Na Mwandishi Wetu
Tamthilia pendwa ya Big Boss imeendelea kufanya vizuri na kuvutia watazamaji wengi ndani na nje ya Tanzania, kwa kuonwa na watu wanaokadiriwa kufikia milioni moja ndani ya wiki, tangu iachiwe kwenye mtandao wa YouTube siku chache zilizopita.
Tamthilia hiyo imepata umaarufu mkubwa kutokana na maudhui yake yanayogusa jamii, ikijikita katika simulizi za kijamii, fedha na changamoto za maisha halisi.
Muandaaji na mzalishaji wa Big Boss, Clam VEVO, amethibitisha kuwa maandalizi ya msimu wa pili yamekamilika, na unatarajiwa kuanza kuonekana katika robo ya mwisho ya mwaka huu.
Msimu wa pili mzima uliachiwa rasmi YouTube kuanzia Oktoba 18, 2025.
Wadau wa filamu wameipokea tamthilia hiyo kwa furaha kubwa, wengi wakisifu ubora wa kazi, uhalisia wa maudhui, na ubunifu wa waigizaji.
Wengine wameandika maoni kwenye mitandao wakisema “uhondo wa Dunia umeongezeka na sasa tunafaidi zaidi kupitia Big Boss.”
Katika mahojiano maalum, Clam VEVO alisema kuwa dhamira yake ni kufanya filamu kwa ubunifu na utambulisho wake binafsi bila kujilinganisha na mtu yeyote.
"Mimi sijifananishi na Kanumba wala mtu mwingine yeyote. Yeye atabaki kuwa bora kwenye kizazi chake, na mimi ninajitahidi kupush kwa sasa,” alisema Clam VEVO.
Tamthilia hiyo inaendelea kupata watazamaji wengi barani Afrika na nje ya mipaka, huku ikipambanishwa na baadhi ya tamthilia kubwa za kiswahili.
Clam VEVO aliwashukuru mashabiki na watazamaji wote wanaoendelea kufuatilia kazi zake, akisisitiza kuwa ushiriki wao unachangia ukuaji na maendeleo ya sekta ya filamu nchini.
