 |
| Mchezaji Bora Afrika (ligi za ndani) Mbwana Samatta |
Na Mwandishi Wetu, Mkuranga
MTANDAO
wa Wasanii Tanzania (SHIWATA) umeamua kumpa uanachama wa heshima
mchezaji bora wa Afrika, Mbwana Samatta pamoja na kumzawadia ekari tano
za ardhi katika kijiji cha Wasanii Mwanzega, Mkuranga kwa ajili ya
kuanzisha Chuo cha Mafunzo ya soka.
Mwenyekiti wa SHIWATA,
Cassim Taalib alisema jana kuwa kikao cha Kamati Utendaji ya Mtandao huo
kilichoketi juzi kilifikia uamuzi huo baada ya kufuatilia kwa karibu
mafanikio ya Samatta akiwa na Timu ya Taifa ya Tanzania 'Taifa Stars',
TP Mazembe ya Jamhuri ya Kongo na kufanya vizuri katika mashindano ya
Afrika hadi kuchaguliwa kuwa mchezaji bora Afrika.
Alisema
SHIWATA inatoa kiwanja hicho kama zawadi kwa mchezaji huyo kutokana na
uwezo wake wa kulitangaza taifa katika medani ya kimataifa katika mchezo
wa soka ambako wengine watafuata nyayo zake..
Taalib
alisema taratibu za makabidhiano zinafanywa kwa mawasiliano na baba yake
mzazi, Ali Samatta na atakabidhiwa eneo hilo mara baada ya kurudi
kutoka Ubelgiji ambako anakwenda kusaini mkataba na timu ya KRC Genk ya
Ligi Kuu ya Ubelgiji wa miaka minne.
 |
|
SHIWATA yenye
wanachama zaidi ya 8,000 inamiliki ekari 300 za kujenga makazi,kumbi za
starehe, viwanja vya michezo na nyumba za kuishi katika kijiji cha
Mwanzega wilayani Mkuranga na ekari 500 eneo la Ngarambe kwa ajili ya
kilimo.
Wakati huo huo
Wasanii
wanne maarufu nchini wakiongozwa na Ahmed Olotu 'Chilo' juzi walinogesha
tamasha la sanaa na michezo wilayani Mkuranga walipoalikwa kuona sanaa
inavyochezwa na wasanii wa wilaya hiyo.
Mzee Chilo
aliyefuatana na Boniface Mwanza Mpango 'King Kikii', Wasanii wa Bongo
Movie, Suzan Lewis 'Natasha, Kulwa Kikumba 'Dude' na Asha Salvador
walijikuta wakishangiliwa kila mara kwa mara na wasanii wenyeji ambao
pia walipiga nao picha.
CHANZO: SHIWATA
Tags: Mbwana SAMATA, SHIWATA, Taifa Stars, TP Mazembe, Mkuranga