu za maombi, zikiainisha taarifa binafsi pamoja na shughuli wanazozifanya.

 Hakuna DM, hakuna link ya bio, hapo ni fomu halali, muhuri halali, na matumaini halali.

Kwa vijana wengi, hii siyo tu fedha, ni uthibitisho. Uthibitisho kwamba kazi zao si “kupoteza muda mtandaoni,” bali ni sehemu ya uchumi wa taifa. 

Ni hatua kutoka kwenye “unasumbua sana na hiyo simu” kwenda kwenye “unaenda lini  kuchukua fomu?” si mnazijua zile kelele za kutoka kwa bi mkubwa au mshua.

Na kwa tasnia ya sanaa na maudhui, huu ni ujumbe mzito: serikali imeamua kuwekeza kwenye ubunifu wa vijana, sio tu kwenye barabara na majengo, bali pia kwenye akili, kamera, kalamu, na mawazo yanayoibadilisha dunia kupitia skrini ndogo.

Kwa kifupi, kama ulikuwa unaota siku ambayo skits, reels, vlogs, podcasts na filamu za mtandaoni zitachukuliwa kwa uzito wa kitaifa, basi leo hiyo siku ndio imefika. 

Na kwa mara ya kwanza, “kupost” kunaweza kweli kukufanya ulipe kodi.

Chapisha Maoni

Please Select Embedded Mode To Show The Comment System.*

Mpya zaidi Nzee zaidi