Na Mwandishi Wetu
Mtengeneza filamu Maarufu
nchini India (Bollywood) S.S. Rajamouli, anatarajiwa kuanza ratiba mpya ya kushuti
filamu yake inayosubiriwa kwa hamu kubwa ya SSMB
29, yenye mastaa wa kimataifa Mahesh Babu na Priyanka Chopra.
Kwa mujibu wa taarifa
mbalimbali, kikosi kazi kitatia kambi na kuanza kurekodi filamu hiyo ndani ya
Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Tanzania, kuanzia mwishoni mwa mwezi Julai, mwaka
huu kwa bajeti ya kufikia TZS bilioni 306.
Filamu hiyo pia
inamshirikisha muigizaji maarufu kutoka Malayalam, Prithviraj Sukumaran, na
inaelezwa kuwa ni mchanganyiko wa vituko, historia ya kale na mafumbo ya
kiutamaduni, ikivutia simulizi za zamani za asili ya kiafrika.
Gazeti la burudani la India Eastern Eye limeripoti kuwa gumzo kuhusu
filamu hiyo ya SSMB 29 limeongezeka
zaidi baada ya gazeti la Tanzania la The
Citizen kuthibitisha uwepo wa ‘shooting’ ya filamu hiyo huko Serengeti
Kwa mujibu wa vyanzo vya
karibu, filamu hiyo inahusu mtafiti jasiri anayeanza safari hatarishi kupitia
maeneo ambayo hayajachunguzwa barani Afrika.
Filamu hiyo, iliyopata
msukumo kutoka kwa filamu maarufu kama *Indiana Jones*, inamuonesha mhusika
mkuu akikabiliana na mazingira hatari, masimulizi ya kale ya wenyeji na adui
mwenye nguvu, huku akifukua siri iliyosahaulika ambayo inaweza kubadili hatima
ya dunia.
Mahesh Babu anatarajiwa
kuigiza mhusika mkuu kwenye filamu hiyo, jukumu ambalo linadhaniwa kuwa gumu
zaidi kwake ukilinganishwa na kazi zake mbalimbali alizofanyaga.
Priyanka Chopra, ambaye
amerudi kwenye tasnia ya filamu za India baada ya kupambana Holywood kwa muda
mrefu, atakuwa na nafasi muhimu katika filamu hiyo.
Licha ya Serengeti kuwa eneo
kuu la upigaji wa awamu hii ya filamu, timu hiyo inatarajiwa kuhamia Afrika
Kusini kwa picha za ziada.
Ripoti za awali pia
zilieleza kwamba filamu hiyo itakuwa na kiini cha kihistoria na kiutamaduni
kinachotokana na masimulizi ya India, hivyo kuiweka filamu hiyo katika daraja
la kipekee kati ya tamaduni za Afrika na Asia.
kushutiwa kwa *SSMB 29*
nchini Tanzania si tu tukio kubwa la kimataifa kwenye tasnia ya Filamu, bali
pia ni fursa ya kuitangaza nchi kama kitovu cha kuvutia kwa waandaaji wa filamu
duniani.
Kwa kuhusisha jina kubwa
kama Rajamouli na waigizaji wa hadhi ya kimataifa, wadau wa sekta ya filamu
wanatabiri kuwa SSMB 29 huenda ikawa
miongoni mwa kazi kubwa zaidi za sinema ya India kuwahi kutokea.
