Mwanatasnia wa filamu nchini Rammy Galis (rammygalisofficial) ameweka historia mpya baada ya kupata nafasi ya kuigiza katika filamu nchini Hispania, hatua inayoongeza uwepo wa Tanzania katika majukwaa ya filamu ya kimataifa.
Kupitia taarifa rasmi, Bodi ya Filamu Tanzania imempongeza Rammy Galis kwa mafanikio hayo, ikisema kuwa anaipeleka sanaa ya filamu ya Tanzania nje ya mipaka ya nchi na kuwakilisha taifa katika jukwaa la kimataifa.
“Bodi ya Filamu Tanzania inakutakia heri katika utekelezaji wa majukumu yako ya kitasnia nchini Hispania,” iliandika kupitia ukurasa wake rasmi, huku ikiwahimiza wanatasnia wengine kutumia fursa mbalimbali za kimataifa ili kuvitangaza vipaji vyao na kuongeza uwakilishi wa Tanzania duniani.
Kwa upande wake, Rammy Galis alithibitisha taarifa hiyo kupitia ukurasa wake wa Instagram siku tano zilizopita, (huku pia akijiunga na andiko la bodi ya filamu nchini, baadae), akieleza shukrani zake kwa Shirikisho la Filamu la Hispania kwa kumuamini na kumpa nafasi ya kushiriki katika filamu ya Kihispania itakayofanyika jijini Madrid mwezi Machi 2026.
“Naahidi kufanya kazi kwa kiwango cha juu na kuiwakilisha vyema kazi ya filamu Tanzania duniani,” aliandika. “Itakuwa heshima kubwa kuwakaribisha nchini Tanzania kwa ajili ya uzinduzi wa filamu itakapotoka.”
Katika filamu hiyo, msanii Rammy Galis atacheza nafasi ya Inspector Emilio Marcos, jukumu linalotarajiwa kumpa mwonekano wa kipekee katika soko la filamu la Ulaya na kuendeleza hadhi ya wasanii wa Tanzania kimataifa.