MIMI NA ANGOLA - MVUA YAZINGUA




SEHEMU YA NNE;

Tulizunguka mjini mpaka jioni tukarudi hotelini kujitayarisha kwa safari ya kesho yake…..

Hii ni hadithi ya maisha yangu ninayoiandika  mimi mwenyewe.
Susan natasha humba.
 Sasa endelea na sura ya tano ya mimi na Angola……


Siku   iliyofuata tuliwasili  katika uwanja wa ndege wa Lusaka, ilikuwa ni saa 8 mchana na siku hiyo kulinyesha mvua kubwa sana kiasi tukaanza kupata wasiwasi kama ndege itafanya safari maana zingine kadha zilikuwa zimeshafutwa.tulikaa airport tukisubiri hatima yetu kwa masaa hadi tuliposikia tangazo la kuingia ndani ya ndege.

 Tuliingia ndani ya  ndege  ya kirusi Aeroflot
 na kupaa mawinguni tayari kwa safari ya Angola, na kuwasili saa 2 usiku na kupokelewa na afisa wa ubalozi na kutupeleka katika nyumba tuliyofikia ambayo kumbe ilikuwa ni hapo hapo ubalozini.
Ubalozi wa Tanzania ulikuwa katika barabara ya silver de porto ukiwa katika  Jengo la ghorofa tano, chini ni ubalozi na juu ni makazi ya wafanyakazi wa ubalozi.  Kama kawaida utalitambua kwa kuona bendera niipendayo ya taifa letu ikininginia ingawa ilikuwa imechoka na kupoteza uzuri wa rangi zake!
 Tulipelekwa moja kwa moja  ghorofa ya tatu na kutua mizigo yetu.
Kwa vile ilikuwa usiku tulijipangia vyumba na kulala moja kwa moja.
Mwaka 1980 tulianza rasmi  ukazi katika nchi ya ugeni.

Angola nchi ambayo kwa huku kwetu kabla hatujaondoka tuliijua kama ni nchi ya Augustino Neto iliyotawaliwa na wareno kwa miaka mia tano na kufanya lugha ya taifa kuwa kireno pia inatawaliwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe kwa lugha nyepesi yaani amani ilikuwa ni msamiati mgumu kueleweka.
Magaidi wakiongozwa na Mwasi Savimbi walikuwa wanaisumbua  sana serikali ya Angola kwa kupigana vita vya msituni kwa miaka kadhaa.
Sasa nakupa mtazamo wangu nilipofika Luanda,ambao ni mji mkuu wa  Angola.kwanza ni amani tupu wala huwezi jua kama kuna mtu anatumia risasi mahali Fulani ili aishi.  Rais ni Eduardo dos Santos, ni nchi nzuri iliyotawaliwa na majengo mengi ya ghorofa  na nimejitahidi kila ninapopita nione kama kuna nyumba ya udongo sikuwahi kuiona zaidi ya nyumba za chini chache.  Ujenzi wa nyumba zao wanatumia milango mingi kama kiunganishi cha chumba na chumba unaweza kukuta sehemu inayotakiwa kuwa na mlango mmoja wao watajenga mitatu!   marmar za ukutani ni jambo la kawaida katika kuta za nyumba zao.
Luanda iko pembezoni mwa bahari ya Atlantiki inayosifika kwa samaki wengi na watamu huko niliwaona  samaki wanaoitwa Kashushu ni samaki pendwa watamu zaidi ya sato maana kwangu sato ni samaki pendwa.kuna sardina na karapau achilia mbali kamba na kambakoche wanaopatikana kwa wingi, kwa wiki tulikuwa tukinunua kiroba cha samaki mpaka nikawa napika sambusa za samaki kila mwishoni mwa wiki!  Maana usipomaliza kiroba hiki kitakutana na kingine cha wiki ijayo, kuna samaki maalum kwa ajili ya kuchoma tu  upo hapo?
Kwenye hiyo pwani kuna sehemu ambayo ardhi imeingia baharini wenyewe wanaita ilha (tamka ilya) pana pendeza sana na hiyo sehemu haina kazi nyingine zaidi ya watu kwenda kushuhudia jua linavyozama tu!  (sunset)
Kwa upande mwingine wa bahari kuna hoteli nzuri iitwayo Panorama ukiiangalia kwa woga unaweza kudhani iko ndani ya bahari na pia upande mwingine kuna matanki makubwa ya mafuta ya petrol.
Usafiri wa mabasi  na sikuwahi kuona  taxi labda kwa vile sikuwa nazihitaji!  Na kwa upande wa daladala  sikuwahi kupanda basi hata mara moja hivyo siwezi kuelezea adha wanazozipata kama za madaladala yetu hapa.
Cha ajabu hakukuwa na maduka yanayayouza nguo,chakula wala vifaa muhimu vya matumizi ya kawaida.bado ile hali kama ya bongo tulipoondoka ya kufunga mikanda ilikuwa inafanana tofauti tu ni wale wako vitani,kwa sisi wageni wa  nchi za nje tulikuwa na duka la madiplomat,  Angodiplo (Angola diplomats)
Huko ndiko tulikokuwa  tukinunua mahitaji ya vyakula na kwa upande wa nguo ,viatu na mafuta ya kupaka inabidi uagize uingereza au marekani kwa kutumia  catalogue (vitabu maalum vinavyouza vitu kwa kuagizia) unachagua unaagiza kisha wanakuletea gharama unazotakiwa ulipe ikiwemo na usafiri unatuma pesa kupitia  benki na baada ya wiki 3 wanakuletea unaaenda kuchukua airport  ambako kuna urasimu mkubwa ukizubaa mzigo wako unaweza kukaa hata miezi lakini nilijilazimisha wanijue idara zote inakopita mizigo yetu na nilijulikana fasta hivyo ikawa nikipata tu invoice ya mzigo asubuhi nasema zege halilali ntanengeneka hadi jioni narudi na mzigo.chezea Natasha wewe!
Domo mali yangu silipii vat!
Kitu kingine kilichonishangaza ni kuona wanawake wengi wanavaa nguo nyeusi kila ukitembea mtaani nikauliza kulikoni?
Nikaambiwa hao wanavaa hivyo wamefiwa na waume zao vitani.
“Mungu wangu mbona wengi!
Katika kundi la wanawake kumi,saba wote wamefiwa!
Kiingine ni kuona vijana wengi wakiwa wamekatwa ama miguu ama mikono! Kuuliza kisa eti ni  vita!
Kumbe vijana wakifika miaka 18 ni lazima waende  vitani baada ya miaka miwili anarudi ama mzima ama kilema ama harudi kabisa! Utawaonea huruma siku ya matibabu ilikuwa alhamisi maana tulikuwa tunakaa karibu na hospitali ya jeshi hivyo utayaona  makundi ya vijana kumi hadi ishirini kila baada ya muda  yanapita  na mbaya zaidi wote wamekatwa ama kiungo kimoja ama kingine!
Mdogo wangu Tony aliingizwa shule ya international school  inayoendeshwa na wafaransa (Alliance francaise) ndio ilikuwa shule pekee inayofundisha kiingereza na  haikuwa mbali na nyumbani.
Mimi nikapatiwa kazi ubalozini ya usafi ambayo niliifurahia sana, kazi ni kazi  nitake kazi ya maana nimesoma? Hiyo hiyo ambayo kwanza ilikuwa kama hisani tu toka kwa mheshimiwa Balozi ama sivyo angeuchuna tu.
Cherrie akabaki nyumbani na mama akimfanyia fujo.
Neno la kwanza la kireno kujifunza likawa embaixada nikahisi tu hata kabla sijauliza kuwa ni embassy  yaani ubalozi nikaambiwa sawa nimepatia likaja la pili ni Bondia nikataka kujibu mi sio Mohamed Ally lakini ukiwa nchi ya watu usijifanye kimbelembele kujibu vitu maana kila eneo lina namna yake ya kuzungumza mfano umetoka juani na kiu imekushika ukafika kwa muangola anaweza kukwambia akupe sumu?  lazima utakataa hakuna mtu anaependa kufa sio?  Lakini kiukweli utashangaa sana ukiona wenzako wanapewa kinywaji na wewe mate lita yanakutoka kwa kunyimwa.kumbe sumu kwa kireno ni juice!
Meza ni meza.kinyentu ni sh. Mia tano wakati huku nasikiaga masela wanasema nyentu ni mia,camarada ni comrade,  Barida kule ni bariga maana yake tumbo.huku kona ni kona kule ni neno lisiloweza kutamkika hadharani.
Shega kule maana yake inatosha, kuna maneno mengine yanafanana na kiingereza hivyo unaweza kuhisi ni neno Fulani ila hili la bondia ilibidi niwe mpole kuuliza maana yake kumbe ni Habari ya asubuhi upo hapo?
Kwa vile nilikuwa nikifanya kazi na pia kuna wafanyakazi wazawa wa pale angola kama vile dereva sumao (jina hili kwa kiingereza ni simon) baba mtumzima mwenye asili ya kongo lakini kalowea  Angola  kwa msaada wake na wafanyakazi wa ndani nilifahamu kireno haraka. Kitu cha kuchekesha wananchi wa kule sio wengi wanaofahamu kiingereza ila usiwatete kwa Kiswahili tulipoligundua hilo tukawa tunaogopa kuongea hata Kiswahili njiani maana ghafla anaibuka mtu akikusapoti unachoongea na kukwambia alikulia morogoro au Dar sasa ole wako uwe umemteta!

Kutokana na cheo cha baba yangu alikuwa akipokea vijana wageni wanaojitosa kwenye kazi ya ubaharia wakidhani kwa vile Luanda kuna bahari basi ni rahisi kupata kazi kwenye meli….


Je? Vijana hawa watafanikiwa kupata meli au  kuwin maisha?
Hayo na mengine mengi utayapata katika sehemu ya sita ya mimi na angola.

Chapisha Maoni

Please Select Embedded Mode To Show The Comment System.*

Mpya zaidi Nzee zaidi