By Charles Mkoka
Katika kila kona ya Tanzania, kuanzia vijijini hadi mijini, kutoka sokoni hadi mashambani kuna hadithi zinazoishi, zenye uhai, zinazopumua, na zinasubiria tuu kusimuliwa, na hatimaye kuigizwa.
Ninaposema hivi simaanishi hadithi za mashujaa pekee, wala za watu mashuhuri, hapana.
Ninamaanisha stori za mtaani kabisa za mama ntilie, vijana wa bodaboda, wakulima, walimu, wasanii wa mitaani, na maelfu ya watu wa kawaida ambao maisha yao ya kila siku yana ujumbe wa kutuelimisha, maumivu ya kutuonya, matumaini ya kutupa hisia na ushindi wa kuamini, kuwa kuna mahali tunastahili kufika.
Filamu, ni sanaa ambayo (yes,ni kioo cha jamii, sikatai), lakini pia ina jukumu kubwa la kuzibeba simulizi hizi, na kuzileta kwetu, kwa kila mtanzania.
Kwa muda mrefu, tasnia ya filamu duniani kote imekuwa ikisimulia hadithi zenye tabaka au hadhi fulani, huku thamani kubwa ya maisha halisi, utamaduni na uhalisia vikiachwa au kupalaswa palaswa tuu kwa juujuu.
Leo hii, tuna fursa nyingine mpya na za kipekee za kurekebisha hili.
Tunaweza kusimulia hadithi zetu wenyewe, kwa sauti zetu wenyewe, na mtazamo wetu wenyewe. Na hili ni jambo jema sana.
Tunaona vijana wetu wakitengeneza skits, na reels fupifupi huko mitandaoni, huku zikibeba maudhui halisi, na kupata watazamaji wengi sana, wengine hata kupata majina makubwa, umaarufu na madili ya matangazo mbalimbali.
Maisha ni Filamu, na kila mtu ana stori, na kila stori inaweza kubadilisha maisha, muhimu kuwa na mwanzo, changamoto, mabadiliko, na matumaini, au na ka-ufundi kidoogo ka kunogesha mambo (utaalamu).
Tuna matukio meengi sana katika jamii yetu, mengi mno. Mazuri na mabaya. Haya matukio yote, ukikutana na wataalamu wanaweza kukuambia jinsi yanavyoweza kuhadithika na kugusa maisha ya kila mtanzania, na mengine hata kuwa fahari ya nchi. Hata nikitolea mifano ni mengi, mengi, mengi mno.
Hembu fikiria, useme unaanza kugusa kila sekta kwenye uchumi, afya, mazingira, utamaduni, sanaa, michezo, ushafirishaji, na kadhalika na kadhalika katika kutafuta masimulizi...unadhani itakuwaje?
Ni labda nadhani tuna wajibu wa kujifunza zaidi na kuwabana bodi ya filamu na wadau wengine kutufundisha kupitia semina, mafunzo na makongamano, ili kujua na kuziona fursa zote muhimu katika filamu.
Kwa watayarishaji na wataalamu wa filamu nchini, hii ni hazina isiyotumiwa ipasavyo. Inashangaza kuona tukin'gan'gana kwenye vitu tunavyoona vimewezekana wakati sekta zingine hakuna hata anayejaribu.
Si kila kitu kiwe cha uswahilini pekee, au mapenzi pekee, au uchawi pekee. Tuna genre nyingi sana za kufanya ikiwemo Mystery, Action (Kupigana, ambayo kiukweli zilianzaga vizuri ila kwa sasa sioni kazi za kutosha za action, nadhani kwa sababu mbalimbali za kitaalamu), Drama (hii ndio uti wa mgongo halisi wa filamu), adventure (Matukio), Crime (Uhalifu), horror (Kutisha), thriller (kusisimua), sci-fi (Sayansi) na zingine nyingi sana.
Na kuzifanya sio lazima kuiga holywood au bolywood, hapana. Ni suala la kujitafuta na kuweza. Mbona Nigeria wameweza kutengeneza genre za kikwao na soko lao linalofanya vizuri kupitia filamu zenye dini, au kuchekesha, au maisha ya kisasa ya mjini? Au south Afrika na filamu za familia na kuchekesha? au hata Zimbabwe wanavyotengeneza filamu zenye maudhui mengi (kikamilifu).
Naamini kuwa Tanzania tunaweza kuwa wakubwa zaidi katika sekta ya filamu kuliko tunavyodhani kama tukiwekeza nguvu kubwa kwenye kuongeza uelewa na kutengeneza miundo mingi inayofanya kazi. Hili ni la kwetu na lipo ndani ya uwezo wetu.
Maendeleo ya vifaa, na wataalamu yanakujaga automatically ukishakuwa na miundo sahihi, nadhani. Serikali inaweza kujenga mazingira wezeshi katika kulifanikisha hili, na naamini kwa nguvukazi kubwa ya vijana, tunaweza kulifikia kwa haraka na kunufaika na sekta hii mapema kuliko tunavyodhani.
Tuna bahari ya simulizi halisi zinazotokana na maisha ya Watanzania, na kubeba utamaduni, sanaa na hadhi yetu kama taifa linalokua kwa kasi sana kiuchumi, na kiutawala kwa Afrika nzima.
Hii si kwa serikali na watumishi wa umma pekee, bali hii ni kwa kila mtanzania anayetazama au kufikiria kutengeneza filamu, kusimulia na hata kunufaika katika sekta hii, kwa pamoja, tunaweza kufanya makubwa zaidi.
Filamu nzuri haiburudishi tu; huelimisha, huponya, huunganisha na huhoji. Inapobeba visa halisi, (au vilivyofikiriwa kwa umakini) inaonyesha hali zetu, maamuzi yetu, makosa yetu na matumaini yetu, na hata ubora wetu, na hii inatupa fursa ya kujitazama, kujirekebisha na kujivunia tulikotoka.
Kwa Tanzania, filamu zetu zinaweza kuhifadhi tamaduni na historia; Kukuza lugha ya Kiswahili kimataifa, kuibua vipaji vipya nchini, kujenga maelewano na mshikamano wa kijamii, na mengine mengi
Leo, ulimwengu unatafuta hadithi halisi, za kweli, zenye mizizi ya kiutamaduni. na tukijitathimi, vyote ulimwengu wanavyotaka tunavyo. Tumeshuhudia wakorea wakipanda juu kwenye soko la tamthilia na baadae filamu, na kufanikiwa, soko la kimataifa halina mwenyewe, linahitaji utofauti, uhalisia na sauti mpya.
Hata Holywood walilishikilia kwa muda mrefu, na bado linawaponyoka mara kadhaa tuu, vivyo hivyo tumeona kwa Bolywood, hadi Telugu walivyopanda thamani na kutajirika.
Tanzania ina kila kitu: mandhari, lugha, historia, na watu wenye simulizi nzito kwelikweli. msishangae hata Idris Elba alionesha nia kuja kuwekeza nchini mwetu
Inawezekana kabisa story kutoka Katavi ikawa filamu nzuri na ya kukuna vichwa vya wengi huko Cannes au Los Angeles na kubeba tuzo kadhaa, inawezekana, na tena bila ya hata kuhitaji makamera makubwa ya holywood au waongozaji filamu wa kimataifa.
Huu ni wakati wa kuandika hadithi, visa na mikasa ya watu wetu. Ni wakati wa kusikiliza, kuhoji, na kuheshimu simulizi za jamii. Ni wakati wa kuacha kufikiria kwamba stori fulanifulani “hazifai kuwa filamu.” mi naamini kuwa Hakuna hadithi ndogo, bali kuna hadithi ambazo hazijawahi kusimuliwa bado.
Zipo nyingi sana, na ninaposema hadithi simaanishi zile za hapo zamani za kale sungura na fisi, na hata hizo naamini zipo ambazo ulimwengu haujazisikiliza bado, na wanatamani kuzikiliza au kuziona kwa uhalisia wa kipekee.
Wataalamu, waandishi, waongozaji na mafundi wengine kwenye filamu, tembeeni mitaani, Sikilizeni simulizi za wazee, vijana, wanawake, na watu wa makundi maalum, watoto, na hata wale waliosahaulika.
Mnaweza kugeuza maisha ya kawaida kuwa kazi za sanaa zenye nguvu. Mwisho wa siku, filamu sio tuu kamera na Runinga (screen), filamu ni sauti, na kila mtu anayo.
Tanzania ina hadithi zisizohesabika. Sasa ni wakati wa kuzisikia, kuziheshimu, na kuzileta kwenye skrini. Kila mtu ana hadithi, na kila hadithi inastahili kusimuliwa.