Baada ya kushiriki mafunzo maalum ya matumizi ya filamu katika kutangaza utalii yaliyofanyika nchini China, Rais wa Shirikisho la Filamu Tanzania (TAFF), Rajabu Amir amesema Tanzania ina kila sababu ya kutumia nguvu ya filamu kuitangaza dunia kuhusu utamaduni wake, lugha ya Kiswahili na vivutio vya utalii.
Akizungumza akiwa nchini humo, Rajabu amesema mafunzo hayo yamefungua uelewa mpya kuhusu namna mataifa makubwa kama China yalivyofanikiwa kutumia filamu, makala na maudhui ya kimkakati kuvutia mamilioni ya watalii kila mwaka na kukuza uchumi wa ubunifu.
“Tumekuwa tukijifunza namna culture, tourism na film zinavyounganishwa. China wamewekeza sana kwenye filamu za kimkakati na dokumentari zinazovutia watu duniani kote kutembelea maeneo yao,” amesema.
Kwa mujibu wa Rajabu, uzoefu alioupata nchini China umeonyesha wazi kuwa tasnia ya filamu inaweza kuwa nyenzo kubwa ya kiuchumi ikiwa itawekewa mkazo katika ubora wa maudhui pamoja na ushirikiano wa kimataifa.
Amesema moja ya mambo yaliyowavutia zaidi ni namna China ilivyofanikiwa kutumia filamu kuitangaza historia, mila na mandhari zake za kipekee hadi kuwa kivutio kikubwa cha utalii duniani.
“Tumeshuhudia namna walivyoweza kutumia filamu kuongeza idadi ya watalii na mapato ya taifa. Hii ni somo kubwa kwetu Tanzania,” ameongeza.
Rais huyo wa TAFF amewataka watayarishaji wa filamu nchini kuanza kufikiria zaidi utengenezaji wa filamu na dokumentari zinazotangaza Tanzania kimataifa, badala ya kuangalia burudani pekee.
Amesisitiza kuwa Tanzania ina hazina kubwa ya simulizi, tamaduni na maeneo ya kuvutia ambayo yanaweza kuuzwa kupitia filamu zenye ubora wa kimataifa.
“Tunapaswa kutengeneza filamu zenye quality na content zinazoweza kwenda worldwide. Dunia inahitaji kuona utamaduni wetu, Kiswahili chetu na uzuri wa Tanzania kupitia kazi zetu,” amesema.
Pia amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya watayarishaji wa ndani na mataifa yaliyoendelea kiteknolojia kupitia miradi ya co-production, jambo ambalo linaweza kusaidia kuongeza maarifa, teknolojia na soko la kimataifa kwa filamu za Tanzania.
Katika hatua nyingine, Rajabu ameishukuru Serikali ya Tanzania chini ya uongozi wa Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kufungua fursa za mafunzo na safari za kimasomo kwa wasanii na wadau wa sekta ya filamu.
Pia amemtaja Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Paul Makonda pamoja na Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu nchini, Dkt. Gervas Kasiga kwa mchango wao katika kuhakikisha wasanii wanapata nafasi za kujifunza na kujitanua kimataifa.
Akihitimisha ujumbe wake, Rajabu ametoa wito kwa wadau wote wa filamu nchini kufanya kazi kwa bidii, weledi na mshikamano ili kuitumia vizuri fursa ya exposure wanayoipata kwa manufaa ya tasnia na taifa kwa ujumla.
