JUMIKITA yalaani kauli ya “Media Uchwara”, Madam Rita aomba radhi, mjadala waibuka Mtandaoni


 Na Mwandishi wetu, mitandaoni

Jumuia ya Wanahabari wa Mitandao ya Kijamii (JUMIKITA) imelaani kauli iliyodaiwa kutolewa na Madam Rita dhidi ya vyombo vya habari, huku mhusika huyo akiomba radhi kufuatia tukio hilo lililozua mjadala mkubwa mtandaoni.

Tukio hilo linadaiwa kutokea wakati wa hafla ya Miss World Tanzania 2026 iliyofanyika katika ukumbi wa Superdome Masaki, ambapo baadhi ya wanahabari waliripoti kuitwa “media uchwara” walipokuwa wakifanya jitihada za kufanya mahojiano.

Kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa na chombo cha habari cha mtandaoni, Mike 360, timu yao pamoja na vyombo vingine walimfuata Madam Rita kwa ajili ya mahojiano baada ya hafla hiyo, lakini walidai mazungumzo hayo yalikatizwa kufuatia kauli hiyo.

Katika taarifa yake, Mwenyekiti wa JUMIKITA, Shaaban Matwebe, alisema kitendo hicho ni kinyume na maadili ya taaluma ya habari na kinapaswa kukemewa.

Hata hivyo, katika chapisho lililowekwa takriban saa tatu zilizopita kwenye ukurasa wa Instagram wa Rita Paulsen na kusambazwa pia na vyombo mbalimbali vya habari ikiwemo ITV Tanzania, Madam Rita ameomba radhi hadharani.

“Binadamu tunaumbwa kukosea na mimi jana bila kutarajia niliteleza, naomba radhi kwa Mike 360 media na kwa kila aliyekwazika kwa kauli yangu ambayo niliisema huku nikiwa na mood mbaya,” alisema.

Tukio hilo limezua mjadala mpana kwenye mitandao ya kijamii, ambapo baadhi ya watumiaji wamekosoa kauli hiyo, huku wengine wakipokea ombi la radhi kwa mitazamo tofauti.

Chapisha Maoni

Please Select Embedded Mode To Show The Comment System.*

Mpya zaidi Nzee zaidi