Na Mwandishi wetu
Shirika la Kutetea Uhai (Prolife Tanzania) limewatoa rai kwa Wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA) kuukataa Muswada wa Ujinsia na Afya ya Uzazi wa Afrika Mashariki wa Mwaka 2024, kwani unahatarisha maadili na mfumo wa maisha ya jamii za Kiafrika.
Akizungumza na vyombo vya habari jiji Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Prolife Tanzania, Emil Hagamu, amesema msukumo wa Muswada wa EAC SRH Bill 2024 ni sehemu ya ajenda pana ya kuendeleza kile alichokiita “Utamaduni wa Kifo,” akieleza kuwa umeathiriwa na ushawishi kutoka mataifa ya Magharibi yanayotaka kubadili mtazamo wa jamii kuhusu thamani ya uhai.
Hagamu ambaye pia ni Mkurugenzi wa Shirika la kimataifa la kutetea Uhai Kanda ya Afrika kwa Nchi Zinazozungumza Kingereza, Human Life International (HLI), amesema mswada huo unapendekeza mabadiliko makubwa kwenye jamii, ikiwa ni pamoja na kuhamasisha matumizi makubwa ya vidhibiti mimba, kujaribu kuhalalisha utoaji mimba katika nchi wanachama wa EAC, kufundishwa kwa elimu ya ujinsia na afya ya uzazi katika shule zote, pamoja na kuruhusu umama wa mbadala (surrogacy) — vipengele ambavyo amesema vinapingana na mfumo wa maadili ya Kiafrika
Amesema tangu enzi, jamii za Kiafrika zimekuwa zikiongozwa na miiko, Mila, Desturi, makatazo na maadili yaliyoweka mipaka ya utendaji na kulinda hadhi ya maisha ya kila mtu kulingana na umri na jinsia. Aidha, amesema kwamba watu wamekuwa wakiishi kulingana na Imani zao kwa Mungu, inayotoa matumaini ya maisha ya baadaye na kuendeleza uhusiano kati ya walio hai na waliotangulia, hivyo mswada huo unakinzana na misingi hiyo ya kitamaduni na kiroho.
Kutokana na hayo, Shirika hilo limewasihi Wabunge wa EALA nchini Tanzania kuukataa Muswada huo, kwani unapoteza mwelekeo wa kulinda uhai na utu wa binadamu.
Shirika hilo pia limehoji uwazi wa mchakato wa muswada huo, kwani umekuwa wa kificho na kutowekwa wazi kwa Wananchi kushiriki jambo linaloashiria nia ovu iliyoko ndani yake.
Hivi karibuni Viongozi HLI Kanda ya Afrika
Mashariki kutoka Uganda, Rwanda, Burundi na Tanzania walikutana jijini Arusha na kujadili muswada, na kutoa maazimio ya kwanini Muswada huo ni hatari kwa watu wa EAC, ambapo kila Kiongozi atawasilisha kwa Wabunge wa EALA.
