Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam – Julai 2025 Msimu mpya wa Tamasha na Tuzo za Filamu Tanzania (TaFFA 2025) umeanza kwa kishindo huku Bodi ya Filamu Tanzania ikifungua rasmi milango kwa ajili ya uwasilishaji wa kazi za filamu zitakazoshiriki katika mashindano ya tuzo za mwaka huu.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa msimu huu, Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu, Dkt. Gervas Kasiga, amesema kuwa tofauti na misimu iliyopita, mwaka huu TaFFA inakuja na maboresho makubwa, yakiwemo mafunzo maalum ya kitaaluma kwa watayarishaji wa filamu kutoka kona zote za nchi.
“Huu ni msimu wa nne wa TaFFA, na mwaka huu tumefanya maboresho makubwa. Kwa mara ya kwanza tamasha linakwenda sambamba na fursa za mafunzo, yanayogusa kila hatua ya uandaaji wa filamu – kutoka uandishi wa hadithi, upigaji picha, uhariri, hadi usambazaji wa kazi hizo,” alisema Dkt. Kasiga.
Wanatasnia ya filamu nchini wamehimizwa kuwasilisha kazi zao kwa ajili ya kushindania tuzo au kwa maonyesho yasiyo ya mashindano ndani ya tamasha hilo.
Uwasilishaji wa kazi unaweza kufanyika kupitia tovuti rasmi ya Tamasha au kwa kuziwasilisha moja kwa moja katika ofisi za Bodi ya Filamu Tanzania, ambapo washiriki watapokelewa na kupewa maelekezo yote muhimu.
Tamasha la mwaka huu limepokelewa kwa hamasa kubwa na wadau wa filamu nchini, wakiliona kama jukwaa muhimu la kufufua ari ya filamu za Kitanzania na kutoa dira mpya kwa kizazi kipya cha waongozaji, waigizaji na watayarishaji.
Mbali na maonyesho ya filamu na utoaji wa tuzo, TaFFA 2025 itajumuisha mafunzo ya kina katika maeneo muhimu ya fani ya filamu, yakiwemo:
-
Uandishi wa hadithi na uongozaji wa filamu,
-
Utayarishaji na uhariri wa kazi za filamu,
-
Mbinu za kupata fedha na kusimamia miradi ya filamu,
-
Masoko ya ndani na ya kimataifa kwa kazi za filamu za Kitanzania.
Kwa taarifa zaidi kuhusu ushiriki na uwasilishaji wa kazi, tafadhali tembelea:
🌐 www.taffafestival.or.tz