TDFAA yazindua rasmi Iringa Film Awards, yapongeza wadau kujitokeza kwa wingi

Na Mwandishi wetu, Iringa

Chama cha Waigizaji Filamu Nchini Tanzania (TDFAA), Mkoa wa Iringa kimezindua rasmi tuzo za filamu za mkoani humo (Iringa Film Awards), huku kikiyapongeza makundi mbalimbali ya wadau kwa kujitokeza kwa wingi na kuendelea kuiunga mkono tasnia ya filamu mkoani humo.

Akitoa pongezi hizo, Mwenyekiti wa TDFAA Iringa, Bw. Khamis Nurdin, alisema lengo kuu la tuzo hizo ni kuinua sanaa katika mkoa huo na kuonyesha mchango wa wasanii katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

“Tulivyoanza tulipokea filamu 27 pekee, mwaka jana ziliongezeka hadi 67. Naam, ninaamini mwaka huu tutafika filamu 100 au zaidi,” alisema Bw. Nurdin.

Aliongeza kuwa mkoa wa Iringa umeendelea kukua kisanaa mwaka hadi mwaka, jambo linalotoa matumaini makubwa kwa mustakabali wa tasnia hiyo.

“Tunawashukuru sana wadau kwa sapoti yenu. Tunatamani kukua zaidi hadi kufikia nyanda za juu kusini kwa kushirikisha mikoa mitano au zaidi,” alisisitiza.

Kwa mwaka huu, chama hicho kimepokea udhamini kutoka kwa wadau mbalimbali ndani na nje ya mkoa huo, huku kikiwahamasisha wengine kuendelea kuunga mkono jitihada hizo.

“Nia yetu ni kukua zaidi na zaidi. Tunafurahia kuwa sehemu ya kuwafanikisha wasanii na waandaaji filamu. Mungu akijaalia, tuzo hizi zifike hata kwenye hadhi ya kuwa jukwaa la kimataifa,” aliongeza Mwenyekiti huyo.

Kwa upande wa wadhamini, hoteli ya Lumilo Classic Hotels imeendelea kudhamini tuzo hizo tangu zilipoanzishwa. Meneja wa hoteli hiyo, kupitia Afisa Masoko, Bi. Yasmine Daniel, alisema udhamini huo ni njia ya kurudisha kwa jamii moja kwa moja.

“Kwetu sisi tunachukulia fursa hii ya kuwa wadhamini wakongwe kama sehemu ya kusaidia jamii. Tunaunga mkono juhudi za maendeleo ya vijana wetu na sekta ya filamu kwa ujumla,” alisema.

Lumilo Classic Hotels imekuwa ikiunga mkono wasanii wazawa, ikiwemo kutoa nafasi za locations kwa ajili ya uzalishaji wa filamu na zawadi kwa washindi wa tuzo kwa njia ya hundi.

Tuzo za mwaka huu, ambazo awali zilipangwa kufanyika Septemba, sasa zimesogezwa mbele hadi Disemba mwaka huu ili kupisha shughuli za uchaguzi mkuu unaoendelea nchini.

1 Maoni

Please Select Embedded Mode To Show The Comment System.*

Mpya zaidi Nzee zaidi