Na Charles Mkoka
Katika ulimwengu wa filamu, mara nyingi tunaona simulizi zinazobaki kwenye skrini pekee.
Lakini kwa msanii wa filamu nchini Tanzania, Hassan Badru, anayefahamika zaidi kwa jina la utani la Mwakinyo, maisha yake halisi yameungana na sanaa kwa namna isiyo ya kawaida.
Kisa chake cha kuigiza ugonjwa wa mguu katika filamu na hatimaye kuishia kukatwa mguu halisi, kimekuwa hadithi ya kushtua, kusikitisha na yenye hisia tofauti na za kipekee, huku ikibeba mafundisho muhimu kwa jamii.
Kisa chake kilianzia katika harakati zake za upambanaji, ambapo alianzia kule nchini kenya tangu mwaka 2019
"Nilianza kuigiza muda mrefu, ila kazi yangu ya filamu nchini kenya ilinipa hamasa ya kukazana zaidi" alianza kwa husuda.
Baada ya muda kidogo kupita, ndipo Hassan Badru akaamua kurudi nchini Tanzania kuendelea na mihangaiko yake, na mwaka 2020 akapata wazo la kuandaa filamu yake iliobadilisha maisha yake yote.
| Hassan Badru 'Mwakinyo' akiwa kwenye mahojiano maalum na kituo cha redio cha BongoFM hivi karibuni. |
Chanzo cha Kisa: Filamu ya “Agano la Wachawi”
Msanii Badru 'Mwakinyo' alijipatia umaarufu kupitia filamu yake ya Agano la Wachawi, ambapo aliigiza nafasi ya mtoto wa “Mzee Msisiri”, akicheza kama kijana anayeteseka na ugonjwa wa mguu.
Katika simulizi ya filamu hiyo, waliigiza vipande pia vikionesha hatua ya kuugua mpaka mguu wa mhusika kulazimika kukatwa.
Lakini, baada ya kurejea kwenye maisha yake ya kawaida, dipo mambo yakambadilikia kikwelikweli..
![]() |
| Msanii Hassan Badru katika hatua za awali za kuugua mguu, kabla hali haijawa mbaya zaidi. (PICHA NA: Hassan Badru) |
“Sikuwahi kudhani ningeishi maisha haya. Nilipoigiza, ilikuwa kama utani. Tulimaliza kushuti na miezi miwili baadaye nikaanza kuugua mguu kikwelikweli, tena kwa maumivu makali,” anasimulia Hassan Badru
Badru anasema alianza safari yake ndefu ya matibabu bila mafanikio. Alitembelea hospitali kubwa nchini zikiwemo Muhimbili, Aga Khan, TMJ na M.O.I, lakini bado, vipimo havikuonesha tatizo lolote.
Aliendelea kutafuta msaada wa kimatibabu hadi jijini Nairobi akitafuta tiba, lakini bado juhudi hizo hazikuzaa matunda.
“Madaktari walishindwa kuelewa kitaalamu, Walisema hakuna ugonjwa, hakuna kinachoonekana. Lakini mimi nilikuwa nateseka kila siku, mguu ulivimba sana, na ukawa unatoa mausaha na damu, na maumivu makali, niliumia sana" anakumbuka kwa hisia.
Wakati akiwa nchini Kenya, aliwaomba madaktari wamkate mguu, jambo ambalo lilipingwa vikali na madaktari wataalamu kwa kutokana na kutokuwa na majibu ya kutosha.
| Msanii Hassan Badru kipindi cha kuugua kwake akiwa nyumbani. Maumivu ya Mguu wake yamedumu kwa muda wa Miaka minne kabla ya wataalamu kuchukua hatua ya kuukata Mguu wake |
Kwa miaka minne mfululizo, aliishi na maumivu makali, hadi hali ilipozidi kuwa mbaya na mguu kupasuka huku damu ikimwagika muda wote.
Nakumbuka nililazimika tena kuja jijini Dar, hadi kwenye hospitali ya Agha Khan, na uchunguzi wao mpya uliweza kuona kunanaina ya bakteria ndio wanaoleta madhara, lakini hakukuwa na namna au dawa ya kuwaondoa" aliendelea kuelezea kwa hisia
Baada ya uchunguzi huo, Hassan alipokea wito kwenda jijini mwanza kwenye hospitali mojawapo kwa ajili ya uchunguzi, ambao nao haukuzaa matunda.
"Nilipigiwa simu niende mwanza kwenye hospitali ya mkoa, lakini uchunguzi wa kina ulifanyika na bado haukuona chanzo cha tatizo hilo" aliendelea kusema
Katika safari yake yote hiyo, hospitali mbili tuu ndio zilifanikiwa kuona kuwa kuna bakteria wanaoushambulia mguu wake, na muda ukawa unaenda, huku maumivu yakizidi kumtesa.
![]() |
| Msanii Hassan Badru baada ya kukatwa mguu wake wa kulia. (PICHA na Hassan Badru) |
Hatimaye, mwaka 2024, madaktari walilazimika kuukata mguu wake ili kuokoa maisha yake.
Maisha Baada ya Upasuaji
Kukatwa kwa mguu kulibadilisha maisha ya msanii Hassan Badru Mwakinyo kwa kiwango kikubwa. Jamii ilianza kumchukulia tofauti, na changamoto za kupata nafasi za kuigiza katika filamu zikizidi.
“Mara nyingi naenda kwenye auditions, naweza kuigiza vizuri, lakini sipati nafasi kwa sababu mimi ni mlemavu. Hili linaniumiza sana, lakini sina jinsi, nimekubali hali yangu,” anasema kwa huzuni.
Anakiri kuwa kucheza filamu sasa ni changamoto, hasa kutokana na kutokuwa na uwezo wa kutumia mguu wa bandia kwa urahisi. Hata hivyo, Mwakinyo hajatetereka na ndoto zake.
"Hali hii, kukatwa kwangu kwa mguu kumeondoa hadi maeneo ya mamungio ya mguu, hivyo kushindwa kutumia miguu ya bandia ya kawaida." Alisema kwa umakini
Kuendeleza kazi zake za Sanaa
Pamoja na mabadiliko yake katika maisha aliopitia, bado msanii Hassan Badru 'Mwakinyo' hajakata tamaa. Filamu zote alizocheza tangu aanze uigizaji ni kwa gharama zake mwenyewe. Si rahisi, ila anakuwa akifanya kwa kudunduliza hivyoivyo.
"Tangu hapo mwanzo, nimekuwa nikipambana kwenye mambo yangu yote, na hata filamu zote nilizoshuti ni kwa mfuko wangu mwenyewe. Nimekuwa nikifanya kazi pembeni, kisha kipato changu naenda kuwekeza kwenye filamu zangu mwenyewe, si rshisi kupata udhamini nchini, na jamii imekuwa ikinilea hivyo" aliongezea
Hivi karibuni msanii huyo ametoa tamthilia mpya inayokwenda kwa jina la Mpangaji Wangu kwenye YouTube kwa kushirikiana na msanii mkongwe wa vichekesho, Kingwendu na wengine.
“Tamthilia hii naifanya kwa nguvu zangu mwenyewe. Sina mdhamini, nikiwa na fedha kidogo nashuti, nikikwama napumzika. Hivyo ndivyo maisha yangu yalivyo sasa,” anaeleza.
Sauti za filamu inatarajia kuandaa makala fupi kuhusiana na uchambuzi wa tamthilia hio, jinsi inavyosadifu maisha halisi ya mtanzania.
Fanya uione youtube kwa link ifuatayo, kisha usubirie uchambuzi wetu wa kina....https://youtu.be/snhuJQ292t4?si=eurwOM2RTKL_Kmub
Kwa Hassan Badru, kujitegemea ndiyo msingi wa kuendelea. Anasema anatamani wasanii nchini washirikiane zaidi ili kuimarisha sekta ya filamu bila kuacha nyuma wale wenye changamoto za kiafya au ulemavu.
Asili ya Jina la utani la ‘Mwakinyo’ na kisa chake
Wengi walidhani kuwa jina la Mwakinyo linahusiana moja kwa moja na bondia maarufu wa kimataifa nchini, Hassan Mwakinyo.
Badru anaeleza kuwa jina hilo alipewa na marafiki zake kutokana na mapenzi yake ya dhati kwa mchezo wa ngumi.
Na kwa vile anaitwa Hassan, na Mwakinyo nae pia ni wajna wake, marafiki hao wa karibu walimbatiza jina hilo
"Nilikuwa napenda sana ngumi, tangu nikiwa Nairobi, nilienda hadi kwenye majudo kadhaa, sema nilikua napenda sana mapigano ya karate na shotokan, nilianzia kwenye mkanda wa njano, ila shughuli zangu za filamu na kuhama hama zikanifanya nishindwe kujiendeleza kwenye michezo hiyo" alisema
Hata alipokuja jijini dar, aliweza kuchezacheza kidogo kabla hajaanza kuugua
“Hata wakati naugua, Mwakinyo mwenyewe alinitafuta, tukaongea na kuweka mambo sawa,” anafafanua kwa tabasamu la kumbukumbu.
Na hapo kwenye kuweka mambo sawa kuna kisa chake kingine, ambapo kuna tuhuma za utapeli zilimkutaga, kipindi akiomba michango ya matibabu.
| Msanii Hassan Badru 'Mwakinyo' akiwa katika pozi |
Alianza kwa kucheka kidogo, kisha akaendelea, "wakati naugua, baadhi ya watu wangu wa karibu walikuwa wanapost mitandaoni kuomba misaada, wakawa wanatumia sana jina la mwakinyo, hii iliniletea shida pale mwakinyo mwenyewe alipoona"
Hali hio ilizua mtafaruku, kwani Hassan Mwakinyo hakuwa anafahamiana na wajna wake Badru, na hata alipopata confirmation kutoka kwenye mamlaka husika za wasanii, alielewa, wakazungumza na kuyaweka sawa, na kisha kumsapoti
Binafsi ninafurahi nikiona wasanii tunapendana na kuelewana ni kitu kizuri kwa kweli, na nawashukuru wote walioonesha nia ya kunisaidia katika kipindi kile kigumu" aliongezea
| Msanii Hassan Badru 'Mwakinyo' akionesha sampuli ya viatu alivyovitengeneza kwa mikono yake yeye mwenyewe kwenye ofisi ya kutengenezea viatu. amekuwa akiishi na taaluma hio kwa miongo kadhaa |
Msimamo wa Maisha na Ndoto Zisizokufa
Licha ya maumivu na changamoto, Hassan Badru anaamini kuwa ulemavu siyo mwisho wa ndoto. Anaona sanaa kama njia ya kuelimisha jamii na kujenga mustakabali bora kwa wengine.
“Ninatamani jamii itambue kuwa walemavu wana nafasi muhimu. Maisha hubadilika ghafla, lakini changamoto haziwezi kuua ndoto. Kila mtu ana jukumu la kufanya kazi na kuendeleza taifa letu,” anasisitiza.
Kwa Hassan Badru, sanaa si kazi tu, bali ni wito na upendo kwa nchi yake. Anaamini kuwa ataendelea kupambana hadi mwisho ili kufanikisha malengo yake, licha ya kukatwa mguu na vizingiti anavyokutana navyo kila siku.
Safari ya msanii Hassan Badru ni simulizi ya kipekee inayounganisha maisha halisi na uigizaji. Ni hadithi ya maumivu, matumaini na uthubutu.
Kupitia changamoto zake, anawaonesha wasanii na jamii kwa ujumla kuwa ndoto zinaweza kuendelea hata pale ambapo maisha yamepoteza mwelekeo.


