Nyumbani Films yazindua Academy: filamu, elimu na uzalendo

Na Charles Mkoka

Kuna watu wanatengeneza filamu, kuna watu wanafundisha filamu, halafu kuna watu wanaamua kufanya yote mawili; kwa wakati mmoja, kwa ujasiri, na kwa imani kuwa sanaa inaweza kubadilisha jamii. 

Hapo ndipo Nyumbani Films inapojitokeza, si kama kikundi cha kawaida cha kutengeneza filamu, bali kama kituo (hub) cha vipaji.

Nyumbani Films, imeanzishwa kwa ajili ya kutengeneza filamu za Kitanzania, na kuamua kuwa na academy maalum ili kuwafundisha vijana na kuwajengea uwezo wa kitaalamu katika filamu na kutengeneza maudhui.

Mwanzilishi wa kituo hicho, Wilson Gastory Mwamakatwe, anasema kuwa wazo hilo lilitokana na kuanzishwa kwa We Technology, ofisi au kituo cha mafunzo kinachofundisha kushuti na kuedit — na hapo ndipo filamu zinapogeuka na kuwa “maudhui ya kutazamwa” kutoka kwenye “maabara ya kujifunzia.”

“Tulianzisha hili ili kukuza vipaji kwa wale wachanga kabisa katika filamu, wapate fursa ya kujifunza na kuweza kufanya filamu,” anasema Wilson kwa msisitizo.

Kwa Nyumbani Films, filamu si mwisho wa safari, bali ni mwanzo wa mafunzo. 

Kampuni inalenga kuzalisha wapiga picha, wapiga video, wahariri, waandishi wa miswada, wasimamizi wa uzalishaji, wataalamu wa mavazi, make-up artists, na wataalamu wengine wote wanaohitajika ili filamu iweze kusimama kwa miguu yake miwili bila kubahatisha.

“Tunaamini filamu ni sehemu ya mazoezi kwa wanafunzi wa We Technology, kwa sababu filamu zina kila kitu. Zinaturahisishia kufundisha kwa nadharia na vitendo kwa wakati mmoja, kurekodi scenes, kuendesha plots, na kusimamia uzalishaji. Hii inaongeza uzoefu wa haraka kuliko kusubiri mpaka mtu afike eneo la kazi ndipo aanze kujifunza,” anaongeza.

Hata hivyo, kila safari haikosi changamoto. Wilson anakiri kuwa baadhi ya wanafunzi hawadumu, hasa upande wa waigizaji, ambao mara nyingi huwa hawakai sehemu moja. Lakini kwa upande wa Nyumbani Films, hili halijawazuia kuendelea.

“Tumekusudia kuwa jukwaa huru la kuwakaribisha waigizaji kutoka sehemu yoyote nchini kama sehemu yao ya kujiimarisha kitaalamu,” anasema. “Ndani ya kila kazi tunazofanya, tunafuata professionalism; kusoma scripts, kufanya rehearsal kabla ya kushuti, na kufanya auditions.”

Na kama kuna mtu anadhani filamu ni watu wachache tu mbele ya kamera, Wilson anawakatisha tamaa kabisa.

“Filamu si waigizaji tu. Kuna production managers, mavazi, make-up, casting, location scouts, editors na wengine. Kiufupi ni timu kubwa sana. Na lengo letu ni kuwakuza wote.”

Malengo ya Nyumbani Films si madogo. Wanataka kutengeneza filamu zinazogusa dini, siasa, na kukuza utamaduni wa Kiafrika, huku wakizalisha waigizaji bora, hata kama watacheza nafasi za ziada (extras). Kwao wanaamini kuwa, kila mtu ana nafasi, na kila nafasi ina thamani.

Kwa sasa, kampuni inaendelea na tamthilia ya Win or Die, na pia wakimaliza hio, kuna chuma kingine kinakuja kinaitwa Ndani ya Bongo, itakayogusa siasa, umuhimu wake, na changamoto zake ndani ya familia na jamii kwa ujumla. 

Wilson anaamini kuwa kuna matukio mengi yanayotokea katika jamii ambayo hayajasimuliwa kwa kina, na filamu zinaweza kuwa darasa bora zaidi kuliko hata hotuba au mahubiri.

Anapoulizwa jinsi anavyoweza kufanya kazi na vijana chipukizi kwa wingi, anacheka kidogo, kisha anasema, “Hii kwetu si changamoto. Tunatambua kuwa anayetaka kuigiza ana sababu za msingi. Sanaa ni kazi, si hobby. Tunapojitolea kumfundisha mtu, inakuwa jukumu letu. Na tunajua kuwa mafanikio yanatokana na commitment.”

Mafunzo, kwa mujibu wa Wilson, hayafanyiki kwa mtindo wa darasa la kawaida. Hakuna ‘kaa chini, andika notsi, halafu kesho mtihani.’

“Kwa mfano Win or Die, tunawaita wale waliopitishwa kwenye casting. Mtu anaweza kufanya mazoezi peke yake, au mapema kabla ya kushuti. Muongozo tunaotoa unamlazimisha mtu ajifunze kwa vitendo,” anasema. Kwa lugha nyingine ya kizaramo anasema: kama hutaki kujifunza, kamera itakuumbua haraka sana.

Kwa mtazamo wa Wilson, academy hii ni jukwaa la msanii chipukizi kuonekana, lakini pia ni kiwanda cha kumkomaza msanii huyo hadi awe tayari kushindana kitaifa na hata kimataifa.

Sauti za Filamu ilifanikiwa kumuuliza, Je, anaamini wanaweza kuzalisha mastaa wa kushindana duniani? Jibu lake ni la kawaida na  lakini lenye uzito: “Labda sio leo, labda sio kesho, lakini tutafika.”

Kwa sasa, anasema wazi kuwa Tanzania haina mwigizaji anayewakilisha filamu zake kimataifa kwa kiwango kikubwa. 

“Kama angekuwepo, kila mtu angekuwa anamjua,” anasema. “Kipindi kile Kanumba alitaka kupanda, lakini bado. Msanii wa leo hapendi kusoma scripts, sasa utawezaje kushindana kimataifa?”

Swali: Kuhusu wimbi la skits na reels fupifupi?

“Mimi sioni zikikuza tasnia. Zinaleta majina ya muda mfupi, lakini hazigusi masuala ya msingi. Mara nyingi utaona mapenzi, uchawi, kufumaniwa, lakini siasa, historia, au changamoto za jamii haziguswi.”

Anaendelea kwa kusema, “Nchi yetu ikiwa na changamoto kama za ubakaji, hatuwezi kukimbia kulibeba (tatizo husika) kisanaa kwa mapana na kuielimisha jamii (juu ya tatizo hilo). Tunapaswa kujijengea mifumo ya kufanya filamu zibebe uzalendo wetu na kujiimarisha kimataifa.”

Anatoa mifano ya Nigeria na Marekani, akieleza jinsi filamu zao zinavyojenga taswira ya taifa lao duniani; iwe ni nguvu ya imani, au nguvu ya kijeshi; hata kama uhalisia una changamoto zake. “Na sisi pia tunapaswa kuwa imara hivyo,” anasisitiza.

Kwa sasa, Nyumbani Films haijaanza matumizi ya akili unde (AI) au akili mnemba katika kazi zao, lakini wanapanga kuanzisha darasa maalum kuanzia mwezi wa tatu, ili kufundisha na kuimarisha fursa mpya kwa filamu na video production kwa ujumla, kwa kila watakaoenda kujifunza.

Kuhusu content creators wa sasa, Wilson anaamini kuwa wana tatizo kubwa la kukosa elimu na hamu ya kujifunza.

“Tuna kizazi kisichopenda kusoma, wala kujua historia ya nchi yetu. Unaweza kuigiza mapenzi, lakini ukose uelewa wa mazingira. Ndiyo maana filamu nyingi za hapa hazishibi. Ukimpa mtu mwenye uelewa wa kimataifa kuigiza hapa, bado atakupa matokeo mazuri zaidi na lazima utaona utofauti.”

Suluhu kwake, ni moja tu: umoja na kushirikiana. “Si lazima kila mtu awe na YouTube channel. Tunaweza kuunda timu na kufanya kwa pamoja, ili mafanikio yawe makubwa zaidi.”

Kuhusu kujiunga, kwa upande wa We Technology, mafunzo ni ya kila mwezi na ada ni Tshs. 165,000/= yakihusisha kushuti, graphics design na mengine. Lakini kwa upande wa Nyumbani Films, kila kitu ni bure.

“Tunapokea watu bure, bila malipo. Mafunzo yote ni free. Tunakuingiza kwenye group, tunakupa script, unafanya mazoezi, siku ya kushuti unakuja mapema, mnafanya rehearsal, halafu mnaingia set. Kadri unavyoimarika, ndivyo unavyoendelea.”

Ndiyo, hataki hela, ni bure kabisa.

Nyumbani Films pia inaamini katika kuuza kazi mitandaoni, huku ikitaja platforms kubwa na kongwe duniani za YouTube na Netflix.

 “Kwa sasa tunajiimarisha YouTube, na baadaye tutafikia Netflix kwa urahisi,” anasema Wilson kwa kujiamini.

Kwa sasa, anaiomba Bodi ya Filamu kuendelea kusapoti wasanii, hasa wale wanaotengeneza maudhui yenye utaalamu na uzalendo, hata kwa msaada wa kifedha inapobidi.

 “Kwa sasa tuna mashabiki wachache kwa sababu hatukuwa na consistency ya kutosha, lakini kuanzia mwezi wa tatu tuna plan nzuri. Tunaamini katika kazi nzuri, na tutakua kwa kasi zaidi.”

Kuhusu kufanya kazi na mastaa, Wilson anawaza kivyake: “Sisi hatuamini katika mastaa wa Bongo. Tunaamini katika young talents. Bongo hatuna mastaa wa filamu, tuna waigizaji wa kawaida tunaokutana nao kila siku, si icons.”

Anafafanua: “Mtu anaweza kuwa maarufu sana kwa muda mfupi kwa kuwa na kipindi kinachooneshwa TV, lakini hiyo siyo alama ya ubora wa uigizaji wa kudumu. Hatuna msanii ambaye hata Rais anaweza kumuagiza kimataifa kutuwakilisha.”

Swali: Na vipi kuhusu mipango ya kuigiza nje ya nchi? 

Wilson: Ndiyo, ipo. “Tulipanga kwenda Kongo, lakini vita vilituzuia. Bado tuna mipango na nchi kama Rwanda, Malawi na Kenya.”

Wilson anamalizia kwa wito mzito kwa wasanii wote wa Tanzania, iwe muziki au filamu kuwa wawe identical kama taifa katika kubeba na kuendeleza utamaduni wetu.

“Hata msanii wa Tanzania akienda harusi, mara nyingi utamkuta amevaa mavazi ya kinaijeria. Hatuna vazi la kitaifa la kutunadi Tanzania, wakati tuna vingi mno. Wasanii tunapaswa kuthamini na kuendeleza vya kwetu.”



Chapisha Maoni

Please Select Embedded Mode To Show The Comment System.*

Mpya zaidi Nzee zaidi