Na Mwandishi wetu
Tamasha la Kimataifa la Filamu la Zanzibar Zanzibar International Film Festival (ZIFF) limetangaza rasmi filamu zilizochaguliwa kwa toleo lake la 29 litakalofanyika Zanzibar kuanzia Juni 24 hadi 28, 2026, huku kaulimbiu ya mwaka huu ikiwa ni “Akili Unde (AI) na Sanaa ya Usimuliaji wa Hadithi.”
Kupitia taarifa rasmi kwa vyombo vya habari iliyotolewa Mei 20, waandaaji wa ZIFF wamesema kaulimbiu hiyo inalenga kuchunguza namna teknolojia ya AI inavyoweza kubadili simulizi za Kiafrika pamoja na changamoto zinazoambatana na matumizi yake ndani ya bara la Afrika.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Afrika bado inakabiliwa na changamoto mbalimbali katika matumizi ya AI ikiwemo uhaba wa miundombinu, upatikanaji mdogo wa data za ndani pamoja na ukosefu wa wataalamu wenye ujuzi wa teknolojia hiyo kwenye sekta ya filamu.
Mwaka huu, ZIFF imepokea zaidi ya filamu 400 kutoka zaidi ya nchi 100 duniani, huku Afrika Mashariki ikichangia filamu 129. Tanzania imewasilisha filamu 45, Uganda 50 na Kenya 23.
Filamu zilizochaguliwa kwa mashindano ya mwaka huu zinajumuisha filamu 14 ndefu, makala 13, tamthilia 10 za televisheni, filamu fupi 22 pamoja na filamu sita za animation, jumla ikiwa filamu 65.
Mbali na maonesho ya filamu, tamasha hilo pia litakuwa na warsha mbalimbali zinazolenga kuwajengea uwezo watengenezaji wa filamu katika maeneo ya matumizi ya AI, elimu ya fedha, usambazaji wa maudhui pamoja na uundaji wa maudhui ya kidijitali.
Miongoni mwa wawezeshaji watakaoshiriki ni pamoja na Lisa Russell ambaye ni mshindi wa tuzo ya Regional Emmy na Balozi wa Women in AI nchini Kenya.
ZIFF pia imetaja filamu ya makala We Are Hadza kama moja ya vivutio vikubwa vya mwaka huu, ambapo wanajamii wa Kihadza pamoja na timu ya uzalishaji wa filamu hiyo wanatarajiwa kushiriki tamasha hilo Zanzibar.
Katika upande wa udhamini, waandaaji wamekiri kuwa bado kuna changamoto ya kifedha katika kuendesha tamasha hilo, ingawa mwaka huu wamepokea msaada kutoka Umoja wa Ulaya (EU), AZAM MEDIA LTD pamoja na Air Tanzania.
Tamasha la Zanzibar International Film Festival limekuwa likifanyika tangu mwaka 1997 na linaendelea kubaki moja ya majukwaa makubwa zaidi ya filamu Afrika Mashariki, likiwaunganisha watengenezaji wa filamu, wasanii pamoja na watazamaji kutoka sehemu mbalimbali duniani.