Rais Samia aongoza maombolezo ya kifo cha msanii Hashim Kambi

 


Na Mwandishi wetu

Tanzania ipo kwenye maombolezo kufuatia kifo cha muigizaji mkongwe wa filamu Hashim Kambi, aliyefariki dunia Jumatatu jijini Dar es Salaam.

Rais Samia Suluhu Hassan ameongoza salamu za rambirambi, akieleza masikitiko yake makubwa na kusema taifa limepoteza kipaji adhimu kilichochangia kwa kiasi kikubwa kukuza na kuitangaza tasnia ya filamu nchini.

“Nimepokea kwa masikitiko taarifa ya kifo cha mwigizaji mkongwe wa filamu nchini, Hashim Kambi… Taifa limepoteza kipaji adhimu,” amesema Rais katika salamu zake, huku akitoa pole kwa familia, wasanii na wadau wa filamu.

Kwa mujibu wa taarifa, Kambi alifariki katika Hospitali ya MICO, Sinza, baada ya kuugua ghafla akiwa kwenye shughuli za kurekodi. Kifo chake kimethibitishwa na Shirikisho la Filamu Tanzania.

Enzi za uhai wake, Kambi alikuwa miongoni mwa waigizaji waliotambulika sana katika tasnia ya filamu za Tanzania, akicheza katika kazi mbalimbali ikiwemo Homecoming, Handsome wa Kijiji na Twisted.

Kabla ya kujikita katika sanaa ya uigizaji, pia alikuwa mchezaji wa soka wa klabu ya Young Africans Sports Club, moja ya timu kubwa nchini.

Taasisi mbalimbali zikiwemo Baraza la Sanaa Tanzania zimeeleza kuwa kifo chake ni pigo kubwa kwa tasnia ya ubunifu nchini.

Kifo chake kimeacha pengo kubwa katika tasnia ya filamu, huku wasanii na mashabiki wengi wakimkumbuka kwa mchango wake mkubwa na urithi aliouacha katika sanaa ya Tanzania.

Chapisha Maoni

Please Select Embedded Mode To Show The Comment System.*

Mpya zaidi Nzee zaidi