Mfahamu Dkt. Nyange: Mwamba wa filamu za Matukio, Daktari anayeishi sanaa kwa uhalisia

Na Mwandishi wetu

Kwa yeyote aliyewahi kuzifuatilia na kuzipenda tamthilia za zamani za ITV na TVT (ambayo baadae ni TBC) ikiwemo Chozi, Hatia, Gumbizi na nyinginezo, jina la Dkt. Pius Nyange si geni masikioni. 

Ni mmoja wa wasanii waliodumu katika tasnia ya filamu na tamthilia za kuigiza kwa miongo kadhaa, bila kelele nyingi, lakini kwa ubora unaojizungumza wenyewe.

Sauti ya Filamu ilifanya mahojiano mafupi na msanii huyu mahiri, ambaye kwa muda mrefu amejijengea jina katika filamu zenye maudhui ya matukio na uhalifu (crime genre)

Ni msanii ambaye ukimuona unaweza kuhisi kama unamfahamu, hata kama humjui kwa karibu kwani taswira yake imekua sambamba na historia ya filamu za Kitanzania.

Cha kuvutia zaidi ni kwamba, licha ya umaarufu wake wa hapa na pale, Dkt. Pius Nyange ana maisha mengine nje ya sanaa, ambayo ni ya kawaida sanaa. Anamiliki vifaa vyake binafsi vya utayarishaji wa filamu, ikiwemo kamera za kisasa na hadi drone, huku akiendelea na shughuli zake za kila siku kama mtaalamu wa afya.

 “Mimi ni daktari. Nimesomea na kubobea katika tiba za mimea asilia. Hii ni tiba bora na nafuu kwa sababu inatoa ufumbuzi wa magonjwa ambayo hata hospitali wakati mwingine hayana tiba,” anaeleza kwa utulivu na umakini.

Kwa mujibu wake, anadhani kuwa kwa msanii kujishughulisha na kazi mbalimbali ni sehemu ya maisha, haijalishi una umaarufu kiasi gani.

 “Nilianza kuigiza tangu enzi za TVT (sasa TBC) na ITV. Nimeigiza katika tamthilia nyingi kama Chozi, Hatia, Gumbizi na nyinginezo,” anakumbuka.

Dkt. Nyange ni mfano wa msanii aliyedumu bila kuchoka. Ameweza kuvuka vizazi kadhaa vya wasanii, huku akizidi kuiva taratibu kama divai bora.

“Nimeigiza na wasanii kama Munah Love na wengine wengi, kabla hata hajaanza kusumbua jiji kwenye mitandao ya kijamii, kabla ya kizazi cha akina Kanumba kuanza mabalaa yake. Uigizaji wa kabla ya kipindi hicho umenifanya niipende sanaa kila siku,” anasema kwa mbwembwe.

Kwa uzoefu huo mpana, ndio uliomvuta taratiibu na kumtumbukiza kwenye kuipenda na kuwa mahiri  katika filamu za matukio (crime).

“Nimeandika na kuigiza filamu na tamthilia kadhaa, nyingi zikiwa na maudhui ya matukio ya uhalifu. Naweza kusema nimebobea zaidi kwenye genre hiyo, ingawa nafanya na nyingine pia,” anaeleza.

Anabainisha kuwa kati ya filamu zake tisa, nyingi zimejikita katika crime genre, licha ya ukweli kwamba soko mara nyingi hupendelea mapenzi, comedy, na burudani flani hivii nyepesinyepesi.

Kwa Dkt. Nyange, filamu za matukio zina nafasi kubwa zaidi ya kubeba ujumbe mzito kwa jamii.

“Kupitia maudhui haya, naweza kufundisha, kuburudisha, kuonya na hata kuhamasisha kampeni mbalimbali. Kuigiza upolisi na wahalifu kumeifanya nikutane na maafisa usalama, wengine wakinipongeza, wengine wakinihoji kwa mashaka, na wengine hata kunitisha. Kuna nyakati niliogopa, lakini wapo pia waliokuwa wakinipa moyo, wadogo kwa wakubwa” anaongeza.

Akiulizwa kwa nini filamu za matukio (crime) huonekana chache na wakati mwingine kudhaniwa kuwa ‘zinaboa’, Dkt. Nyange anakataa hoja hiyo.

“Sio kwamba zinaboa. Tatizo ni waandaaji wengi hawalinganishi kazi zao na uhalisia wa jamii. Ukiziangalia filamu zangu, utaona mambo halisi ya maisha ya kila siku, migogoro ya kifamilia, siri, uhalifu, rushwa, matumizi mabaya ya madaraka na mengine mengi. Jamii inapaswa kujifunza kila kitu kupitia sanaa,” anasisitiza.

Filamu yake ya Saa Mbovu, anaeleza kuwa kazi hiyo ilimlazimu kuchambua dhana ya mapenzi kwa uhalisia mkubwa zaidi, si kwa maneno tu bali kwa taswira inayoeleweka na wote.

“Si rahisi. Ndio maana nachukua muda kuandaa kazi zangu. Nikitoa filamu, nataka iishi muda mrefu, hata kwa watoto wangu na vizazi vijavyo. Mimi nikishakuwa msanii, sifanyi kwa ajili ya kujifurahisha tu, bali kwa ajili ya jamii,” anasema kwa msisitizo.

Swali: Je, haogopi kuwa maudhui yake yanaweza kukera wahusika halisi wa matukio yanayoigizwa?

“Msanii ana wajibu wa kufanya kazi bora. Kuna namna ya kuwasilisha ujumbe bila kumnyooshea mtu kidole. Tunapaswa kuonesha kuwa mambo haya yapo ili jamii ichukue tahadhari, nashangaa wasanii wengine wanaooonesha vitu vya hovyohovyo katika jamii ambavyo havina maana, ili kuwa maarufu” anakazia.

Kwa ujumla, Dkt. Nyange ni mfano wa msanii anayechanganya taaluma, uzoefu na dhamira ya kweli ya kuielimisha jamii kupitia filamu. Ni mwamba wa tasnia, anayethibitisha kuwa sanaa bora huishi muda mrefu kuliko umaarufu wa muda mfupi.


Itaendelea…

Chapisha Maoni

Please Select Embedded Mode To Show The Comment System.*

Mpya zaidi Nzee zaidi