Na Mwandishi Wetu
Mwanatasnia wa filamu na michezo ya kuigiza nchini, Bi. Stella Mbuge (@officialstellambuge), ameibuka kidedea baada ya kushinda Tuzo ya MVAA na kumfanya kuwa chipukizi kinara barani Afrika.
Tuzo hizo zimefanyika jijini Lagos, nchini Nigeria, tarehe 11 Oktoba 2025, ambapo Stella alitangazwa mshindi katika kipengele cha Mwigizaji Bora Chipukizi wa Mwaka – Best MVAA Upcoming Actress of the Year 2025.
Stella aliwania tuzo hizo kupitia tamthilia mbili alizocheza za “Nuru” na “Jiya.”
Akizungumza mara tu baada ya kutangazwa mshindi, Stella alisema kuwa asingeweza kufikia hatua hiyo bila kumtanguliza Mungu mbele.
“Namshukuru Mungu kwa kuniwezesha na kunikuza zaidi… juhudi pekee hazitoshi,” alisema Stella kwa hisia mchanganyiko akiwa jukwaani.
Katika hotuba yake fupi, aliwashukuru pia waandaaji wa tuzo hizo kwa kutambua na kuthamini kipaji alichokionesha.
Tuzo hii inaendelea kumuweka Stella katika ramani ya mafanikio katika filamu barani Afrika, huku ikimfungulia milango ya kupata fursa za kimataifa katika uigizaji.
Kwa upande mwingine, Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania, Dkt. (PhD) Gervas Kasiga (@chuma_kaole), ametoa pongezi rasmi kwa mrembo huyo kupitia ukurasa wa Instagram wa bodi hiyo, akisema:
"Umeiwakilisha vyema nchi yetu. Hongera! Hii ni ishara ya kukua kwa fursa wezeshi katika sekta ya filamu nchini.”
Stella anatarajiwa kurejea nchini muda mfupi baada ya kukamilika kwa hatua zote za mashindano hayo
