Na Mwandishi wetu, Shinyanga
Kikundi cha sanaa cha SHY TALENT FILMS kimeendelea na mazoezi ya kina ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kutengeneza filamu na tamthilia mpya zitakazolenga kuelimisha na kuhamasisha jamii kupitia sanaa.
Mazoezi hayo yamefanyika katika mazingira ya nidhamu, mshikamano na ushirikiano mkubwa miongoni mwa wanakikundi, yakilenga kuimarisha uwezo wa uigizaji, mawasiliano ya jukwaani pamoja na uelewa wa kina wa ujumbe unaotarajiwa kufikishwa kwa jamii.
Tukio hilo lilihudhuriwa na Mtendaji wa Mtaa wa Miti Mirefu, Angelight Emmanuel Mwanri, ambaye baada ya kushuhudia mwenendo wa mazoezi aliwapongeza vijana hao kwa juhudi na ari kubwa wanayoonesha.
Mazoezi hayo yalishirikisha Katibu wa SHY TALENT FILMS, Daniel Sibu, Mkurugenzi wa Misalaba Media, Mapuli Misalaba, pamoja na Mwenyekiti wa SHY TALENT FILMS, Daniel Elimboto, sambamba na walimu wa kikundi hicho akiwemo John Jackson, ambao waliendelea kutoa miongozo na maelekezo kuhakikisha kazi zinazotarajiwa zitakuwa na ubora wa juu na maudhui yenye tija kwa jamii.
SHY TALENT FILMS inaendelea kujijengea taswira kama jukwaa muhimu la kukuza vipaji vya vijana, huku ikiitumia sanaa kama chombo cha kuelimisha, kuhamasisha na kuijenga jamii ya Manispaa ya Shinyanga na Tanzania kwa ujumla.