Baada ya ukimya wa muda mrefu uliowaacha wengi wakijiuliza kama bado yupo kwenye mchezo, Haji Adam hatimaye amefungua pazia la kurejea kwake, na safari hiyo inaanza na tamthilia mpya ya Siri Yako, kazi anayoiita si tu comeback, bali ni kauli ya kisanii kuhusu maisha halisi ya Mtanzania, hadithi zenye uzito, na sinema inayoweza kuishi kwa muda mrefu zaidi
Katika mahojiano maalum na Sauti ya Filamu, Haji Adam alizungumza kwa utulivu wa mtu anayejua uzito wa jina lake kwenye tasnia. Swali la kwanza lilikuwa lile ambalo mashabiki wengi wamekuwa nalo: kwa nini alikuwa kimya kwa muda mrefu?
“Ni ukweli ulio wazi kwamba nilikuwa kimya kwa muda mrefu kidogo. Nilikuwa natafakari namna ya kazi nzuri iwe ya kwangu au ya mtu mwingine, lakini lazima iendane na hadhi yangu na vile watu wanavyonijua.” alianz kusema kwa utulivu
Safari yake kwenye sanaa ilianza mwaka 1998, akiwa na ndoto kubwa za kuifanya filamu kuwa sehemu ya maisha yake.
“Napenda kuji-involve kwenye kazi ambayo ninaona ina tija. Kwanza kipato, pili ubora wa kazi yenyewe. Script nzuri, wazo zuri, na wazo hilo lishabihiane na Utanzania wetu, ule utamaduni wetu na namna tunavyoishi.”
Tangu hapo amejijengea uzoefu wa karibu miongo mitatu, akipitia hatua mbalimbali za ukuaji wa Bongo Movie kutoka zama za VCD hadi sasa kwenye mambo haya ya YouTube na streaming.
Kwa mujibu wa Haji Adam, tamthilia hii imejengwa juu ya msingi wa uhalisia wa maisha ya Watanzania wa kawaida, watu wa daladala, vijijini, mitaa ya mabondeni, nyumba za kawaida, na mapambano ya kila siku.
anabainisha wazi kuwa yeye sio wa kupendelea “kuonekana kwenye sofa na staircase za kifahari.”
Kwa maelezo yake, anasema kuwa ujio huu ni ule wa kupendwa na wengi, uhalisia wa maisha halisi. maisha ya tope, mvua, kijiji, nyoka, ziwa, na sauti ya Mtanzania wa leo. na zingatia sana neno nyoka, maana utanielewa vizuri baadae.
“Sikutaka kujifananisha na maisha ya Waingereza au Marekani. Hadithi hii imezungumzia maisha halisi ya Mtanzania wa leo na wa kesho.” alisisitiza.
Kwenye moja ya maswali muhimu zaidi, tulimuuliza: ni ubora gani watazamaji wautarajie tofauti na kazi nyingine?
“Tulizingatia ubora wa hadithi kwanza. Tukahakikisha sauti iwe nzuri sana, mtu akisikika asikike kwenye ubora wa hali ya juu. Lakini pia ubora wa picha, na acting yenyewe tukaitaka ifanane na uhalisia. Mtazamaji atazame aone kwamba hata kinachotokea, angekuwa yeye angefanya kama hivyo.”
Na hapa ndipo exclusive inakuwa tamu zaidi.
Tulipoingia kwenye upande wa mazingira ya shooting, Haji Adam alifunguka jinsi walivyolazimika kwenda kijijini kutafuta mazingira halisi, badala ya kutegemea set za mjini.
“Tulitaka kijiji halisi. Tukitaka kilima tukipate, tukitaka mto tuupate. Tukakutana na tope nyingi, mvua, mazingira magumu, lakini tukasema haya ndio maisha yetu.”
Katika baadhi ya scene, crew ilikutana hata na nyoka halisi wenye sumu, na hapa Haji Adam aliisimulia kwa namna ambayo tayari unaweza kuyaona haya yote kuanzia episode ya saba.
“Yule mkamataji nyoka akasema wekeni kamera tatu hapa, mimi nitaishi naye. Akasema kuwa Nyoka huyu hapendi kelele, ukitikisika tuu ni shida.”
Kwenye swali la ushirikiano, Haji Adam aliweka wazi kabisa nafasi ya Kitale, ambaye ndiye muongozaji wa tamthilia hio.
“Namheshimu sana Kitale, ameongoza vizuri sana, sikutegemea kama angeongoza jahazi namna hii, na kama wananchi wakimpendekeza kutunukiwa tuzo ni kweli anastahili. Kitale anasimamia sana maandishi. Kila neno lililoandikwa atahakikishwa lisemwe kama lilivyo kwa sababu lina maana yake.”
Akiwazungumzia wasanii vijana, Haji Adam alisisitiza kuwa tasnia inaweza kulipa vizuri iwapo itaendeshwa kwa nidhamu, mipango na uelewa wa soko.
Kwenye moja ya mahojiano, tulimgusia kuhusu mjadala wa sasa wa short-form content, reels, vibonzo na YouTube clips, huku wengine wakiamini tamthilia ndefu zimepitwa na wakati.
“Vibonzo ni upepo tu, unapita. Filamu haiwezi kuondoka duniani. Content fupi inamhitaji mtu mwenye stress ajisahaulishe kwa muda mfupi. Lakini filamu na series zinaeleza maisha halisi, mabadiliko.”
Tulipofika kwenye mustakabali wa tasnia, Haji Adam alizungumza kwa matumaini kuhusu mikopo na uwekezaji kupitia Bodi ya Filamu, akisema sasa wasanii wana nafasi ya kufikiria soko la nje.
“Kukuza sinema zetu ziende abroad lazima inahitaji mtaji, na sasa mtaji upo. Tunaweza kwenda Nigeria, Ghana, South Africa na kufanya kazi na wasanii wa kule.”
Na hii ndiyo philosophy yake kubwa: sanaa si hobby, ni biashara.
“Kijana aje kwenye sanaa kwa lengo kuu la kutafuta fedha. Hobby mwisho wake ni majuto.”
Kwa mashabiki waliom-miss kwa muda mrefu, Haji Adam alikuwa na ujumbe wa moja kwa moja.
“Mashabiki wangu bila wao mimi nakuwa sipo. Walionielewa toka zamani nawapenda, na wale wapya waje pamoja nami kwa sababu baada ya Siri, vitu havitakauka.”
kutoka kwenye namna alivyoelezea uhalisia, mazingira, Kitale, nyoka halisi, village cinematography, na ndoto za tuzo za dunia, Siri haionekani kama comeback ya kawaida.
“Sitaki kumfanya shabiki anayenipenda aonekane kama mjinga. Nataka aone kwamba ninamthamini na kila muda anaoutumia kunitazama una thamani sana"
Kwa sasa, macho ya mashabiki yapo ijumaa hii, Aprili 3, wakisubiri kuona kama Siri Yako itakuwa moja ya tamthilia zitakazorejesha ule msisimko wa kukaa mbele ya TV mapema kabla hata intro haijaanza.