Tanzania Creators Awards imezinduliwa rasmi leo na Best Brand Africa, ikiwa ni jukwaa jipya la kutambua, kuthamini na kuenzi mchango wa watengeneza maudhui ya mitandao ya kijamii nchini.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mwenyekiti wa Best Brand Africa, Zakayo Shusho, alisema kuwa lengo kuu la tuzo hizo ni kupima impact, value na mchango halisi unaotolewa na mtengeneza maudhui kupitia kile anachowasilisha mbele ya kamera.
“Tumejikita kupima kama mtengeneza maudhui anafanya vizuri katika maeneo matatu: To educate, to inform and to entertain. Tunakwenda kumpongeza yule anayeleta mchango chanya na wa thamani kwa jamii,” alisema.
Alisisitiza kuwa watengeneza maudhui hawatapimwa kwa idadi ya wafuasi, umaarufu au hamasa pekee, bali kwa mchango na athari wanayoacha katika jamii.
Watanzania watapiga kura kwa washiriki watakaochaguliwa, na mshiriki atakayepata kura nyingi zaidi ndiye atakayetwaa tuzo katika kila kada.
Uzinduzi huo pia umefungua rasmi dirisha la mapendekezo kwa wananchi wote.
“Tuna zaidi ya segment 15, na tumezipitia ili kuhakikisha zina mchango chanya kwa Watanzania. Ndio maana pia tunapokea maoni au ushauri wa kuboresha au kupunguza pale inapobidi,” aliongeza.
Kwa mujibu wa waandaaji, tuzo hizi zinatarajiwa kuongeza hadhi kwa watengeneza maudhui na kuwafanya kuvutia zaidi kwa wafanyabiashara, wadau na makampuni yanayotamani kufanya kazi nao.
Kamati ya maandalizi pia imetambua BASATA pamoja na wadau wengine kama walezi muhimu katika mchakato wa upimaji na uteuzi wa washiriki sahihi.
Kwa mujibu wa ratiba, kuanzia Januari 17 hadi 23 dirisha la mapendekezo litakuwa wazi rasmi. Januari 24 hadi 26 kutakuwa na mchakato wa judging (udahili), huku Januari 27 hadi 30 majina ya waliochaguliwa (nominees) yakitangazwa. Baada ya hapo kutakuwa na siku 10 za kupiga kura, kabla ya kilele cha tuzo zitakazofanyika Mlimani City.
Sekta zitakazohusishwa ni pamoja na:
Vichekesho na video fupi (Skits); Muziki na Kucheza (Dance); Elimu na Mafunzo; Mtindo wa Maisha (Lifestyle) na Fashion; Misosi na Mapishi; Utalii na wapenda Kusafiri (Travel Culture); Michezo na Mazoezi; Matibabu na Afya; Ujasiriamali na Biashara; Visual Creators (motion & graphics designers, wachora vikatuni); Waandishi wa Habari na Watangazaji; Waandaaji sherehe na kupamba; Urembo na Vipodozi ; Filamu na Tamthilia; Branding and Uhamasishaji (influencing) — jumla ya kada 15.
Tuzo hizi zinatarajiwa kuendelea kufanyika kwa miaka ijayo, kulingana na sapoti kutoka kwa wadau, wazazi, walezi, Bodi ya Filamu, BASATA na washirika wengine.
Godfreu Pius, maarufu kama King Hati, alisema kuwa tuzo hizi zinapaswa kutazamwa kama fursa ya kukubalika na kukua kwa watengeneza maudhui.
“Lengo la waandaaji ni kututambua sisi na mchango wetu chanya kwa jamii. Uwepo wa categories nyingi unaonesha umuhimu wa tuzo hizi kugusa kila sekta ya jamii,” aliongeza.
Alisema pia kuwa tuzo hizo zinarasimisha ushirikiano kati ya makampuni makubwa, wafanyabiashara, wadau na watengeneza maudhui wa ngazi zote.
“Kushirikisha kila mtu kunatia hamasa kwa kila mtengeneza maudhui. Ni wajibu wetu kujitokeza kushiriki ili kuchangia maendeleo yetu,” alisema.
Kwa upande wake, Happines Mwita kutoka kampuni ya Sarufi, inayotengeneza conversational AI chatbot, alisema kampuni yao imepewa jukumu la kusimamia mifumo ya kuhamasisha upigaji kura.
“Tumeunganisha mifumo yetu ili kurahisisha zoezi zima la kuhamasisha kupiga kura. Mwananchi ataanzia kwenye post ya Instagram, ataona link itakayompeleka WhatsApp, ataandika ‘Nominate’, na atapatiwa maelekezo na machaguo ya kupiga kura,” alieleza.
Naye Emmanuel Ndumukwa kutoka Bodi ya Filamu na Michezo ya Kuigiza alisema mashindano haya yanaongeza ushindani, ubunifu na thamani katika jamii.
“Mshindi atafanikiwa kukuza ‘mileage’ yake ndani na nje ya Tanzania. Kwa upande wetu, tunashauri watengeneza maudhui wote warasimishwe kwa kufuata utaratibu uliowekwa,” aliongeza.
Alifafanua kuwa Bodi ya Filamu ina mfumo unaoitwa AMIS, unaowezesha kurasimisha watengeneza maudhui wote wa picha jongevuni nchini.
Afisa Sanaa Mwandamizi kutoka BASATA, Bw. Abel Ndaga, alisema anaunga mkono juhudi hizo huku akisisitiza umuhimu wa maadili kwa watengeneza maudhui.
“Kumekuwa na changamoto ya baadhi ya watengeneza maudhui kutozingatia maadili, ilhali maadili ndiyo msingi wa taifa letu katika kujenga jamii yenye uadilifu,” alisema.
Aliwasihi wasanii wote kuzingatia mila, desturi na maadili ya Kitanzania, akisema hilo litafungua milango ya fursa hata katika ngazi za kimataifa.
BASATA pia imesisitiza washiriki wote kupitia na kufuata mwongozo uliowekwa mtandaoni ili kuhakikisha mchakato unaeleweka kwa wote.
Akijibu maswali, Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi Bw Zakayo alisema kuwa asilimia kubwa ya watengeneza maudhui ni vijana na wamekuwa wakitumia teknolojia kwa ufanisi mkubwa.
“Tumeungana na Sarufi kuanzisha chatbot ya WhatsApp inayozungumza na mtu moja kwa moja, kuanzia Instagram DM ya tuzo hizi. Hii itarahisisha sana elimu na uhamasishaji wa upigaji kura nchi nzima,” aliongeza.
Alimalizia kwa kusema kuwa waandaaji wamejumuisha wataalamu wengi kutoka nyanja mbalimbali ili kuhakikisha mchakato wa kuwarasimisha watengeneza maudhui unakuwa wa kitaalamu, wa haki na wenye tija.