Biggy Matovolwa aingia TAFFA mara mbili: “Bado najitafuta katika tasnia”

Msanii Lumole Matovolwa (Biggy) akiwa jukwaani kwenye mchezo wa kuigiza nafasi ya mfalme wa Pate, kwenye kitabu cha Fumo Liongo 

 By Charles Mkoka

Msanii mkongwe wa filamu na tamthilia, Lumole Matovolwa @kobisi_kikala, maarufu kama Biggy Matovolwa, ameonesha unyenyekevu wa hali ya juu baada ya kuteuliwa (nominated) katika vipengele viwili vya Tuzo za TAFFA msimu huu, akisisitiza kuwa bado ana safari ndefu katika tasnia ya filamu nchini.

Akizungumza na Sauti za Filamu kwenye mahojiano maalum (exclusive interview), Biggy amesema kuwa uteuzi huo si ushindi binafsi pekee, bali ni ushahidi wa mchango wa wadau wote wanaoendelea kuijenga na kuiinua sekta ya filamu Tanzania.

“Pongezi ziende kwa wote wanaohusika. Hizi tuzo zinachochea ukuaji wa tasnia yetu, na zinatoa motisha kwa wasanii na wadau kwa ujumla,” amesema.

Biggy, ambaye amedumu kwenye tasnia kwa miongo kadhaa, alipoulizwa iwapo sasa ndiyo muda wa kuvuna matunda ya kazi yake ndefu, alijibu kwa kauli iliyojaa tafakuri na unyenyekevu:

“Mimi bado najitafuta katika hii industry. Bado sana… tena bado mno. Sijui nisemeje, ila mimi bado,” alisisitiza.


Kwa wasiomfahamu, Lumole (Biggy) amekuwa kwenye kazi nyingi sana za filamu za kitaifa na kimataifa, na amekuwa akichukulia sanaa ya uigizaji very seriously, na pia kuhusika kwenye kazi mbalimbali za uigizaji wa sanaa ya jukwaani kwenye matamasha na matukio mbalimbali ya kimataifa.

TAFFA Awards zimefanyika kwa misimu minne mfululizo, na Biggy aliteuliwa msimu wa pili pekee, ambapo Jacob Steven JB alikuwa kinara wa Chaguo la Mtazamaji huku Kojack akitwaa tuzo ya Msanii Bora wa Kiume wa Tamthilia.

Akizungumza kuhusu heshima ya kuendelea kutambuliwa, Biggy amesema sapoti ya jamii ndiyo inayochochea kuimarika zaidi kwa kila msanii wa maigizo.

“Ni heshima kuona watu wana-support unachokifanya. Inatia moyo kuona jamii inatambua mchango wako katika sanaa,” amesema.

Ameongeza kuwa uteuzi wa msimu huu kama ilivyokuwa msimu wa pili, unapaswa kuimarika huku akitoa wito kwa majaji na wapiga kura kuzingatia kufanya vizuri kwa washindani kwa mwaka husika.

Msanii Lumole Matovolwa katika tukio akirekodi baadhi ya vipande vya Tamthilia ya Kombolela inayorushwa na Azam TV (PICHA na Azam TV)

“Nawapongeza wote wanaowania tuzo. Ushindi uamuliwe kwa kuangalia nani amefanya vizuri kwenye msimu husika,” alisisitiza.

Kauli hiyo ameielekeza kwa wapiga kura wa Chaguo la Mtazamaji, wadau wa filamu, pamoja na majaji wa vipengele vingine vyote.

Akigusia maandalizi ya tuzo hizo, Biggy ameipongeza Bodi ya Filamu Tanzania kwa juhudi zake, huku akisisitiza umuhimu wa taaluma na uadilifu ili kuepuka migogoro isiyo ya lazima.

“Nimehudhuria TAFFA tangu msimu wa kwanza kule Mbeya, baadae Arusha hadi sasa Dar es Salaam (kwa mara mbili mfululizo). Juhudi zinaonekana, lakini pia malalamiko yapo. Ushauri wangu ni kuyaangalia madhaifu ili yapungue, siyo yaongezeke,” amesema.

Biggy, ambaye kwa sasa anaendelea kung’ara kwenye tamthilia ya Kombolela, ametoa wito mzito kuhusu matumizi ya weledi katika utoaji wa tuzo.


“Sio wapiga kura tu, hata waandaaji watumie taaluma zao. Tusigawe tuzo kwa mihemko au mashinikizo. Anayestahili kupewa na apewe, sio mimi tu, bali yeyote aliyefanya vizuri kwa mwaka huu.” ameongezea.

Kwa mujibu wa ratiba, Tuzo za TAFFA 2026 zinatarajiwa kufanyika Februari 14, 2026, katika ukumbi wa Superdome, Masaki, Dar es Salaam.

Akizungumzia kauli ya Rais wa Shirikisho la Filamu ( ingawa si kwa lazima) kuhusu uwezekano wa washindi kupewa bahasha (fedha), Biggy amesema hilo ni jambo jema na la kuhamasisha pia.

“Nadhani neno sahihi ni kuwa wanaliangalia. Tumeona sekta nyingine kama wachekeshaji na waandishi wa habari wakipewa fedha kama sehemu ya pongezi. Kwenye filamu naamini inawezekana pia,” amesema.

Mwisho, Biggy amewaomba wapiga kura na wapenzi wa filamu kuhakikisha ushindi unaenda kwa anayestahili zaidi, ili kuendeleza heshima, uwazi na ukuaji wa tasnia ya filamu Tanzania.

Chapisha Maoni

Please Select Embedded Mode To Show The Comment System.*

Mpya zaidi Nzee zaidi