Shaykaa apata ubalozi wa filamu, kuendeleza tasnia kati ya Tanzania na India


Na Mwandishi wetu

Bodi ya Filamu Tanzania imemtambua rasmi mwanatasnia mashuhuri, Bi. Shahista Alidina maarufu kama Shaykaa, kuwa Balozi wa Bodi ya Filamu Tanzania katika sekta ya filamu nchini India.

Katibu Mtendaji wa Bodi hiyo, Dkt. Gervas Kasiga, alimkabidhi Shaykaa cheti maalum cha kuthibitisha ubalozi wake siku ya Ijumaa, Februari 6, 2026.

Shaykaa ni mtayarishaji filamu wa Tanzania anayetambulika kimataifa, akiwa mshindi wa Tuzo ya World Oscars Signature ya Mwigizaji Bora wa Kike mwaka 2021 kupitia uigizaji wake katika filamu Uhuru na Gharama Zake. Tuzo hiyo iliongeza hadhi ya filamu za Tanzania katika majukwaa ya kimataifa.

Kwa miaka kadhaa, Shaykaa amekuwa daraja muhimu kati ya wadau wa filamu wa Tanzania na masoko ya kimataifa, hususan India. 

Kupitia nafasi yake mpya ya ubalozi, anatarajiwa kuimarisha ushirikiano kati ya tasnia za filamu za Tanzania na India, kuitangaza Tanzania kama kituo bora cha kurekodia filamu, pamoja na kufungua fursa za ubia, mafunzo na usambazaji wa filamu za Kitanzania duniani.

Chapisha Maoni

Please Select Embedded Mode To Show The Comment System.*

Mpya zaidi Nzee zaidi