Naipa Atingisha YouTube na “Msitu” Tamthilia bora ya Akili unde (AI)


 Na Mwandishi Wetu

Abduli Yusuph, maarufu kama Naipa, amekuwa gumzo kubwa mitandaoni baada ya tamthilia yake mpya ya Msitu kufikisha watazamaji zaidi ya 50,000 ndani ya saa 24 tu kwenye YouTube idadi ambayo hata baadhi ya misitu haipati wageni wengi kwa siku.

Tamthilia hiyo imepokelewa kwa sifa nyingi kutokana na ubora wa uigizaji, msisimko wa simulizi, pamoja na matumizi ya akili unde (AI) na akili mnemba, yaliyoongeza ladha ya kisasa kwenye kazi yake.

Lakini kabla ya mafanikio haya, safari ya Naipa haikuanza kwenye filamu.

“Nilikua nafanya muziki, na ndipo jina la Naipa lilipozaliwa. Baada ya kuacha muziki miaka michache iliyopita, nikaanza kuwaza kutengeneza short films” anasimulia.

Mwaka 2024, ndipo alipoanza rasmi safari ya filamu akiwa Masumbwe, wilaya ya Mbogwe mkoani Geita, kabla ya kuhamia Kahama, ambako anaishi hadi leo.

Anaeleza kuwa kufanya filamu katika ukanda wa ziwa si kazi rahisi.

“Changamoto kubwa ni uhaba wa wasanii wanaochukulia uigizaji kama kazi. Wengi wanafanya kwa sababu wanapenda kuonekana tu, si kwa sababu wanaona thamani ya sanaa kama taaluma,” anasema.

Mbali na hilo, kupata maeneo ya kurekodi (locations) pia ni mtihani mwingine.

“Leo unaweza kuruhusiwa kurekodi, kesho unaambiwa hapana. Watu bado hawaamini sana kwenye maigizo,” anaongeza.


Kwa upande wake, Msitu (2026)  ni moja ya kazi kubwa zaidi alizowahi kufanya.

“Hii inanipa pongezi kubwa kwa sababu nimeshuti na kuedit mwenyewe hadi kazi ikawa sawa. Nimepongezwa hata na maafisa utamaduni kwa jinsi nilivyorekodi msituni, ni kweli imeleta hamasa kuwa tunaweza kulinda miti na mazingira yetu” anasema kwa fahari.

Anasisitiza kuwa mafanikio haya siyo tu kutokana na idadi ya watazamaji, bali zaidi maoni chanya kutoka kwa mashabiki.

Swali: Kwenye kazi hii umetumia akili unde na akili mnemba. Umewezaje kufanikisha hili?

Naipa: Watu wanafikiria AI ni kitu rahisi, lakini kila kitu kina maandalizi makubwa sana.

Swali: Kivipi?

Naipa: AI inakusaidia, lakini bado wewe ndio mwenye kazi ya kuiongoza vizuri. ni sawa na kuendesha gari.. Kila clip niliyoitumia, AI ilisaidia labda kwa asilimia 10 tu. Nilitumia zaidi ya programu tatu za AI, zaidi ya apps tano za editing, na bado nikatumia akili nyingi sana hasa kwenye mipangilio ya kamera, settings, shots, kila kitu."

Kwa sasa, Naipa anafanya kazi peke yake bila mdhamini, bila executive producer, na wala bila ufadhili wowote.

“Ninajikongoja mwenyewe. Kamera ninayotumia ni ya gharama, inalipiwa. Natamani kupata vifaa vikubwa zaidi na crew ya wataalamu ili kuboresha ubora wa kazi,” anasema.

Anaongeza kuwa kazi aliyoitoa sasa ni kama robo tu ya mawazo aliyonayo.

“Nataka kufanya kazi kubwa zaidi, ngumu zaidi, na itakayodumu kwa muda mrefu. Ndiyo maana natumia muda mwingi kupanga.”

Swali: Je, una mpango wa kupokea volunteers?

Naipa: Kwa sasa bado najifunza sana. Sijafika hatua ya kufundisha wengine bado, lakini baadae huenda ikawezekana.


Swali: Msitu ipo live YouTube. Je, itabaki huko au utaifikiria iende kwenye masoko makubwa kama Netflix?

Naipa: Nina ndoto za kupata pesa nyingi sana kupitia sanaa. Bado najifunza, bado nakua. Kama Mungu atanipa fursa kubwa zaidi, nitaipokea.

Swali: Msitu inatarajiwa kuwa na misimu mingapi na episodes ngapi?

Naipa: Kwa sasa sijajua (anacheka). Tuna mpango wa kutengeneza episodes nyingi kadri itakavyowezekana, nyingi sanaa mpaka Watazamaji wetu watuchoke (anacheka tena). Hii ni elimu kuhusu miti, misitu na mazingira, na ni elimu endelevu inayodumu kizazi hadi kizazi.

Swali: Baada ya Msitu, kuna kazi nyingine?

Naipa: Ndiyo, tuna mambo mengi sana ya kuonesha. Msitu itaendelea, na kazi nyingine zinakuja.

Naipa ametoa shukrani kwa wadau wote wa filamu nchini, ikiwemo sekta husika, Bodi ya Filamu Tanzania, Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, BASATA, na wadau wengine.

“Nawashukuru watazamaji kwa kunipokea vyema. Maoni yenu na utazamaji wenu vinanipa nguvu na kuniboresha zaidi. Naomba muendelee ku-subscribe na kufollow Naipa Films,” anasema.

Pia ametoa wito kwa Serikali kuendelea kuboresha mazingira ya kazi kwa watengenezaji filamu, ikiwemo kupitia semina, mafunzo na elimu ili kazi zinazotengenezwa ziwe na tija kwa jamii na taifa.


Swali: Je, una mpango wa kukata vipande vifupi kama reels au zitabaki YouTube?

Naipa: Shorts zipo, maana mashabiki wanapenda kuona matangazo ya TikTok, Facebook, Instagram na hata WhatsApp. Sina shida, mradi mwisho wa siku wote tukutane YouTube na kupeana sapoti.

Anahitimisha kwa kusema:

“Mashabiki wasiwe wachoyo angalia burudani hii na umsambazie mwenzako. Kizuri kula na ndugu yako.”

Chapisha Maoni

Please Select Embedded Mode To Show The Comment System.*

Mpya zaidi Nzee zaidi