Mfahamu @Streetjournalisti: Kijana anayeigeuza Redio kuwa burudani ya filamu mitandaoni

Na Charles Mkoka

Katika anga la burudani na filamu nchini Tanzania, jina moja limeanza kutikisa mitandaoni kwa kasi kwelikweli hasa kwa watengeneza maudhui.

Huenda usimtambue kwa jina lake halisi, la Adili Constantino, lakini kama ni mtumiaji wa mitandao ya kijamii, lazima utamfahamu kwa jina la @streetjournalisti,

Wengine wamekuwa wakitumiana clips au skits zake mitandaoni huku wakicheka na kufurahia vituko vyake huku wakiridhika na utangazaji wake adhimu.

Yeye binafsi anachukulia jukwaa lake hilo kama sehemu ya kufurahi na kujiachia,

Ninakuandalia makala hii adhimu ili uweze kumjua kijana huyu, mwenye asili ya nyanda za juu kusini na kusomea uandishi wa habari, hadi kufikia kubuni jukwaa lake linalopendwa na wengi.

Adili Constantino, kijana aliyeanzisha chapa ya kidijitali ya @Streetjournalisti, huku  akichanganya ucheshi, ubunifu na sauti ya utangazaji wa redio kwenye video fupi zinazosambaa kila siku.

Akiwa mtulivu na mwenye busara, Adili anaeleza kwamba mapenzi yake kwa redio yalianza tangu enzi zake za utotoni. 

Makuzi yake katika familia ya mwalimu aliyekuwa akiiwasha redio muda mwingi, na tangu hapo, kikawa kitu pekee kwenye shauku ya mtoto wake, ya kutaka kujua kinachoendelea nyuma ya kipaza sauti.

“Tangu nikiwa mdogo nilipenda redio. Kijijini kwetu tulikuwa tunasikiliza redio sana. Nilijiuliza sana, hivi studio za redio zikoje?” anasema huku akitabasamu.

Akiwa mhitimu wa Masomo ya Uandishi wa habari na uhusiano wa umma, kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) mwaka 2024, Adili tayari alishajizolea umaarufu mitandaoni kwa kuwa na wafuasi zaidi ya 60k (followers), ndani ya mwaka wake wa pili wa masomo.

Watu wamekuwa wakivutiwa na ucheshi wake huku akitangaza kwa ufanisi unaojaa utani, na kuwa burudani kwa wapenzi wote wa redio, uandishi wa habari na hata manguli ndani na nje ya nchi.

"@Streetjournalist ni harakati. Ni chapa (brand) iliyoanza muda mrefu, na zile video za mwanzo ziliweka dira ya ndoto yangu.”

Leo, harakati hiyo imekua maradufu. Mchanganyiko wake wa ucheshi wa kibunifu, maigizo ya studio za redio, na sauti ya utangazaji uliopangiliwa umemfanya kuvutia mamia ya maelfu ya wafuasi kila wiki, tena kwa kasi inayoongezeka kila siku.

"Kila ninachopost kwenye hio akaunti ninakimiliki, ni mali yangu, nakifanya mwenyewe, nazalisha na kisha kupost mtandaoni” anasema. “muda mwingi naomba usaidizi kwenye kushuti, lakini script na mawazo ya msingi kwenye kutengeneza maudhui hayo ni yangu.”

Video zake zinachungulia ‘nyuma ya redio’, zikionyesha namna ya kufurahisha, kuelimisha na kuhamasisha bila kupoteza ubora wa kiuanahabari. 

Ndicho kilichomfanya awe kipenzi cha mashabiki wa burudani, filamu za mtandaoni (skits), na vijana wa Gen Z.

Adili anathibitisha kuwa sasa anapokea simu kutoka kwa wanahabari wakubwa ndani na nje ya Tanzania, jambo ambali hataaa hakuliwazia sana.

Kuhusu swali la kama anaweza kuwa mchekeshaji zaidi ya mwandishi wa habari:

“Naweza kufanya vyote viwili, lakini siwezi kuacha uandishi. Sanaa inanivutia, ndiyo, lakini uandishi ni msingi wangu.”

Na Jee, kuhusu ucheshi ulipoanzia? Jibu lake, hauwezi amini. Siku zote tunda halidondoki mbali na mtini, yote haya yamechagizwa na baba.

(Anacheka.)

“ucheshi umeanzia kwa Baba, yeye ni mtu wa kupenda wengine wafurahi, yes ni mwalimu, anafundisha, lakini pia ni mtu wa burudani na heshima. Anaweza kuandaa mambo (events) hasa kukiwa na sherehe au mahafali, na atahakikisha burudani ya vichekesho au maigizo yanakuwa, na lazima kuna mtu anakonga nyoyo za watu wote kwa vicheko. Nahisi mambo hayo yameanzi hukooo, tangu utotoni.”

Kwa sasa, @Streetjournalisti sio tu akaunti ya mitandaoni; ni jukwaa la burudani linaloangaliwa kama moja ya mtengeneza maudhui ya mtandaoni wa kiswahili zinazoongoza kwenye vichekesho, ubunifu na vipande vya uhalisia wa studio kwa mtazamo wa filamu.

Hivi karibuni, mafanikio yake yamechukua mtandao kwa kasi, huku majukwaa makubwa yakimsifu kwa namna anavyochanganya ucheshi na uandishi kwa ubunifu wa kipekee akibadilisha kabisa mtindo wa “maudhui ya kuchekesha redioni” nchini Tanzania.


Chapisha Maoni

Please Select Embedded Mode To Show The Comment System.*

Mpya zaidi Nzee zaidi