Dar es Salaam – Maonesho ya Tanzania Film, Festival and Awards (TAFFA) 2025 yamebeba sura mpya baada ya Play and Learn Africa (PAL Africa), taasisi inayojikita katika kukuza masomo ya STEAM (Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hisabati) kwa watoto, kuonyesha ubunifu wake unaochanganya elimu na sanaa.
Akizungumza wakati wa maonesho hayo, mwakilishi wa PAL Africa, Ali Lupatu, alisema taasisi hiyo inalenga kujenga uelewa wa vitendo kwa watoto kupitia mchanganyiko wa sayansi, hisabati, uhandisi, sanaa na ubunifu.
“Kwa mfano, tuna kitabu kinachoitwa She Garage, hadithi ya wahandisi wawili wadogo wa kike wanaofanya mabadiliko katika jamii yao kupitia uhandisi,” alisema Ali.
Kitabu hicho kinawasilisha simulizi kuhusu watoto waliopata hamasa ya uhandisi kutokana na magari yaliyokuwa yakipita kijijini kwao. Mbali na hadithi, kitabu kimeambatanishwa na shughuli za vitendo kama kukunja, kuchora na kufunga karatasi zinazomsaidia mtoto kutengeneza mfano wa gari.
“Hizi shughuli ni sehemu ya mchakato wa kujifunza, na kuwasaidia watoto kukuza uratibu wa ubongo, utulivu, fikra za ubunifu na umakini,” aliongeza Ali.
Mbali na vitabu, PAL Africa pia inatekeleza miradi ya kielimu kama robotics, coding na ubunifu mwingine, ikigawanywa kulingana na umri na kiwango cha umahiri wa watoto.
Pia, inaendeleza progrmau zake katika Sayansi ya Michezo ikiwemo michezo ya Mpira wa Kikapu (Basketball), mchezo wa ubao wa kuteleza kwenye theluji (Skateboarding) na mchezo wa kuteleza kwenye roller (Roller Skating)
Kwa miaka michache tu ya uwepo wake, ubunifu huu umevutia wengi, wakiwemo watoto wenye changamoto za kujifunza kama vile dyslexia na autism.
Lakini zaidi ya elimu, simulizi za PAL Africa zinatambulika kama mbegu ya sanaa na ubunifu kupitia mtindo wa STEAM. Sanaa yao ya uandishi wa vitabu inaoanisha na sayansi na maisha yetu ya kila siku na wapo katika maandalizi ya kuweka vitabu vyao kwenye Animation .
Kitabu cha She Garage, kwa mfano, kimeonekana kuwa na uwezo mkubwa wa kutafsiriwa katika filamu fupi au cartoon series za kuhamasisha watoto, sawa na filamu maarufu za kimataifa zinazochukua simulizi za vitabu vya watoto.
Kwa kuhusisha maudhui ya kisayansi na kijamii, PAL Africa inafungua milango kwa script writers, animators na film producers wa Tanzania na Afrika Mashariki kuibua kazi mpya zitakazohamasisha kizazi kipya kupitia hadithi za Kiafrika.
“Tunachofanya ni kuonyesha kwamba kujifunza kunaweza kuwa safari yenye furaha na hadithi hizi zinaweza kuishi zaidi ya kurasa, zinaweza kufika kwenye filamu na animation,” alisema Ali.
Hii inaleta mjadala mpya kwenye TAFFA: je, vitabu vya kielimu vya watoto vinaweza kuwa chanzo cha franchise kubwa za filamu Afrika, sawa na hadithi za Disney au Pixar zilivyotokana na simulizi rahisi za vitabu vya watoto?