Nancy: Sekta ya Vitabu Afrika Ni Injini ya Filamu, Utamaduni na Uchumi wa Ubunifu


Na Mwandishi wetu

Dar es Salaam – Katika Kongamano la Tanzania Film, Festival and Awards (TAFFA) 2025, mwandishi na mwanaharakati wa ubunifu, Nancy, ametoa wito wa kuwekeza zaidi katika sekta ya vitabu barani Afrika, akieleza jinsi tasnia hii inavyokuwa chanzo kikuu cha hadithi zinazochochea maendeleo ya filamu, michezo ya jukwaani na kazi nyingine za ubunifu.

Akiakisi maudhui ya ripoti ya UNESCO The African Book Industry: Evidence and Dialogue, Nancy alisimulia safari yake ya uandishi, akimtaja Mama Ellie Shirema kama chanzo cha msukumo tangu akiwa chuoni zaidi ya muongo mmoja uliopita.

“Kuwa na kitabu ni msukumo, lakini kukimaliza ni nidhamu ya kujituma,” alisema Nancy. “Bado naamini vitabu ni uchawi — na ndio chanzo cha hadithi nyingi tunazoziona zikibadilishwa kuwa filamu, vipindi vya televisheni na kazi za sanaa.”

Alibainisha kuwa zaidi ya nusu ya nchi za Afrika zimeanza kuimarisha mnyororo wa thamani wa uchapishaji na vitabu, jambo ambalo linafungua milango ya ubunifu katika filamu kupitia hadithi asilia za Kiafrika, simulizi za kihistoria na fikra za wabunifu.

Nancy alisisitiza kuwa kuunganisha sekta ya vitabu na filamu kutaleta mabadiliko makubwa: “Vitabu ni vyanzo vya kwanza vya script. Tukivithamini, tunauimarisha pia mustakabali wa filamu za Kiafrika.”

Kwa kuhitimisha, aliwataka wadau wa filamu, wachapishaji na waandishi kushirikiana zaidi, ili Afrika iwe na hadithi zinazovuka mipaka ya bara na kuonyesha utambulisho wake kwenye jukwaa la kimataifa.

Chapisha Maoni

Please Select Embedded Mode To Show The Comment System.*

Mpya zaidi Nzee zaidi