Tasnia ya filamu mkoani Mbeya ipo kwenye majonzi kufuatia taarifa za kifo cha msanii wa filamu Yohana Mwakapalila maarufu kwa majina ya Plezdar au MC Mwakapalila, aliyefariki dunia jioni ya leo baada ya kupata ajali.
Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na watu wa karibu na marehemu, Plezdar alikuwa akisindikiza basi kama sehemu ya shughuli zake za kazi ya uajenti wa mabasi kabla ya kupata ajali hiyo katika eneo la Mswiswi mkoani Mbeya.
Mbali na kujulikana kama muigizaji wa filamu, marehemu alikuwa pia akijihusisha na shughuli za uajenti wa mabasi, jambo lililomfanya kufahamika kwa watu wengi ndani na nje ya tasnia ya sanaa.
Aidha, marehemu alikuwa Kiongozi wa Chama cha Waigizaji Wilaya ya Mbeya Mjini (TDFAA), ambapo alitambulika kwa mchango wake katika kuunganisha na kutetea maslahi ya wasanii wa filamu mkoani humo.
Taarifa za awali zinaeleza kuwa Plezdar ameacha mke na mtoto mmoja.
Kifo chake kimewaacha katika majonzi wasanii, marafiki pamoja na mashabiki waliokuwa wakifuatilia kazi zake mbalimbali za sanaa mkoani humo.
Mpaka sasa, taarifa zaidi kuhusu chanzo kamili cha ajali hiyo pamoja na taratibu za mazishi bado hazijatolewa rasmi na familia au mamlaka husika.
Sauti za Filamu inaendelea kufuatilia taarifa zaidi kuhusu msiba huo