Mfahamu Happy Swebe, maarufu kama Tabu wa Kombolela, ni miongoni mwa wasanii wanaokua kwa kasi nchini Tanzania
Ni msanii chipukizi wa kike anayeendelea kupanda kwa kasi katika tasnia ya filamu na tamthilia.
Safari yake ya sanaa ilianza akiwa mdogo jijini Mbeya, kabla ya kufanya uamuzi mkubwa wa kuhamia Dar es Salaam.
Kwenye mahojiano ya dhati na Sauti za Filamu, Happy anasimulia mwanzo wake wa mafanikio kupitia Tamthilia za Maneno ya Kuambiwa ilioruka miaka michache iliopita na ya Kombolela inayoendelea kutamba hivi sasa.
“Abduli alinipigia simu, sijui aliniona wapi, Akaniambia mimi ni new character wa Kombolela." anamalizia kwa kucheka.
Happy alianza rasmi kuigiza kwa kulipwa mwaka 2017, akipitia makundi mbalimbali ya sanaa ndani ya miaka zaidi ya miwili kabla. Na leo hii anaheshimu kila hatua aliyopitia, akiamini sanaa ni njia ya kumfikisha katika ndoto zake.
“Ninapenda sana kuigiza nafasi ngumungumu, na naamini katika kufanya vitu vigumu vinafungua milango mikubwa.” alisistiza kwa umakini.
Msanii Hapy Swebe, pia ameonekana kwenye filamu fupi ya Nia ilioongozwa na Seko Shamte, pamoja na Malaika iliyorushwa DStv miaka michache iliopita. Kazi zote hizi anaamini kuwa zimemjenga kuwaza kuigiza kwa mapana zaidi.
Akitia neno kuhusu uigizaji nchini, Happy anaamini uigizaji wa Tanzania umeendelea na sasa unaanza kuvuka mipaka.
“Naona wasanii wa Tanzania wakifanya kazi nje ya nchi, na hii ni hatua nzuri sana. Mimi natamani kuigiza kimataifa, nje ya Tanzania pia.”
Tulipomlinganisha kwa heshima kuwa anaweza kufikia hadhi ya Lupita Nyong’o wa Kenya, Happy alichagua mtazamo ufuatao:-
“Naamini katika kufanya vizuri popote. Kenya wana Lupita, ndio, nami natamani Tanzania pia iwe na Lupita-wake. Na hata kama tukizidi (zaidi ya mmoja), bado sio mbaya. Maendeleo ya wengi yanaanza kwa mmoja.” aliongezea Happy Swebe
Swali: Je, tutarajie kubeba tuzo ya Oscar kutoka kwako, miaka michache ijayo?
Happy: “Ndiyo, naamini katika hilo. ila Mungu ana mipango yake, lakini nikiwa hai, namwomba anipe hicho kibali.” alikazania.
Licha ya mabadiliko ya tasnia, Happy bado ana mapenzi makubwa kwa maigizo ya jukwaani.
“Nikipewa nafasi ya kufanya stage play, nipo tayari kabisa. Zamani zilikuwepo, sasa sijui zimepotelea wapi, lakini binafsi napenda sana.”
Akiigiza nafasi ya ububu kwenye msimu wa pili wa Kombolela, Msanii Happy anasema kuwa uzoefu huo ulimgusa hadi kwenye maisha yake ya kawaida, nje ya maigizo.
“Kulikuwa na muda hata kuongea napata shida. Nafasi ile ilinibadilisha kidogo, tena mwanzoni mwanzoni nilijikuta naishi kama Tabu kweli.” aliongea kwa msisitizo.
Happy anashindanishwa kuwania tuzo ya Tanzania Global Awards katika nafasi ya Msanii Chipukizi wa Kike, jambo analosema linampa nguvu mpya katika sanaa.
“inatia moyo, inaonesha kuwa kazi yangu inaonekana katika jamii na kuna watu wanatambua, na inaniongezea ari ya kuendelea kuigiza. Napenda sana sanaa, sana tena sana.”
Mbali na uigizaji, ana ndoto ya kuwekeza katika filamu kama producer, na anapenda kufanya filamu za genre mbalimbali hadi za Action. Na anapenda sana mazoezi hata ya filamu za mapigano.
“Nilipataga cast ya filamu ya kupigana, nikavumilia mazoezi yote, zaidi ya miezi sita, na stunts zake mbalimbali. Naisubiri kwa hamu sana filamu hiyo itoke.” aliongezea.
Mbali na sanaa, Happy pia ni mpenzi wa mitindo.
“Napenda kubuni, kuvaa na kufuatilia sana mitindo,” anasema.“Sijafika mbali sana (anacheka), lakini niliwahi kufanya fashion, na bado napenda ila sio kwa sasa.”
Happy anaamini Tanzania ina uwezo mkubwa wa kufanikiwa kimataifa, endapo uwezeshwaji utaimarishwa.
“Bado tunahitaji support. Sanaa ni kazi kama kazi nyingine, na waigizaji wanastahili kunufaika zaidi. Kenya wananufaika kuliko sisi. Tunaomba serikali iongeze msaada ili msanii aweze kutoa mchango chanya kwa taifa letu.”
Akihitimisha, Msanii huyo anaacha ujumbe wa shukrani kwa mashabiki wake:
“Mimi ni msanii mchanga, bado nakua, na sijafikia hata robo ya ndoto zangu. Naahidi sitawaangusha, na nawaomba mashabiki zangu na watanzania wote waendelee kunisapoti.”


