Ni
siku nyingine mpya katika mji huu wa Bagamoyo, Mji wenye utajiri wa historia ya
kale, watumwa na kisima cha zamani kisichokauka maji, magofu pamoja na hoteli za
kisasa zilizojengwa katika kipindi hiki na kuufanya mji kupata sura mpya lakini bado ule ukale uanaowavutia
wazungu wengi kuja kutalii bado unaonekana.
Bagamoyo ni mji ulio kandokando ya bahari ya Hindi, bahari
iliyopambwa na mikoko ukingoni mwake na pia chuo pekee cha sanaa mjini hapa TASUBA ni kimbilio
la wasanii wengi toka mikoa mbalimbali ya nchini Tanzania.
Huwa
ninaendaga mara nyingi kumtembelea mtoto wangu anaeishi hapa na kama kawaida ya siku nyingine zote, niliamshwa asubuhi na mwanga uliopenya
kupitia pazia zuri na jepesi lililowekwa dirishani huku kiupepo chepesi
kikinipiga na kunifanya nihisi baridi flani hivii...kitu ambacho sio cha kawaida, maana kila siku huwa
nakifurahia hiki kiupepo lakini nashang’aa leo nahisi baridi! Mmh!? Kuna
jambo!
Niliamka
pale kitandani na kuhisi maumivu katika viungo
na mwili haukuwa katika hali yake ya kawaida. nilitoka nje baada ya
taratibu za usafi na kumsalimia mwanangu Anita na kumweleza kinachonisibu.
“najihisi
naumwa, sijui ni nini.. lakini aah, tuache tu
hii hali itapita”
Anita
hakukubali, aling’ang’ania uamuzi wake wa kunipeleka hospitali na hatimae
ilinibidi nikubali na kwa pamoja tuliongozana wote hadi kwa daktari ambae aliponiona
tu alisema.
“mama
mjata si wiki iliyopita tu tulipima malaria na ukawa huna? lakini
sio mbaya tukipima tena”
Nilienda
kupima na kukutwa na malaria ambayo kwa umri kama wangu huwa inaambatana na
shoga yake presha! Nikalazwa.
Nilipofika
wodini na kupewa kitanda nilishangazwa na sauti ya mkoromo uliosikika hivyo
nikaanza kuangalia majirani zangu upande huu na ule na kumwona bi mkubwa mmoja
akiwa katika hali mbaya ndie anaesababisha mkoromo huo! sikuweza kwenda
kumwangalia kwa vile nilishatundikiwa dripu hivyo nikawa naishia kumsikiliza
huku nikimwombea kimya kimya.
Anita
ilibidi arudi nyumbani kwa ajili ya kuandaa chakula maana nilikuwa na njaa sana
na daktari alishauri nipate chakula kutokana na madawa ninayotumia, hivyo nikabaki
peke yangu nikiiangalia dripu inavyoteremka tone baada ya tone.
Kawadia
ya mfanyakazi yeyote anapopatwa na tatizo kama hili la kuuguliwa inabidi arudi
kazini na kuomba ruhusa au kutoa taarifa kuwa hatakuwepo kwa muda akamhudumie
mgonjwa kisha atarudi, na ndivyo alivyofanya Anita na baada ya kupewa ruhusa
alirudi nyumbani na kuanza kazi ya kuandaa chakula cha mgonjwa.
Ghafla nilisikia ukimya ukitawala na ile sauti ya mikoromo niliyoisikia mwanzoni haikuwepo tena ! mmh!
Kuna jambo! nikajiuliza he! Ina maana
bi mkubwa amefariki? Maskini! Rooho iliniuma sana ingawa sikuwahi kuiona
hata sura yake.
Nesi
alikuja na kumshughulikia Yule bi mkubwa na wakamtoa na kumpeleka panapo husika
wodi ya mwisho hospitalini inayoitwa mortuary. Wodi ambayo kila nafsi itaingia hata ukiwa mjanja vipi?
kawaida ya ukarimu wa watanzania muda wa kazi
ulipoisha wafanyakazi wenzie Anita walikuja hospitali kuniangalia mama wa mfanyakazi
mwenzao ambao pia walinifahamu, kiukweli nani asiyenifahamu Mama Mjata mie?
Mmoja
wapo wa wafanyakazi hao alimwona nesi Yule aliemhamisha bi mkubwa wodini
aliyefariki wakamwomba ili awape ruhusa waweze kuniona kwa vile muda ulikuwa bado kidogo wa
kuruhusiwa kuona wagonjwa.
“mama
nesi tunaomba tukamwone mama wa mfanyakazi mwenzetu mwl. Mhina amelazwa hapa”
Nesi
bila ya kuwaza mara mbili akatamka “aah! Mbona yule mama amefariki”
Wakastuka
wote na kutaka kujua zaidi kuhusu kifo na nesi aliwahakikishia kuwa ni kweli amefariki
na wametoka kumpeleka mourtuary sasa hivi.
Mwenye kulia alilia mwenye presha ilipanda ili
mradi kila mwenye kuupokea msiba kwa staili yake aliupokea lakini mwisho
walipeana moyo wakafuta machozi na safari ya kwenda kwa Anita ilianza.
Huku
ndani wodini mimi nimekaa njaa sasa inanikwangua sana, nikafikiria kumwomba nesi
akaninunulie walau chips lakini nikajitia moyo kuwa mwanangu si analeta chakula
ntakula tu. mfano nikinunua chips, nikala, nkashiba yeye akija na chakula halafu
akaona sili si atajisikia vibaya? na nitakuwa kama nimemsumbua bure.... ngoja tu
nijikaze, nilijiwazia peke yangu.
Lakini
pia wasiwasi ukaanza kunishika.... mbona anita ametumia muda mwingi sana toka
alipotoka hapa nikizingatia kuwa sio mbali kutoka hospitali na nyumbani kwake?
au kuna lolote limemkuta? Au kapata ajali kwa vile anatumia usafiri wa bodaboda?
Nikaanza kujitisha inawezekana kapata ajali? Ndio atakuwa amepata ajali maana
haiwezekani kuchelewa hivi.
Wafanyakazi
wanaofanya kazi na Anita walifika nyumbani na kumkuta Anita yuko busy
anamalizia kufunga chakula ili arudi hospitali huku akionekana wazi hana habari
za kifo cha mama yake mpenzi. Wakaangaliana
na kukosa la kusema, maana walitegemea watakuta kilio au walau vitu vimeshatolewa
nje na pilika za maandalizi ya msiba yanaendelea lakini haikuwa hivyo
wakaangaliana na mmoja akajitia moyo na kutamka.
“Anita
lete hicho chakula sisi tupeleke wewe baki hapa upumzike maana utakuwa umechoka
sana”
Kabla
anita hajapata nafasi ya kujibu chakula kilishachukuliwa na mchukuaji kisha
ondoka nacho. Wengine wakajikaza lakini msiba ni msiba huwezi kujikaza lazima
mmoja atashindwa kuzuia machozi yake ikabidi wamkalishe mfiwa chini na
kumweleza kilichotokaea kwamba mama hatunae tena duniani!
Wewe
hukuwepo lakini malaika wako alikuwepo Anita kwanza alistuka pili hakuamini
tatu hakuelewa kwa mara moja inakuwaje? Kwa homa ile ile? Au presha au? Mama yangu
mimi kaitoka? kilio kilipamba moto na
ndipo hakukuwa na siri tena ila ni kweli mama amefariki ndipo sasa msiba
ukaanza kukusanya watu na majirani,wenye kumlilia mama, bibi, mwalimu, msanii
mashuhuri, shangazi ili mradi ikawa mtafaruku kilio kimepamba moto. Kumbuka hapa ni bagamoyo hivyo mara moja simu
ikapigwa dar na Tanga na Tanzania nzima pia habari zikafika chuo cha sanaa bagamoyo (tasuba)
na raisi wa wasanii chuoni hapo akaziweka kwenye mtandao na huko dare s salaam
akina natasha na caftany wakazipata pamoja na wasanii wengine na ghafla R.I.P.
zikaanza kutupiwa kwenye mtandao kwa fujo kila mmoja akijaribu kuonyesha upendo
wake kwa marehemu.
Wodini
mimi njaa inazidi kukwangua na woga nao ukinitawala mbona Anita amechelewa
itakuwa ni ajali tu na kwa vile simu ilizima na sikuona sababu ya kuichaji
maana ni mgonjwa itanisumbua tu kumbe huko nje watu wanapiga simu yangu na
wanapoona haikuwa hewani wanajua hakika nimekufa.
Ndugu
wa dar wakatafuta usafiri na kuanza safari ya kuja bagamoyo msibani.
Jambo
limezua jambo!
Mchungaji
na wasaidizi wake ambao wana ruhusa ya kuingia wodini muda wowote alikuja akiwa
katika ratiba yake ya kawaida huku akiwa ameshapata habari za msiba kwa vile
ananifahamu na huwa tunasali pamoja
akawa anapita kuwaombea wagonjwa labda akiwa na mawazo akimaliza ratiba yake
hapa ndio aende msibani, katika pitaptia yake akaniona akastuka kidogo ila kwa
vile ni mchungaji akajikaza na kuja
kunisalimia na tukafanya maombi pamoja
na alipomaliza akaondoka akiwa amepoteza uchangamfu wake wa kawaida.
Mchungaji
alienda moja kwa moja msibani na kukuta watu wako busy na kilio.mchungaji
akaamua kuwanyamazisha bila mafanikio.
“amani
iwe kwenu” vilio villiendelea .
Ikabidi
atumie nguvu ya ziada na kuwanyamazisha na waliponyamaza akawaambia ukweli
ulivyo kuwa mama hajafa ni mzima wa afya hospitalini, habari zikaanza tena
kuvuma kuwa badala ya rest in peace sasa ni live in peace na badala ya machozi
ya kilio sasa yakageuka machozi ya furaha!
Rais
wa wasanii bagamoyo tasuba akamtuma mwalimu hospitali kuja kuthibitisha na aliniona na nikaongea nae ingawa haya yote
yanafanyika hakuna mtu alieniambia chochote hivyo mimi sikuwa najua kama
nimekufa na kufufuka na kila anaekuja ingawa anastuka lakini hawaniambi ingawa nilishangazwa na hali iliyojitokeza
ghafla watu wakaanza kuja wodini wanachungulia madirishani wakiniangalia mimi
nikadhania kwa vile ni staa kama kawaida
ya wapenzi wetu huwa wanafurahi kuniona kumbe wenzangu walikuwa wanashang’aa
mimi kuwepo hai. mwalimu wa chuo
alietumwa alipopata uhakika akarudi chuo
na kumwambia rais wa wasanii tasuba na akabadilisha tangazo la kifo mtandaoni .
Usiniulize
wale waliokuwa njiani wakitoka dar kuja msibani bagamoyo maana walifika kweli,
mkanganyiko uliotokea tanga na Tanzania nzima kwa wale wanaonifahamu utajaza mwenyewe.
Swali
ambalo wengi walijiuliza ilikuwaje mpaka haya yote yakatokea?
Kwanini
nesi ajibu kuwa nimekufa wakati niko hai?
Ni
kweli nesi hakuwajibika na alikurupuka?
Sikiliza
nikwambie kilichotokea mpaka hali ikafikia hapa ilipofika
Nililazwa
hospitali nikiwa nasumbuliwa na malaria na simu yangu ilikuwa haina chaji
nikaizima na sikuiwasha tena, hili lilikuwa jipu la kwanza.
Mimi
naitwa mama mjata na mwanagu anaitwa Anita
au mwl. Mhina na Yule bi mkubwa aliefariki anaitwa ne Mhina.
Kwahiyo
kwa lugha nyepesi unaweza sema mama mzazi wa mwl.Mhina anaitwa ne mhina! Nesi akaunganisha! Simple as that! Lakini hakujua kuwa kosa alilofanya
liliathiri taifa zima!
Na
hili linaweza kuwa jipu letu wote sio
nesi peke yake ila watanzania wote. TUTAFAKARI KABLA YA KUTAMKA CHOCHOTE. ULIMI NI KITU KIDOGO LAKINI KINAWEZA
KUSABABISHA BARAKA,LAANA AU MAUAJI YA KIMBARI.
Habari
hii imeandikwa na Susan Natasha Humba kwa niaba ya mama mjata
alienihadhithia mwenyewe.
Nina
mshukuru Mungu kwa ajili ya mama Mjata ni mama mwema, mpole na muelewa na
tumepewa tena huyu mama na Mungu ili tuendelee kuchota hekima na Baraka zake, nakuombea
uishi zaidi na zaidi ili jina la bwana lizidi kubarikiwa kupitia wewe.
