Na Mwandishi wetu
Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania, Dkt. Gervas Kasiga, ametoa wito kwa watayarishaji wa filamu, hususan watengeneza maudhui ya video mtandaoni (Content Creators), kujisajili kupitia Bodi ya Filamu Tanzania ili kutambuliwa rasmi na kupatiwa vibali halali vya upigaji picha jongevu katika maeneo mbalimbali nchini.
Akizungumza kupitia kipindi cha televisheni cha TBC1 — Jambo Tanzania, Dkt. Kasiga amesisitiza kuwa Bodi ya Filamu, kwa mujibu wa sheria na muundo wake, inawatambua rasmi Content Creators kama watayarishaji wa makala fupi za video zinazotumia picha jongevu kuwasilisha dhana, elimu, burudani na ujumbe kwa jamii.
Hata hivyo, amebainisha kuwa idadi kubwa ya Content Creators bado hawajasajiliwa na Bodi ya Filamu, hali inayowafanya kukumbana na changamoto katika utekelezaji wa shughuli zao za kurekodi maudhui katika maeneo mbalimbali nchini.
Kwa mujibu wa Bodi, wasimamizi wa maeneo husika wanahitaji vibali rasmi vya upigaji picha, ambavyo hutolewa na Bodi ya Filamu pekee.
“Vibali vya upigaji picha jongevu vinatolewa kwa mujibu wa sheria, hivyo ni muhimu kwa Content Creators na watayarishaji wote wa filamu nchini kujisajili ili kuepuka usumbufu unaojitokeza kutokana na kukosa vibali hivyo,” alisema Dkt. Kasiga.
Kupitia wito huo, Bodi ya Filamu Tanzania imewakumbusha watayarishaji wote wa filamu na Content Creators kujisajili ili kutambuliwa rasmi na serikali, kupewa vibali vya upigaji picha, kuunganishwa na fursa mbalimbali za mafunzo ndani na nje ya nchi, pamoja na kunufaika na faida nyingine za kifani, kisheria na kimasoko.
Hatua hii inalenga kuimarisha mazingira ya kazi kwa wabunifu wa maudhui, kuongeza uhalali wa uzalishaji wa filamu na video, na kukuza tasnia ya filamu nchini kwa misingi ya kitaalamu, ubora na ushindani wa kimataifa.