Na Mwandishi wetu
Leo Ijumaa, Februari 6, 2025, Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania, Dkt. Gervas Kasiga, amezungumza na waandishi wa habari na kutambua mchango mkubwa wanaoutoa katika kuhakikisha vipaji vya wanatasnia wa filamu na michezo ya kuigiza vinafikia walaji wao ambao ni watazamaji wa ndani na nje ya nchi.
Amesema kazi ya waandishi wa habari imekuwa nguzo muhimu katika kuipa tasnia ya filamu na sanaa ya uigizaji thamani, mwendelezo na nafasi kubwa zaidi katika jamii, huku ikichangia ukuaji wa vipaji na maendeleo ya sekta kwa ujumla.
Aliongeza kuwa, “Siku zote Bodi ya Filamu inatambua mchango unaotolewa na waandishi wa habari katika kuhakikisha thamani na ukuaji wa vipaji na sanaa unawafikia Watanzania wote na hata nje ya nchi. Vipaji ni biashara endelevu, inayoleta kipato kwa wasanii wanaoigiza, na mafanikio haya yanaendelea kuimarika.”
Wakati huo huo, Bodi ya Filamu imetangaza kufanyika kwa Tuzo za Filamu Tanzania (TAFFA) 2025/2026, zitakazofanyika Februari 14, 2026, katika ukumbi wa The Super Dome, Masaki jijini Dar es Salaam.
Wananchi wamehimizwa kununua tiketi mapema kupitia tovuti www.taffafestival.or.tz/tiketi huku tukio hilo pia likitarajiwa kurushwa mubashara kupitia Azam TV, Chaneli ya Sinema Zetu.
