Na Charles Mkoka
Bodi ya Filamu Tanzania imeungana na wadau wa mazingira katika shughuli za awali za utayarishaji wa makala ya Guardians of the Peak Msimu wa Pili, zilizofanyika Januari 21, 2026 mkoani Kilimanjaro.
Akiongoza shughuli hizo, Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania, Dkt. Gervas Kasiga, alishiriki katika zoezi la upandaji miti pamoja na kutoa elimu ya uhifadhi wa mazingira kwa wakazi wanaoishi pembezoni mwa Mlima Kilimanjaro.
Katika juhudi za kurithisha kizazi kipya utamaduni wa kutunza mazingira, wanafunzi wa Shule ya Msingi Kaloleni pamoja na wanafunzi wa shule za sekondari za Msasani na Bomambuzi walishiriki.
Makala hii imewaleta pamoja wadau mbalimbali wa uhifadhi wa mazingira, wakiwemo Taifa Gas, ambao waligawa mitungi ya gesi ya kupikia kwa wakazi wa maeneo yanayozunguka Mlima Kilimanjaro, ili kuhamasisha matumizi ya nishati safi na kupunguza uharibifu wa uoto wa asili.
Mradi huu unaendana na juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kulinda mazingira na kuhimiza matumizi ya nishati safi nchini.
Kupitia Guardians of the Peak, filamu inaendelea kuonesha mchango wake katika kutangaza utalii, kutoa elimu ya mazingira na kuhamasisha jamii kulinda rasilimali asilia kwa vizazi vijavyo.
Bodi ya Filamu Tanzania imewahimiza wanatasnia wa filamu na michezo ya kuigiza kutumia majukwaa yao kusimulia hadithi zitakazotangaza vivutio vya utalii na kuhamasisha uhifadhi wa mazingira, huku zikiongeza fursa za kipato kwa wasanii na taifa kwa ujumla.