Hali halisi ya usambazaji na utengenezaji filamu kwa Tanzania na barani Afrika kwa ujumla

Maonesho ya sinema ya kumbi za wazi yanayoendesha na Ajabuajabu kwa kushirikiana na Kijiweni Production. Picha na Nafasi Art Space 2025. (imewahi kuonekana medium)
Anaandika Ha Bib

Utengenezaji wa filamu haujawahi kuwa rahisi kama ilivyo sasa, hasa barani Afrika na katika nchi za ukanda wa kusini. 

Ukuaji wa teknolojia ya kidijitali, upatikanaji wa vifaa kwa gharama nafuu, na mitindo ya kibunifu inayoibuka mara kwa mara vimewawezesha watengenezaji filamu wa kiafrika kusimulia hadithi zao kwa uhuru ambao haujawahi kushuhudiwa. 

Hata hivyo, wakati shughuli za uzalishaji filamu zimefunguka zaidi; usambazaji wa filamu bado umebaki kuwa kizungumkuti, kilichosheheni urasimu na upendeleo unaowatenga walio wengi. 

Kwa watengenezaji wengi wa filamu, changamoto halisi haianzi baada ya kuuandika mswada tu au kuitengeneza filamu yenyewe, bali ni kile kinachofuata baada ya filamu hiyo kukamilika kutengenezwa.

Katika kukabiliana na gharama kubwa za uendeshaji na hali ya kiuchumi isiyotabirika, wamiliki wa sinema mara nyingi huchagua filamu wanazoamini zitarejesha fedha haraka. 

Mtazamo huu wa kibiashara unaacha nafasi ndogo sana kwa filamu za ndani hapa nchini ama zile za kikanda (Kwa maana ya Afrika), hasa zile zisizo na majina makubwa au kampeni za matangazo zilizoimarishwa. 

Matokeo yake, hadhira za Kiafrika hupata kwa nadra sana fursa ya kutazama sinema zao wenyewe kwenye skrini kubwa, isipokuwa tu, mpaka wakati wa tamasha au matukio maalumu. 

Kwa tafsiri nyingine ni kwamba, Ubora pekee wa filamu hautoshi kuhakikisha kuwa filamu hiyo ya kitanzania au kiafrika kupata nafasi ya kuoneshwa katika kumbi hizo. 

Kwa muda fulani, majukwaa ya mtandaoni kama vile Netflix, Apple, Amazon Prime, Showmax n.k yalionekana kuwa njia mbadala ya usambazaji, yakinadiwa kama suluhisho la kimapinduzi katika kuwaunganisha watengenezaji filamu moja kwa moja na watazamaji wao kwa vigezo vya kiufanisi, urahisi na gharama rafiki. 

Ajabu ni kuwa, ahadi hiyo sasa imeanza kupoteza nguvu. Kama zilivyo biashara nyingine, Majukwaa haya mengi ni ya kimataifa na yamekuwa yakijikita zaidi katika kuzalisha faida. 

Picha hii imebuniwa na akili unde ili kusanifu kinachozungumzwa na Mwandishi

Kadri majukwaa ya kimataifa yanavyojikita zaidi kwenye faida na ukubwa wa soko, ununuzi wa filamu umepungua na maudhui yamekuwa yakichujwa kwa ukali zaidi. 

Filamu kutoka Afrika na ukanda wa jumuiya za kusini zinazopata nafasi kwenye majukwaa haya mara nyingi huachiwa kimyakimya, bila msaada wa kutosha wa matangazo inayopelekea mwonekano mdogo katika mifumo ya mapendekezo. 

Hii inamaanisha kwamba, filamu kuwepo kwenye majukwaa hayo haimaanishi kuwa itaonekana.

Masoko na matangazo yamekuwa nguvu kuu inayobainisha hatima ya filamu. Katika mazingira ya vyombo vya habari, mwonekano ni mtaji. 

Watengenezaji wakujitegemea kwa kawaida hawana rasilimali za kuendesha kampeni ndefu za matangazo au kushindana na filamu zinazoungwa mkono na studio kubwa. 

Bila nguvu ya masoko, hata filamu zilizotengenezwa kwa ubora na zenye umuhimu wa kitamaduni zinaweza kutoweka ndani ya siku chache baada ya kuachiwa. 

Mfumo huu huthamini uwezo wa kifedha zaidi kuliko thamani ya kisanaa.

Hali hii inazidishwa na kupotea kwa filamu za bajeti ya kati. Hadithi nyingi za Kiafrika zinahitaji zaidi ya bajeti ndogo sana, lakini haziendani na matarajio ya uzalishaji mkubwa wa kimataifa au filamu za kibiashara za kiwango kikubwa. 

Mifumo ya ufadhili mara nyingi huwalazimisha watengenezaji filamu kuchagua kati ya miradi ya bajeti ndogo kupita kiasi au uzalishaji unaosukumwa zaidi na matakwa ya masoko ya nje na hadhira za kigeni.

Picha hii imeundwa kwa akili mnemba

Nafasi ya filamu zinazojengwa katika uhalisia wa ndani, zenye rasilimali za kitaalamu, na uhuru wa ubunifu imezidi kupungua.

Katika kukabiliana na vikwazo hivi, watengenezaji filamu wanaanzisha njia zao wenyewe za kuwafikia watazamaji. Maonyesho ya kijamii, vituo vya utamaduni, vyuo, maonsho yasinema ya kusafiri, na matamasha ya kikanda yamekuwa majukwaa muhimu ya usambazaji. 

Baadhi ya waandaaji wanajaribu kuachia filamu moja kwa moja kwa njia ya kidijitali kama vile YouTube, kupitia ushirikiano na vituo vya utangazaji au maonyesho ya mtandaoni yanayolipiwa kama ambavyo inasimamiwa na ShowMax au Azam Max. 

Wengine wanategemea matangazo ya kijamii na mahusiano ya karibu na hadhira zao, wakijenga uaminifu kupitia ukaribu badala ya ukubwa wa soko. 

Njia hizi zinaweza kuwa ndogo kwa ukubwa, lakini hujenga ushiriki wa maana na uimara wa muda mrefu.

Uendelevu wa juhudi hizi unaonesha ukweli muhimu. Hadithi zinazowakilisha maisha, lugha, na uhalisia wa watu wa Afrika bado zinahitajika sana. 

Tatizo si ukosefu wa hamu bali ni ukosefu wa fursa za kufikia hadhira. Watengenezaji wa filamu hawashindwi. Wanapambana na mfumo ambao haukuwahi kubuniwa kwa ajili yao.

Licha ya vikwazo vya kimuundo, watengenezaji filamu wanaendelea kuunda, kubadilika, na kudai kuonekana. Kazi zao zinapinga simulizi zilizotawala soko kwa muda mrefu na kupanua wigo wa vile sinema inaweza kuwa duniani. 

Kwa kufanya hivyo, hawasimulii hadithi tu, kimya kimya, wanaunda upya mustakabali wa usambazaji wa filamu katika namna ambayo haijawahi kudhaniwa hapo awali

Chapisha Maoni

Please Select Embedded Mode To Show The Comment System.*

Mpya zaidi Nzee zaidi