TDFAA Iringa yazindua rasmi Iringa Film Awards, tuzo kusogezwa mbele kupisha Uchaguzi

Na Mwandishi Wetu

Iringa – Chama cha Waigizaji Filamu Nchini Tanzania, Mkoa wa Iringa (TDFAA) kimezindua rasmi msimu wa tatu wa Iringa Film Awards huku kikitangaza kusogeza mbele tuzo hizo hadi mwezi Desemba mwaka huu, ili kupisha shughuli za uchaguzi mkuu.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Katibu Mkuu wa TDFAA, Ndugu Hassan Rafiq, alisema uamuzi huo unalenga kutoa nafasi kwa wadau wote kushiriki kikamilifu na kuimarisha mchango wa tasnia ya filamu katika mkoa huo.

“Tumezindua rasmi msimu huu wa tatu, tumepiga hatua kubwa tangu tulipoanza misimu miwili iliyopita kwa juhudi na imani. Leo tunashukuru kuona ukuaji unaoendelea katika tasnia yetu,” alisema Bw. Rafiq

Aliongeza kuwa chama kinatambua mchango wa waandishi wa habari na wadau wengine wanaounga mkono maendeleo ya filamu mkoani humo.

“Filamu zetu zimekuwa sehemu muhimu ya jamii katika kuelimisha na kuburudisha. Tuzo hizi ni jukwaa la kuwatambua na kuthamini wote wanaoleta uhai katika kazi za filamu. Kazi yenu inaonekana na mna thamani kubwa,” alisisitiza.

Katibu Mkuu huyo pia aliwakumbusha wasanii na wadau kwamba sanaa ni ajira, elimu na sauti ya jamii, akibainisha kuwa TDFAA itaendelea kuwa mstari wa mbele katika kuwawezesha na kuwatambua watengenezaji filamu.

Kwa upande wa wadhamini, chama kimeendelea kuomba ushirikiano wa wadau mbalimbali ili kufanikisha msimu huu wa tuzo. 

Aidha, katibu huyo aliwataka wasanii wote kujiunga na chama hicho kwa mustakabali mwema wa tasnia ya filamu nchini.

Mwaka jana, tuzo hizo zilipokea jumla ya filamu 67 kutoka wilaya mbalimbali, ambapo Wilaya ya Mufindi iliongoza kwa ushiriki na ushindani mkubwa. 

Kwa msimu huu, TDFAA Iringa imetangaza kuwa filamu zitakazowasilishwa mitandaoni, ikiwemo YouTube, zitakubalika kwa ushindani rasmi.

Kaulimbiu ya tuzo za mwaka huu ni:
“Uwekezaji katika sanaa ni kukuza utalii: wasanii tupo tayari kushiriki uchaguzi mkuu Oktoba, TDFAA tunaibeba sanaa.”

Chapisha Maoni

Please Select Embedded Mode To Show The Comment System.*

Mpya zaidi Nzee zaidi