Jafari Makatu: Mzee wa Maadili, Nidhamu, na mwalimu wa vizazi vya filamu


Na Charles Mkoka

Leo tunakutana na msanii mkongwe Jafari Makatu, mmoja wa watu walioweka msingi wa tasnia ya filamu na maigizo nchini Tanzania, mtu ambaye anaigiza, anaandika miswada, na amekuwa katibu wa muda mrefu wa chama cha waigizaji nchini TDFAA mkoa (wa kikanda, au wilaya) wa Kinondoni. 

Safari yake inaanzia mbali, miaka ya sitini, alipokulia pwani ya Dar es Salaam. Akiwa bado mdogo, alianza kuvutiwa na maigizo ya jukwaani enzi hizo ni michezo ya kuigiza ya maonesho, kipindi ambacho kamera zilikuwa nadra kabisa, na umaarufu ulikuwa ni labda kupigiwa makofi na majirani, au kushangawa na kadamnasi na sio kuwa na “likes” nyingi wala "followers" wa mitandaoni.

“Nililelewa sana na bibi yangu wa upande wa mama. Alikuwa ananisimulia hadithi nyingi, na baadaye nikaona vikundi vingi vya uigizaji pale DDC Kariakoo. Miaka hiyo sanaa ilikuwa kwenye majukwaa machache, yakiambatana na ngoma, sarakasi na michezo mingine,” anasimulia.

Anakumbuka kipindi ambacho vikundi vya sanaa ya kuigiza kutoka Magereza vilikuwa vikisafiri mikoani, na kujipatia umaarufu, huku maigizo ya televisheni yakiwa bado hayajachukua nafasi yake hata kuruka bado kabisaa. “Tulikuwa tunaenda taratibu sana. Hakukuwa na kamera za kurekodi, hivyo hata ndoto za kuonekana zilikuwa ndogo,” anasema, akisema kwa upole.

Lakini pamoja na mazingira hayo magumu, sanaa ya wakati huo ilikuwa na msingi mmoja mkubwa: nidhamu na heshima kwa uongozi. 

“Kipindi hicho ilikuwa ngumu hata kumuona mwenyekiti wa kikundi. Na akija, msanii anaogopa, si kwa sababu amefanya kosa, bali kwa sababu heshima ilikuwa kubwa sana. Na mara nyingi mwenyekiti hakuwa hata msanii,” anasisitiza.

Kuja kwa DTV na CTN kulileta mapinduzi makubwa katika uigizaji wa televisheni, hasa kupitia maigizo ya akina Boka na Sudi. 

"Msanii aliyenipa hamasa ya kupenda sana kuigiza ni Mzee Majuto "King". huyu amenifanya niendelee kuwa imara kwelikweli, maana nikiona kazi zake nakuwa natamani na mimi kuigiza kwa ubora wa hali ya juu. ingawa yeye ni nguli katika uchekeshaji, ila ukiwa muigizaji ni rahisi kujua kuwa amekuwa na kiwango cha hali ya juu mpaka alipotangulia mbele za haki"

Kwa wasiomfahamu, Mzee King Majuto alianzaga kuigiza zamani sana, tena sana, akiwa tuu na miaka tisa, na unguli wake ulikuwa unaonekana sana majukwaani, tangia miaka ya sitini na sabini.

“Nakumbuka tulikuwa kwenye kundi moja na akina Mzee Chilo, Gabo na wengine. Tulikuwa tunafanya mazoezi kila siku, Jumatatu hadi Jumamosi, na mapumziko ni Jumapili tu. Na tulifundishwa kila kitu: mavazi, maadili, nidhamu, hadi namna ya kusimama jukwaani kwa umahiri,” anasema.

Kwa pamoja na watu wengine wanne, alianzisha kundi lililofahamika kwa jina la Bahari Sanaa Group, lililokuwa na makao yake pale Friends Corner. Kundi hilo liliwahi kuitishia hata Kaole ya kipindi hicho, iliyokuwa na akina Ray na Kanumba

“Tulipeleka kazi kadhaa ITV na Channel 10, kabla ya kundi kuvunjika. kazi zilionekana, ila kwenye upande wa maslahi mambo yalikuwa bado magumu. Ndipo baadae, akina Mzee Chilo wakaendaga kujiunga kwa Tuesday Kihangala,” anakumbuka.

Baada ya kupitia makundi mengi na kuona mengi, mwaka 2011, Jafari Makatu alipata zali la kuigiza filamu fupi ya Chumo, kupitia audition ambayo kiukweli ilibadilisha maisha yake ya uigizaji kisanaa.

“Nilipigiwa simu na Hidaya Njaidi kipindi hiko tulikuwa wote kundi moja la sanaa, na aliniambia kuhusu audition ya Chumo. nilipoenda, baada ya mchujo, Nikapita mimi, Jokate Mwengelo, Yusuph Mlela na marehemu Sharo Milionea,” anasema.

Baada ya hapo, akashiriki katika filamu ni EONI (2023), Kisiwa cha wachawi, Binti (2021, ya Seko Shamte), na tamthilia  nyingi zikiwemo Panguso (Ya Jimmy Mafufu), Huba, Dunia nyingine, Bunji, Chanda (2023), Fahari (2025, ya Jennnifer Kyaka), na nyingine nyingi zinazorusha televisheni na mitandaoni. Lakini kwake, msingi wa sanaa bora bado unabaki kuwa kwenye mazoezi ya kutosha, na nidhamu ya kujifunza zaidi.

“Nilivyoigiza kwenye Chumo, nilijiona nakua. Mimi napenda kujifunza, na rehearsal pia zinanijenga sana. Ilikuwa filamu fupi, lakini imeniweka pazuri mimi na wenzangu. Iliongeza kujiamini hasa kwenye kufanya kazi za kimataifa,” anaongeza.

Swali: Na umesema kuwa unaandika sana miswada?

Jafari: Ndio, na naanza kuwashukuru walimu wangu akiwemo Marehemu Chaiba, amenifunza mengi, pia mwingine ni Richard Ndunguru. naweza kusema kuwa wamenijenga pakubwa ile kiu ambayo Mungu ameiweka ndani yangu, na kuwa wasaidizi wema kwangu, nawaombea kheri Mwenyezi Mungu awalipe popote pale walipo. nimeweza kujifunza na bado naendelea kuandika vizuri sana, na pia najifunza kwa wanaojua zaidi yangu.

Swali: Kuna Miswada (Scripts) ambayo umeshaifanya tayari?

Jafari: Ndio, kuna nyingine sijaziuza bado, zipo na pia kuna kazi tumeifanya kwa pamoja na chama cha waigizaji TDFAA wilaya zote; Kinondoni, Temeke, Ubungo, Ilala na Kigamboni. Tumeunganisha nguvu na akili na kutengeneza filamu ndefu inayokuja hivi karibuni. Mimi ndiyo nimetunga story na kuandika script.

Swali: Inaitwaje?

Jafari: Inaitwa Hanifa. Inahusiana na elimu kuhusu ugonjwa wa fistula, ambao matibabu yake ni bure. Filamu imelenga kuielimisha jamii moja kwa moja ili kuondoa hofu.


Swali: hamasa yake hasa ni ipi?

Jafari: Jamii inafahamu vitu, lakini uelewa huwa haujitoshelezi. Wengine wana dhana potofu. Tumefungua ukweli na tunaamini kila Mtanzania ataweza kujua, kukabiliana nao, na hatimaye kusaidia jamii, mijini na vijijini.

Anasema wazo la filamu hiyo liliungwa mkono na viongozi wa TDFAA wilaya zote za Dar es Salaam, na kama kitapokelewa vizuri, huenda kikazaa matunda mengine mengi.

Kwa upande wa uongozi, Makatu amekuwa katibu wa TDFAA Kinondoni kwa awamu kadhaa.

Swali: Nini siri ya mafanikio ya uongozi wako?

Jafari: Ni kujua unaowaongoza. Naamini katika kusikiliza watu, kuwasaidia kimawazo na kutatua changamoto zao. Mengi yanategemea jinsi unavyohudumia kwa busara na hekima.

Anaongeza kuwa falsafa hiyo ameitoa kwa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere. “Ukiona watu wanaanza kukuonyesha wamechoka, ni ishara ya kupumzika, si kung’ang’ania kuendelea kuwaongoza,” anasema.

Makatu ameshafanya kazi kadhaa za kimataifa ambazo zipo hadi kwenye IMDb, lakini hilo halimfanyi ajione mkubwa kuliko wengine. 

“Kwenye sanaa kuna kujifunza, kurekebisha, kujifunza tena na kurekebisha tena. Hata kama unaona upo sahihi, jicho la mwingine linaweza kuona changamoto ulizokosa kuzigundua,” anasisitiza.

Pia anaamini sanaa bora lazima izingatie maadili na nidhamu. 

“Nidhamu inaanzia kuwahi kazini. Msanii ukifika set umechelewa masaa matatu, unamkasirisha muongozaji na unajikosesha nafasi ya kujiandaa vizuri. Kwangu hilo ni tatizo. Ndiyo maana napenda sana kuwahi na kujiandaa,” anasema.

Mpaka sasa, Makatu amefanya kazi na vizazi kadhaa, ikiwemo cha miaka ya Tisini: cha enzi za kanumba, na hadi hiki cha sasa cha kidigitali. 

“Lazima tukubali maendeleo. Kuna biashara kwenye YouTube, cable TV, na hata huko TikTok. Ni suala la kujua jukwaa lipi linataka nini na kufanya kazi kulingana na jukwaa hilo,” anasema.

Swali: Hauoni kuwa kuna mahali panaweza kukuacha?

Makatu: Hapana. Ukijua wanachotaka producers, au Dairekta wako, unawapa. Lakini muhimu zaidi ni kuelimisha jamii na kusimama kwenye maadili, hata kama unafanya kisasa.

Swali: Utandawazi umekuwa ukishambulia maadili, hasa mitandaoni. Je, hili linaweza kuathiri filamu pia?

Makatu: Ndiyo, na mamlaka husika kama BASATA na Bodi ya Filamu zinapaswa kuwa macho, mchana na usiku, hata vyama pia vinapaswa kuamka kwenye hili, ili kuhakikisha maadili yanatunzwa na vijana wanaelimishwa mapema.

Anaongeza kuwa maadili yote yanaanzia kwenye familia.

Swali: Unawezaje kumudu kazi na familia vizuri?

Makatu: Familia yangu wanapenda sanaa. Wanajua naigiza, na wanajua kinachoigizwa si maisha yangu halisi bali ni elimu kwa jamii. Hilo ni muhimu sana kutofautisha kazi na maisha binafsi.

Swali: Ni mtoto yupi unayemwona anaweza kubeba kijiti chako cha uigizaji?

Makatu: Yule aliyemaliza kidato cha nne hivi karibuni. Anapenda sana. Wakati mwingine anasoma hadi scripts zangu ninapofanya mazoezi. Kuna siku nilienda naye kazini Muhimbili, walimjaribu kuigiza tangazo fulani, alifanya vizuri sana hadi waandaaji wakachanganyikiwa. So, ndio, Najua yupo vizuri, lakini muda wake bado haujafika, naye anajua hilo.


Makatu anamshukuru Mungu kwa maisha yake na anamkumbuka sana Mzee Makatu wa awali, aliyewalea wengi kwa nidhamu ya hali ya juu.

“Tulilelewa na Mzee Makatu mwenyewe, alikuwa makini sana kwenye nidhamu na maadili. Ilifika kipindi alikuwa anapewa hadi watoto wengine waishi naye ili awaweke sawa. Ndiyo maana tulikua kama ndugu wengi kwenye nyumba moja, na wote tukila na kuishi na kucheza, kwa upendo kwa wakati mmoja,” anasema.

Kwa upande wake, msanii Jafari Makatu anaamini heshima hufanya kazi pande zote. 

“Mimi ni msanii, ninaweza kuwa na jina, lakini sipaswi kumdharau mtu yeyote. Hujui mwenzako (unayemdharau) anapitia nini. Unaweza kuwa umekula leo, lakini mwenzako hajala tangu jana. Heshima inasaidia zaidi kuliko sisi tunavyofikiri,” anasisitiza.

Swali: Na neno la kukazia?

Jafari Makatu: Nawashukuru Watanzania wote, na pia namshukuru na kumuombea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Ameonyesha upendo mkubwa kwetu waigizaji kupitia fedha zilizotolewa kwa watengeneza maudhui. Tunaomba upendo huu uendelee. Mashabiki wote wa filamu wanaoendelea kutuangalia, kutusikiliza na kutusoma pia upendo wenu ni muhimu sana kwetu. Na zaidi ya yote, tuwe na hofu ya Mungu, maana yeye ndiye kila kitu. Mungu ni fundi." alimalizia

Chapisha Maoni

Please Select Embedded Mode To Show The Comment System.*

Mpya zaidi Nzee zaidi