Mwili wa Director Nyanza wafukuliwa ndani ya nyumba yake baada ya Kupotea kwa siku kadhaa


Na Charles Mkoka

Tukio la kushtua limeibuka eneo la Chanika Zingiziwa, jijini Dar es Salaam, baada ya mwili wa Dairekta anayejulikana kwa jina la Athumani Nyanza kufukuliwa ndani ya nyumba yake mwenyewe, siku sita tangu atangazwe kupotea.

Muongozaji huyo, ambaye ni maarufu miongoni mwa wasanii na waandaaji wa kazi za filamu nchini, akifanya kazi nyingi sana na Msanii Madebe Lidai, amedaiwa kupatwa na maswahibu hayo ya kusikitisha nyumbani kwake mwenyewe huku mwanamke aliyewahi kuwa na mahusiano naye, akihusishwa kwenye mkasa huu.

AyoTV imeripoti kwa undani zaidi, ikisema kuwa mwili wa marehemu Othman Nyanza ulipatikana tarehe 16 Machi 2026 majira ya jioni, ukiwa umefukiwa chini ya baraza la nyumba, hali iliyozua taharuki kwa familia, majirani na wadau wa karibu waliokuwa wakifuatilia kupotea kwake tangu tarehe 10 Machi mwaka huu.

Kwa mujibu wa rafiki wa marehemu ambaye ni msanii Madebe Lidai, safari ya kutafuta ukweli ilianza baada ya mawasiliano ya Nyanza kukatika ghafla jioni ya tarehe 10 Machi, alipokuwa ameenda Kigamboni kumuona mwanamke wake.

Siku iliyofuata, hali ilianza kuzua mashaka zaidi baada ya mwanamke huyo kuonekana nyumbani akifanya usafi usiku wa manane, huku akitoa maelezo tata kuhusu alipo marehemu.

“Nilipofika pale niliona shimo limechimbwa barazani. Nilipomuuliza, akasema wanafanya usafi wa taka… lakini moyo wangu haukuridhika,” alisimulia Msanii Madebe, akiongea kwenye mahojiano yake maalum na AyoTV.


Kadri siku zilivyopita, hali ilizidi kuwa ya kutatanisha. Ujumbe wa simu uliodaiwa kutoka kwa marehemu ulitumwa kwa ndugu ukieleza kuwa ameuza nyumba na kukimbia baada ya kufanya tukio kubwa, jambo lililoibua maswali mengi.

Katika mahojiano hayo, Msanii Madebe Lidai ameelezea kuwa uchunguzi wa familia ulibaini kuwepo kwa mikataba ya mauziano ya nyumba yenye utata, ikionyesha thamani tofauti (milioni 30 na milioni 18), bila kusainiwa na mwanasheria, na mapungufu mengine mengi, ikiashiria udanganyifu wa kitapeli.

Hatua hiyo ilizua tuhuma za uwepo wa njama za kudhulumu mali ya marehemu.

Mwanamke anayeishi na marehemu ndiye anayetajwa kuwa mtuhumiwa mkuu wa tukio hilo. Inadaiwa alikamatwa na polisi baada ya kuonekana akiuza mali za ndani ya nyumba na kujaribu kutoroka.

akiendelea kusimulia, Madebe aliendelea kusema kuwa hata hivyo, baada ya kupewa dhamana, mshukiwa huyo alitoroka na kutokomea kusikojulikana, hali iliyozidisha mashaka ya kuhusika kwake na tukio hilo.

Polisi kwa sasa wanamshikilia mmoja wa wadhamini wake huku wakiendelea na msako mkali wa kumtafuta.


Katika upekuzi wa nyumba hiyo, familia na mashuhuda walibaini uwepo wa vifaa vinavyodaiwa kuhusiana na uganga, ikiwemo kilinge na mavazi maalum.

Madebe alidai kuwa marehemu aliwahi kueleza kuwa mwanamke huyo alikuwa akijihusisha na masuala ya tiba za asili na uganga, jambo ambalo limeingizwa katika mstari wa uchunguzi kama sehemu ya mazingira ya tukio.

Baada ya shinikizo kutoka kwa familia, polisi waliruhusu eneo la tukio kufukuliwa, hatua iliyopelekea kupatikana kwa mwili wa marehemu ukiwa umekunjwa, umefungwa kamba na kufukiwa ndani ya kiwanja, nje kidogo ya nyumba yake mwenyewe.

Ugunduzi huo ulithibitisha hofu ya muda mrefu ya ndugu na kugeuza tukio hilo kuwa kesi ya mauaji yenye utata mkubwa.


Tarehe 19 Machi, Muongozaji @ally_njenje amethibitisha na kuandika kwenye mitandao yake ya kijamii kuwa mtuhumiwa amekamatwa na kushikiliwa na kituo cha polisi chanika.

"Mtuhumiwa Amekamatwa Akiwa yupo katika mkoa wa Morogoro na sasa yupo kituo cha polisi chanika, Shukrani kwa kila mtu alieshiriki na sasa jambo hili lipo chini ya polisi nasi tubaki kumuombea marehemu Mungu ampunguzie Adhabu ya Kaburi"

Baba mdogo wa Marehemu, Simba Nyanza, baada ya kuhojiwa na AzamNews amesema kuwa anaamini chanzo cha tukio hilo kimesababishwa na kutaka kuuzwa kwa nyumba hiyo ya marehemu.

"chanzo hasa inavyoonekana ni mwanamke alikuwa na tamaa ya kutaka kuuza nyumba, hata tulivyofuatilia, alifikia hatua ya kufoji hati, na alipofanikiwa kufoji ndipo alipofanya tukio hilo, hata tulivyombana (pamoja na polisi), mwenyewe alikiri kuwa hati ile ilikuwa feki, na mpaka hivi sasa tunafanya utaratibu huyo jamaa wa Zanzibar aliojifanya amenunua nyumba apatikane" aliongezea.

Majirani wameshuhudia zoezi zima la uchimbaji wa shimo hilo, na kuelezea kwenye vyombo vya habari kuwa lilikuwa na sintofahamu nyingi.


"Kipindi walivyochimba ilikuwa vigumu kujua kama ni kwa ajili gani. Tuliona ila hatukujua, maana walichimba jioni hadi kiza kilipoingia" alisema mama jirani ambaye hakuweka wazi jina lake.

Rajabu AbdiSwalehe, Mjumbe wa serikali ya mtaa wa Rubakaya amesema kuwa kwa mazingira yalivyokuwa, marehemu aliuawa sehemu ingine na kisha kufukiwa eneo hilo.

"Hakumuulia hapa, inawezekana aliuliwa huko kwao kigamboni ndio amekuja naye hapa kumfukia. Sasa majirani wengine wanadai imechukua siku chache, wengine wanadai tukio limefanyika zaidi ya siku 29." aliongezea Mjumbe huyo, katika mahojiano yake na vyombo vya habari.

Mwili wa marehemu unatarajiwa kuzikwa Kiare, Kisarawe mkoani Pwani, baada ya kukamilika kwa uchunguzi wa kitabibu (post-mortem).

Polisi wamethibitisha kutokea kwa tukio hilo katika ripoti ya Afande Murillo leo tar 20 machi, na kumtaja Rehema Maulidi (42) mkazi wa kigamboni na mwingine ambaye jina lake limehifadhiwa

Ripoti hiyo iliosomwa na Murilo mwenyewe imesema kuwa wanaendelea na uchunguzi ili kuwabaini washiriki wote wa tukio hilo.

Chapisha Maoni

Please Select Embedded Mode To Show The Comment System.*

Mpya zaidi Nzee zaidi