Agness Suleiman Kahamba (Aggybaby) ashinda tuzo ya mwigizaji bora wa kike Afrika 2025

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Msanii wa muziki na filamu nchini, Agness Suleiman Kahamba, maarufu kama Aggybaby, ameshinda Tuzo ya Mwigizaji Bora wa Kike wa Mwaka 2025 kutoka Achievers Awards International ya nchini Nigeria.

Tuzo hiyo imetolewa kama kutambua mchango wake mkubwa katika tasnia ya filamu na huduma za kijamii kupitia taasisi yake ya Tupaze Sauti Foundation (Tanzania).

Waandaaji wa tuzo hizo wamesema wametambua ubunifu na ubora wa kazi za Agness, hususan kupitia tamthilia maarufu ya “Panguso”, “Huba” na filamu zingine zinazoendelea kusambaa mitandaoni YouTube.

Tuzo hiyo pia imetajwa kuwa ishara ya ushirikiano wa muda mrefu wa kifilamu kati ya Tanzania na Nigeria. 

Akizungumza baada ya ushindi huo, Agness alisema waandaaji wa tuzo hizo wamevutiwa na filamu kutoka Tanzania, wakibainisha kuwa zinatambulisha vyema utamaduni, amani na ushirikiano wa Kitanzania huku vikikuza utu wa Mwafrika.

Akinukuliwa, Agness alisema tamthilia ya “Kombolela” imekuwa mfano bora wa simulizi yenye kuonesha maadili na utu halisi wa kiafrika.

kwa upande mwingine, Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania (TFB), Dkt. Gervas Kasiga (PhD), amekutana na kufanya mazungumzo na msanii huyo katika ofisi za bodi hiyo jijini Dar es Salaam.

Katika mazungumzo hayo, Dkt. Kasiga amempongeza Agness kwa juhudi zake na kwa kuiwakilisha vyema Tanzania kwenye majukwaa ya filamu ya kimataifa.

Aidha, Dkt. Kasiga amemshauri Agness kuendelea kufanya kazi zake kwa ubunifu, nidhamu na weledi mkubwa, ili kuendelea kuitangaza vyema Tanzania na utamaduni wake kupitia sanaa ya filamu.


Chapisha Maoni

Please Select Embedded Mode To Show The Comment System.*

Mpya zaidi Nzee zaidi